
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ameteua watatu kuongoza bodi mbalimbali, akiwemo Dk Irene Isaka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Wengine walioteuliwa ni Ludovick Nduhiye, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na Jamhuri Ngelime, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Taarifa ya uteuzi huo, imetolewa leo, Ijumaa Mei 22, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.
Uteuzi wa Mwenyekiti wa PSSSF, unakuja siku nane tangu Rais Samia aivunje bodi hiyo, iliyokuwa inaongozwa na Joyce Mapunjo, aliyeiongoza kwa miezi 14.
