Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeelezwa kuwa Tanzania Railways Corporation itaendelea kuwatumia wataalamu wenye uzoefu wa muda mrefu ndani ya shirika hilo huku hatua maalum zikiendelea kuchukuliwa kuboresha mfumo wa ajira kwa wataalamu hao.
Hayo yameelezwa Mei 23, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Shiwa, mbele ya Kamati ya PAC ilipotembelea na kukagua utendaji kazi wa karakana ya TRC mkoani Morogoro.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Khalfan Hilary, amesema kamati hiyo imeridhishwa na maboresho makubwa yaliyofanyika katika karakana hiyo ikiwemo uundaji na ukarabati wa vichwa vya treni vya MGR.
“Mara ya mwisho tulipofika hapa hali ilikuwa tofauti, lakini sasa kuna maboresho makubwa na ufanisi unaonekana wazii tumeridhishwa na kazi nzuri inayoendelea,” amesema Mhe. Aeshi.
Aidha, amesema kamati hiyo itaendelea kuishauri Serikali kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya TRC na taasisi zake zinarejeshwa kwenye mashirika husika ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu.
Kwa upande wake, Mhandisi Shiwa amesema TRC itaendelea kuweka kipaumbele katika kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuhifadhi wataalamu wenye uzoefu mkubwa ili kuongeza tija ndani ya shirika hilo.
Mmoja wa wahitimu wa Chuo cha Reli cha TIRTEC, Elizabeth Ng’oko, amewahamasisha wasichana kujiunga na masomo ya reli akisema fursa za ajira ndani ya TRC zinaendelea kuongezeka.
(Feed generated with FetchRSS)
