
Ismail Baqaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amechapisha nukuu ya ripoti ya jarida la masuala ya tiba la The Lancet kuhusu uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Taasisi ya Pasteur ya Iran, na kusisitiza kwamba kuharibiwa taasisi hiyo ni tishio kwa usalama wa kikanda.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma sehemu ya ripoti hiyo ya jarida maarufu la matibabu la The Lancet kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.
Jarida la The Lancet limeandika katika ripoti yake kwamba: “Taasisi ya Pasteur ya Iran ni mojawapo ya nguzo kuu za mfumo wa afya wa Iran kwa zaidi ya karne moja. Taasisi hiyo imekuwa na jukumu muhimu na imefanya kazi kubwa ya kutengeneza na kuzalisha chanjo, ikitumika kama marejeo ya shughuli za kimaabara, na imekuwa ikifanya kazi ya kutambua, kuchunguza na kufuatilia magonjwa ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa corona, kipindupindu, kichaa cha mbwa, surua, Ukimwi n.k.
Kuharibiwa taasisi hiyo ni tishio kubwa kwa afya ya jamii, iimesema ripoti ya The Lancet. Na kuongeza kuwa: Suala hili halilihusu tu taifa la Iran bali uharibifu uliosababishwa kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel unaweza kuathiri afya ya umma katika kanda nzima ya Asia Magharibi.
Ripoti ya jarida hilo maarufu la kitiba imeeleza kuwa: Kushambulia kituo cha kisayansi na afya chenye historia ya zaidi ya karne moja sio kushambulia jengo tu, ni mashambulizi dhidi ya haki ya afya, haki ya kufaidika na utaalamu, na haki ya kuishi ya watu wa Iran.
