
Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kupanda kwa bei za mafuta duniani hakuendelei kuwa mzigo kwa wananchi, huku ikionya wafanyabiashara wanaotumia hali hiyo kuongeza bei za bidhaa kiholela bila kuzingatia uhalisia wa gharama za uzalishaji na usafirishaji.
Kauli hiyo imekuja wakati ambao Watanzania wameendelea kukabiliwa na ongezeko la gharama za maisha kama vile kupanda kwa nauli, gharama za usafirishaji wa mizigo na bei za bidhaa muhimu ikiwemo vyakula.
Katika kipindi hicho, bei za mafuta nchini zimefikia zaidi ya Sh4, 000 kwa lita, jambo linalowafanya baadhi ya watu kuanza kutafuta njia mbadala za kupunguza matumizi ya mafuta, ikiwemo kufunga mifumo ya gesi asilia kwenye magari.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Mei 22, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, katika mkutano wa wadau kuhusu mashauriano kuhusu athari za mabadiliko ya bei ya mafuta duniani.
Amesema Serikali haiwezi peke yake kubeba mzigo wa changamoto hiyo kupitia ruzuku au kupunguza tozo bila ushirikiano wa wadau wengine wa uchumi.
Profesa Kitila, amesema ni muhimu kwa sekta binafsi kushiriki katika kuhakikisha bei za bidhaa zinapangwa kwa uwajibikaji, huku wakiboresha ufanisi wa minyororo ya ugavi na kuwekeza katika ubunifu utakaopunguza gharama za usafirishaji.
“Ndiyo maana tunahitaji ushirikiano wa jamii nzima, si Serikali pekee. Sekta binafsi ina wajibu mkubwa kuhakikisha inawajibika kupanga bei, kuboresha ufanisi wa minyororo ya ugavi na kuwekeza katika ubunifu unaopunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji,” amesema.
Amesema Serikali haitarajii kuona wafanyabiashara wakitumia mgogoro huo kama sababu ya kuongeza bei kiholela kwa bidhaa ambazo hazijaathiriwa moja kwa moja na gharama za mafuta.
“Hatutarajii wafanyabiashara kutumia mgogoro huu kama kisingizio cha kuongeza bei kiholela. Kwa sababu sasa hata bei ya baiskeli inapopanda, ukiuliza kwa nini wanaongeza bei, wanajibu ni kwa sababu ya mgogoro wa Iran, si sawa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka za udhibiti nchini kuongeza uwazi katika soko pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa bei ili kuzuia vitendo vya unyonyaji dhidi ya wananchi.
Mbali na hatua za muda mfupi, amesema Serikali imeanza kufikiria mikakati ya muda wa kati na mrefu, itakayosaidia kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nchi chache.
Amesema Serikali pia itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika Mashariki katika uwekezaji wa miundombinu ya kusafisha mafuta ndani ya ukanda huo ili kupunguza utegemezi.
“Hata nchi zinazozalisha mafuta bado husafirisha mafuta ghafi nje ya Afrika. Hivyo mgogoro huu unatukumbusha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika viwanda vya kusafisha mafuta ndani ya bara letu,” amesema.
Profesa Kitila, amesema mjadala mpya umeanza kuhusu uwezekano wa kujengwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta ama Tanga nchini Tanzania au Mombasa nchini Kenya, hatua inayolenga kuongeza usalama wa nishati hiyo Afrika Mashariki.
Aidha, amesema hali hiyo imeonyesha umuhimu wa kuimarisha biashara ndani ya Afrika kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), akisisitiza bara hilo lina uwezo wa kuwa kitovu cha biashara ya nishati, endapo litawekeza katika miundombinu na uzalishaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Tausu Kida amesema tathmini ya kitaalamu inaonyesha kuna maeneo matatu muhimu yanayohitaji uangalizi wa karibu katika kipindi kilichopo.
Ametaja eneo la kwanza ni ufuatiliaji wa viashiria vya uchumi kama bei za mafuta, chakula, upatikanaji wa mbolea, gharama za usafirishaji, mwenendo wa ubadilishaji fedha na ustawi wa kaya.
Pili, amesema kuna umuhimu wa kuunganisha hatua za haraka za kupunguza madhara ya kiuchumi na mageuzi ya muda wa kati yatakayosaidia kuimarisha uzalishaji wa ndani, mifumo ya usafirishaji na usalama wa nishati.
Amesema eneo la tatu ni kuhakikisha sera za muda mfupi haziharibu uendelevu wa kifedha wala kuathiri utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Shigeki Komatsubira amesema athari za ongezeko la bei za mafuta zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa kaya zenye kipato cha chini.
Katika kipindi hiki, amesema Tanzania inapaswa kutumia changamoto hiyo kama fursa ya kujenga uchumi wenye ustahimilivu, kupunguza utegemezi wa nje na kuimarisha mifumo ya maendeleo jumuishi.
