MEE: Misri iliishinikiza Al-Azhar ‘kuunga mkono UAE’ katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya IranMEE: Misri iliishinikiza Al-Azhar ‘kuunga mkono UAE’ katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran

Ripoti zinasema kwamba Ofisi ya Rais wa Misri iliishinikiza taasisi ya Al-Azhar, ambayo ni mamlaka ya juu zaidi ya Waislamu wa madhehebu ya Suni, kuunga mkono hadharani Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na mataifa mengine ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Middle East Eye (MEE) imenukuu vyanzo vilivyo karibu na Al-Azhar vikisema: “Mwanzoni mwa vita vya sasa, taasisi za serikali ya Misri ziliitaka Al-Azhar kupendelea na kujiunga waziwazi na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na kuepuka kuzungumzia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran”.

“Ilisemwa waziwazi na moja kwa moja na taasisi ya rais kwamba kuna maslahi makubwa kuwa pamoja na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na Marekani na kwamba hatuwezi kutupilia mbali maslahi hayo katika mazingira ya sasa ya kiuchumi … na kwamba Al-Azhar ingebeba lawama za Wamisri ambao watapoteza ajira zao katika Ghuba ya Uajemi iwapo itachukua msimamo tofauti,” kimesema chanzo kingine.

Wakati wa uvamizi Juni 2025 uliofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, Al-Azhar ilivitaja vita vya siku 12 kuwa ni “uchokozi wa utawala vamizi wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Kwa mujibu wa MEE, “msimamo huo wa awali wa al Azhar uliikasirisha UAE, ingawa haikulengwa kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran wakati huo.

Wakati huo, gazeti la Imarati la Al-Khaleej, ambalo ni chombo cha utawala wa Al Nahyan, lilikosoa msimamo wa Imam Mkuu wa al Azhar, Ahmed al-Tayeb.

Hata hivyo, tangu kuanza uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28, taasisi hiyo kuu ya Kisuni huko Cairo imetoa taarifa nne, ambazo hakuna hata moja kati yazo iliyolaani mashambulizi ya Marekani au Israel, ikiwa ni isharia ya mabadiliko kutoka kwenye msimamo wake wakati wa vita vya mwaka jana.

Taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na al Azhar mapema Mei iliyataja mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya milki na kambi za kijeshi za Marekani katika UAE kuwa ni “uchokozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya jirani yake Mwislamu, yaani Imarati”.

Vyanzo vya kuaminika vinasema uhusiano wa karibu wa kibinafsi kati ya Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi na mwenzake wa Falme za Kiarabu, pamoja na maslahi ya kiuchumi ya Misri huko Abu Dhabi, uliilazimisha Al-Azhar kutoa taarifa inayolaani mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Marekani na Israel.

Middle East Eye (MEE) imeongeza kuwa, serikali ya Misri ilitumia mbinu hiyo hiyo na Al-Azhar wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya raia wa Palestina huko Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *