
Dar es Salaam. Katika michezo ya zamani, mchezo wa “tobo-ngumi” au “tobo-bao” ulikuwa muhimu sana. Lakini wakati ule watoto hatukuujua umuhimu huo. Mchezo huu ulifunga dimba la michezo ya siku nzima. Pale ambapo watoto walikaribia kuagana ili kila mmoja arudi kwao kuoga, dada zetu walimaliza kwa “Kidali-po” saa kumi na mbili jioni na sisi ndipo tulipolianzisha kwa tobo-ngumi saa moja kasoro.
Mchezo huu ulihusisha mpira uliochezwa bila sheria wala mfumo maalum. Hakukuwa na timu, magoli wala sheria za kimichezo. Wote tuliugombania mpira shakalabaghala, goli letu likiwa tobo, yaani kuupitisha mpira huo katikati ya miguu ya mmoja wetu. Atakayepigwa tobo ataadhibiwa kwa kipigo, na kinga yake ni kukimbia na kushika alama tuliyoichagua. Mara nyingi tulipendekeza mti uliokuwa kando ya uwanja wetu.
Faida ya kwanza ya mchezo huu, ilikuwa kuweka ukomo wa michezo ya siku hiyo. Hii ni kwa sababu watoto hawapendi kuoga wala kulala, sasa wanapofikiria kuachana na michezo na kwenda kuoga huwa wanavurugwa sana. Hivyo tobo-ngumi ilisaidia kwani hakukuwa na nafasi ya kufikiria wala kuagana; mmoja aliyenasa alipigwa hadi akaangua kilio, watoto wote walilazimika kutawanyika kwa woga.
Lakini faida ya pili kwenye mchezo huu ilikuwa kulipa kisasi. Mara zote watu waliowindwa zaidi kupigwa matobo walikuwa ni wale tuliowahara zaidi kwenye mchezo wa ngumi. Ngumi nazo ulikuwa na muhimu wake hasa kwenye masuala ya kuheshimishana. Kila mara wapiganaji walikuwa ni watoto waliokosa kuheshimiana. Wakapigiwa mstari kati yao kugawanywa kila mmoja na himaya yake.
Yule aliyejiamini aliuvuka mstari kuteka himaya ya mwenzake. Mwenzake alipaswa kupigana ili kuilinda. Ama mmoja wa wapiganaji aliufumbata mchanga mkononi, mchokozi akauputa mkono huo na kuumwaga mchanga. “Lipa ng’ombe wangu!” aliyeputwa mkono akadai. Kilichofuata hapo ni ngumi kwa kwenda mbele.
Mtoto anayeshindwa kwenye mchezo huu anabaki na kisasi. Hapa ndipo umuhimu wa tobo-ngumi unapoingia. Kila aliyekula kichapo kwenye mchezo wa ngumi, alijitahidi kila awezavyo kumpiga tobo mbabe wake. Alipofanikiwa akamaliza hasira zake, kwani kipigo cha hapo kilikuwa halali na cha wengi. Ukimzuia mmoja, wengine wanakuongezea kipigo.
Lakini tulishuhudia wababe wengi wakipigwa na wanyonge wao kwenye mchezo wa ngumi. Pale kwenye utaratibu wa kuputa mchanga, ghafla mnyonge aliruka kichwa au kumshtukiza mbabe kwa ngumi ya jicho, na mchezo ukaishia hapo. Mtindo huu wa kushtukiza ukachukua umaarufu kama ukombozi kwa wanyonge mbele ya watemi wao.
Hili limejitokeza hivi karibuni kule Mkoani Njombe, ambapo kijana alichelewa kurudi nyumbani, akaulizwa na kaka yake sababu iliyomchelewesha. Jibu lake lilikuwa ni shambuio la ghafla kichwani mwa kaka yake na kumsababishia umauti. Mpaka sasa tunajiuliza huyu dogo alikutwa na nini? Au kama kawaida itasemwa kuwa ni “afya ya akili”! Naona sasa tunaliweka neno “afya ya akili” kwenye kila jambo tusilohitaji kulijadili kwa kina.
Kuna aina ya majibu yanayolazimisha ukomo wa maswali. Kwa mfano kesi ya mtu aliyeua “bila kukusudia” haiwezi kulinganishwa na mauaji ya shambulizi. Polisi wana namna yao ya kuchunguza kama kulikuwa na matumizi ya silaha, silaha hiyo ilikuwa ya namna gani na ilitumika mara ngapi. Nadhani kuna tofauti iwapo nondo ilitumika mara moja kusababisha mauaji na ile iliyotumika mara nane, au bunduki iliyofyatuliwa mara nne.
Hivi sasa kila kosa linahusishwa na “afya ya akili”. Majuzi tena tumesikia kule Mkoani Arusha, ambapo kijana kauawa kwa kisa cha kutosalimia kijiweni. Ebu tujiulize kama kijiwe hicho nacho kilikumbwa na hitilafu ya afya ya akili. Kama ndivyo, basi kuna haja ya kuutangaza upungufu wa afya ya akili kuwa “janga la kitaifa” katika mwaka huu. Watu wasije wakafanya ubakaji, uhujumu na uhaini kwa kisingizio hicho.
Ni lazima tuwe makini. Haya majaribu na matatizo yapo kila siku, na wala hakuna binadamu mwenye ukamilifu wa kuyaepuka. Jukumu letu linabaki kuwa kuepuka maovu na kukumbatia mema. Upungufu wa afya ya akili haujaanza leo wala jana, ulikuwapo tangu kale na mpaka sasa unabadilika majina tu. Watu wa zamani wanashangaa majina mapya, wakati watu wapya wanashangaa mambo ya kale.
Naamini kuna wakati tutakuwa sawa. Kuna mwenzetu alimtongoza mrembo alipokuwa ugenini. Alipoingia naye ghetto akagundua kuwa msichana huyo alikuwa na miguu ya mbuzi! Akatoka mbio lakini njiani akashikwa na askari. Alipohojiwa mbio zote zilikuwa za nini, kwa kitete akajibu “nimekutana na demu ana miguu ya mbuzi!” Askari akapandisha shruali na kuvua kiatu, “kama hii?” kumbe naye alikuwa walewale. Jamaa akaendelea kukimbia.
Lakini baada ya muda alichoka sana. Akawa hana jinsi ila kupumzika, hivyo alijitupa panapo nyasi na kuvua viatu. Hammadi! Akaiona miguu yake ikiwa na kwato za mbuzi! Ndipo alipopata jawabu kuwa kwenye ardhi ile miguu yote hubadilika na kuwa ya mbuzi. Ndivyo tatizo la lugha lilivyo. Kitu kama hukielewi kinakuwa cha ajabu sana, lakini ukikielewa kinakuwa rahisi sana. Uhaba wa afya ya akili kila mtu anapita nao, tofauti ni jinsi mtu huyo anavyoshughulika nao.
