
Wito wa Baku wa Kuchukua Hatua
Wito huu ulioundwa kupitia sauti kutoka nchi 176, unaweka njia ya pamoja ya kusonga mbele, ikiwa ni pamoja na:
• Kutazama upya suala la makazi kama mfumo kamili, kwa kuunganisha nyumba na ardhi, miundombinu, usafiri, huduma na fursa za kiuchumi badala ya kuangalia ujenzi pekee kwa kujitenga.
• Kukabiliana na shinikizo zinazohusiana – kuanzia kupanda kwa gharama na biashara ya kubahatisha ya ardhi hadi kuhama kwa watu, usimamizi dhaifu na majanga ya tabianchi – kupitia suluhisho jumuishi yanayomweka mwanadamu katikati.
• Kutambua kwamba haki ya makazi na haki ya tabianchi haviwezi kutenganishwa, huku jamii zilizo hatarini zaidi zikikabiliwa zaidi na mafuriko, joto kali na hatari za mazingira.
• Kupanua makazi yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kupitia majawabu ya kiasili, ukarabati wa majengo, kuboresha makazi yasiyo rasmi na kuimarisha maandalizi dhidi ya majanga.
• Kubadilisha ahadi kuwa vitendo, kupitia utawala imara wa ngazi mbalimbali, kuongeza ufadhili, kuboresha takwimu na kuunga mkono zaidi suluhisho zinazoongozwa na jamii za wenyeji.
‘Hakuna njia’ bila miji na makazi
“Hakuna njia ya kufanikisha Ajenda ya 2030 bila miji endelevu na makazi bora,” amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, akifunga jukwaa hilo lililoanza tarehe 17 mwezi Mei mwaka huu.
Amesema kuwa jukumu lililopo sasa ni kujenga miji inayojumuisha watu wote, yenye ustahimilivu na yenye uwezo wa kutoa makazi salama na fursa kwa kila mtu, huku ikihakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Kwa Amina Mohammed, mgogoro wa makazi uko katikati ya karibu kila changamoto kubwa ya dunia – kuanzia umaskini na ukosefu wa usawa hadi mabadiliko ya tabianchi, migogoro na ukosefu wa utulivu.
“Makazi bora huleta maji safi na huduma za usafi wa mazingira. Nishati ya kupika chakula, kupasha joto au kuangaza chumba. Ni kuhusu uwezo wa kumudu gharama. Usalama. Uhakika wa umiliki,” amesema.
Ameongeza kuwa miji ni “muundo wa vipaumbele” – unaoonesha kile ambacho binadamu wamechagua kujenga, jinsi wanavyojenga na kwa ajili ya nani.
Jaribio kwa ushirikiano wa kimataifa
Naibu Katibu Mkuu pia ameonya kuwa Kongamano hilo lilifanyika katika kipindi kigumu kwa ushirikiano wa kimataifa.
“Maadili na misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa vinadhoofishwa. Mivutano imeongezeka na imani inapotea. Mgawanyiko unaongezeka,” amesema.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa ushirikiano ndio njia pekee ya kushughulikia changamoto za kiwango hiki, hasa kupitia mamlaka za mitaa.
“Serikali za mitaa ndizo zinazopokea simu wakati dhoruba inapopiga. Ndizo zinazotoa maji, usafiri, makazi na kazi zenye hadhi.”
Wakati muhimu kwa makazi
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat, Anacláudia Rossbach, amesema kongamano hilo limetuma “ujumbe wenye nguvu na wa pamoja” kuhusu dharura ya kuchukua hatua.
“Tuko katika wakati wa maamuzi kwa mustakabali wa makazi. Hatuwezi tena kumudu anasa ya kutokuchukua hatua,” amesema.
Kutoka ahadi hadi utekelezaji
Katika Kongamano lote, kulikuwa na makubaliano mapana kwamba ahadi za kisiasa lazima ziendane na suluhisho za vitendo.
Katika mahojiano na UN News, Francine Pickup, Mkuu wa ujumbe wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP kwenye mkutano huo, ameeleza kuwa upatikanaji wa ufadhili ni changamoto kuu, hasa kwa miji midogo na ya kati.
“Nadhani ufadhili ni sehemu muhimu sana,” amesema, akitaja mradi huko Punjab, ambako ruzuku za umma, mikopo nafuu na uwekezaji wa sekta binafsi viliunganishwa kupanua upatikanaji wa makazi kwa familia za kipato cha chini na cha kati.
Ameongeza kuwa UNDP na Muungano wa Ulaya, wamefanya kazi na karibu manispaa 400 katika nchi za Ushirikiano wa Mashariki kusaidia mamlaka za mitaa kubuni suluhisho zinazomweka mwananchi katikati na kuvutia uwekezaji.
Baku yakabidhi kijiti
Kikao kijacho, WUF14, kitafanyika nchini Mexico mwaka 2028, huku nchi wanachama zikialikwa kuonesha nia ya kuandaa Kongamano hilo mwaka 2030.
Mkutano uliandaliwa kwa pamoja na UN-Habitat kwa kushirikiana na serikali ya Azerbaijan, na kukutanisha washiriki zaidi ya 57,000 kutoka nchi 176, wakiwemo zaidi ya 3,000 waliohudhuria mtandaoni.
