Mchungaji Msigwa arejea Chadema, aitaja Oktoba 29Mchungaji Msigwa arejea Chadema, aitaja Oktoba 29

Iringa. Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini kupitia Chadema, Mchungaji Peter Msigwa aliyejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) Juni 30, 2024 ametangaza kurejea Chadema.

Mchungaji Msigwa ametangaza uamuzi huo leo Jumamosi, Mei 23, 2026 akisema ni baada ya tafakari ya kina kuhusu hali ya haki na utu wa binadamu nchini.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo Jumamosi kupitia mitandao ya kijamii, Mchungaji Msigwa amesema amefikia uamuzi huo baada ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, dhuluma na ukosefu wa utu yaliyotokea Oktoba 29, 2025.

Mwananchi limemuuliza juu ya ujumbe huo kama kweli ni wa kwake ambapo amesema:”Ni kweli ni wa kwangu.”

Katika akaunti za Chadema zimeuweka ujumbe huo na kuandika:”Karibuni tena Chadama Mchungaji Msigwa.”

“Matukio hayo yaliniumiza na kunifanya nishindwe kuendelea kuishi katika huzuni na ukimya,” imeeleza taarifa hiyo ya Mchungaji Msigwa ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa.

Mchungaji Msigwa amesema kwa dhamira yake binafsi ameona ni vyema kurejea Chadema kwa kufuata taratibu zote rasmi za chama hicho.

Katika ujumbe wake, mwanasiasa huyo pia amewaomba radhi wanachama wa Chadema pamoja na Watanzania wote ambao waliwahi kuumizwa au kukatishwa tamaa na msimamo wake wa awali alipokuwa nje ya chama hicho.

“Na binadamu hukosea lakini jambo muhimu ni uwezo wa kutambua makosa na kurekebisha pale dhamira inapozinduka,” amesema Mchungaji Msigwa.

Mchungaji Msigwa amesema matukio mbalimbali yaliyoshuhudiwa nchini yalimfanya aanze kutafakari upya kuhusu nafasi yake kisiasa na wajibu wake kwa jamii na kuwa haki, utu na demokrasia ni misingi ambayo haipaswi kupuuzwa katika taifa lolote.

Kupitia taarifa yake hiyo, Mchungaji Msigwa ameonyesha kurejea kwake Chadema ni sehemu ya safari mpya ya kisiasa inayolenga kuendelea kupigania maslahi ya wananchi na ameahidi kushirikiana na viongozi na wanachama wa chama hicho katika kujenga Tanzania yenye haki na usawa kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *