Viwango vya Undumakuwili wa Ulaya; Kwa Nini Jinai za Israel Zinanyamaziwa KimyaViwango vya Undumakuwili wa Ulaya; Kwa Nini Jinai za Israel Zinanyamaziwa Kimya

Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kukamata meli 50 zilizokuwa zimebeba wanaharakati 428 wa haki za binadamu na misaada ya kibinadamu kutoka nchi 44 kwa ajili ya Wapalestina wanaozingirwa na utawala huo huko Gaza katika bahari ya Mediterania imeibua wimbi la hasira na chuki dhidi ya Wazayuni.

Irene Montero, mjumbe wa Bunge la Ulaya amekosoa vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya msafara wa kimataifa wa meli za “Al-Sumud” na kimya cha viongozi wa Ulaya katika kukabiliana nayo, na hivyo kufichua undumakuwili wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala zima la haki za binadamu. Amesikitishwa na ukweli mchungu kwamba jinai dhidi ya Wapalestina zinakabiliwa na kile amesema ni siasa za “kufumbia macho na kutabasamu tu.” Mjumbe huyu wa Kihispania wa Bunge la Ulaya amehoji: “Mngefanya nini kama Iran au Russia zingewateka nyara raia wa Ulaya?”

Msafara wa meli za Al-Sumud ulianzia safari yake huko Marmaris, Uturuki, kwa ajili ya kuvunja mzingiro wa Gaza, lakini ukasimamishwa katika maji ya kimataifa na jeshi la wanamaji la Israel ambapo abiria wake walikandamizwa na kulazimishwa kupiga magoti huku wakiwa wamefungwa mikono. Video ya udhalilishaji ambayo ilisambazwa na Itamar Ben-Gvir, waziri mbaguzi wa rangi wa usalama wa ndani wa Israel kuhusu tukio hilo, imewathibitishia walimwengu sura halisi ya utawala huo ghasibu. Matukio ambayo Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Uhispania, amesisitiza kuwa “hayakubaliki kabisa.” Serikali ya Uhispania imemwita balozi wa Israel mjini Madrid kufuatia kusambazwa kwa picha za kukamatwa, kudhalilishwa na kutusiwa watetezi wa haki za binadamu katika msafara wa kimataifa wa Al-Sumud.

Huku kukiwa na wimbi la ukosoaji mkali wa kimataifa kuhusu suala hilo, Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Palestina, amechukua msimamo ambao ni zaidi ya taarifa rasmi zinazotolewa katika uwanja huo. Ripota huyo ambaye awali alikuwa ametunukiwa “Medali ya Ubora” na serikali ya Uhispania kutokana na juhudi zake za kurekodi ukiukaji wa haki za binadamu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ametoa jibu la kuvutia kuhusu tukio hilo. Ameashiria matamshi ya Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Italia ambaye amelaani kitendo cha Ben Gvir, na kuandika katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Bi. Meloni, kumlaani Ben Gvir ni jambo zuri lakini maneno pekee hayatoshi,”

Francesca Albanese

Ameitaka Italia kuachana na upinzani wake dhidi ya kusitishwa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati wa Umoja wa Ulaya na Israel na kuchukua hatua za kivitendo dhidi ya jinai za utawala huo ghasibu. Katika taarifa yenye maneno makali Albanese amesisitiza kwamba udhalilishaji uliofanywa dhidi ya wanaharakati wa Al-Sumud ni “kitendo cha anasa” kikilinganishwa na mateso wanayoyapitia Wapalestina katika jela za kuogofya za Israel. Ripota huyo wa Umoja wa Mataifa awali alikuwa ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kidiplomasia kwa ajili ya kuachiliwa bila masharti wafungwa wa matukio kama hayo, likiwemo lile la kukamatwa meli ya misaada ya kibinadamu ya “Madeleine” na vikosi vya Israel.

Sisitizo la mara kwa mara la Albanese kuhusu udharura wa nchi za Uaya kuchukua hatua zaidi za kivitendo badala ya kulaani kwa maneno matupu hatua za kikatili za Israel linaibua swali la msingi kuwa je, Ulaya iko tayari kulipa gharama ya kisiasa ya kukabiliana na Israel?

Mienendo ya serikali za Ulaya mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni inatoa taswira ya undumakuwili ambao kwa miaka mingi umekuwa sera ya kistratijia katika siasa za nje za bara hilo.

Kwa mfano, nchi saba za Ulaya, ambazo ni Ufaransa, Uhispania, Italia, Ubelgiji, Uholanzi, Ugiriki na Ureno, zimeripotiwa kuwaita mabalozi au mabalozi wadogo wa Israel kwa ajili ya kuwalalamikia kuhusu tukio la karibuni. José Manuel Álvarez, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ametaja kitendo walichofanyiwa wanaharakati hao kuwa cha “kuchukiza, aibu na unyama.” Waziri mkuu wa Italia ameitaka Israel iombe msamaha mara moja, nayo Ufaransa “imetaka ufafanuzi zaidi” kutoka kwa balozi wa Israel. Antonio Costa, Mkuu wa Baraza la Ulaya, amesema, “ameshtushwa” na tabia hiyo.

Global Sumud Flotilla

Lakini je, ukosoaji huo wa kidiplomasia ni mzito kwa kiasi gani? Ukweli ni kwamba hakuna nchi yoyote kati ya hizo zilizotajwa ambayo imechukua hatua yoyote ya kivitendo mbali na kuwaita mabalozi wa Israel na kutoa taarifa za kulaani kitendo hicho. Kusitishwa makubaliano ya kimkakati ya ushirikiano wa Ulaya na Israel, suala ambalo Albanese amekuwa akilisisitiza mara kwa mara, bado halijatekelezwa. Vikwazo vya kiuchumi au kisiasa dhidi ya Israel, mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani, haviko kwenye ajenda ya Ulaya. Pengo hili lililopo kati ya maneno na vitendo vya viongozi wa Ulaya ndilo linabainishwa na Montreux na Albanese wakisema: “Ulaya inapokabiliwa na jinai za Israel, “hutabasamu tu na kuamua kutazama kando,” katika hali ambayo ikiwa kitendo kama hicho kingefanywa na nchi isiyofungamana na Ulaya, ingewekewa vikwazo vya kulemaza mara moja.” Katika viwango vya undumakuwili vya nchi za Magharibi, maisha ya Wapalestina na wanaharakati wanaowaunga mkono yana thamani ndogo yakilinganishwa na ya wanadamu wengine. Montreux, kwa kufichua unafiki huu wa kihistoria, naye Albanese kwa kuitaka Ulaya ichukue hatua za kivitendo katika uwanja huo, wameibua swali ambalo linatoa changamoto kubwa kwa dhamiri ya pamoja ya Ulaya: Je, Ulaya iko tayari kusimama imara katika kukabiliana kiadilifu na jinai, bila kujali utambulisho wa kijinai wa Wazayuni, badala ya kukaa kimya na kutabasamu tu?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *