
Orlando Pirates imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) baada ya leo, Jumamosi, Mei 23, 2026 kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Orbit College katika Uwanja wa Royal Bafokeng, Rustenburg, Afrika Kusini.
Ushindi huo wa leo, umeifanya Orlando Pirates kumaliza msimu ikiwa juu kileleni mwa msimamo wa PSL na pointi 69 huku waliokuwa mabingwa watetezi, Mamelodi Sundowns wakimaliza katika nafasi ya pili na pointi zao 68.
Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Pirates kuchukua ubingwa wa Afrika Kusini tangu ilipofanya mara ya mwisho katika msimu wa 2011/2012.
Kuhitimishwa kwa ukame wa miaka 14 wa Orlando Pirates kutotwaa taji la PSL kumeenda sambamba na kumaliza utawala wa muda mrefu wa Mamelodi Sundowns katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Kabla ya kupoteza taji msimu huu, Mamelodi Sundowns ilikuwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini kwa misimu nane mfululizo.
Mabao ya ushindi ya Orlando Pirates katika mchezo wa leo yote yalikuwa ya kujifunga ya wachezaji wa Orbit College.
Bao la kwanza lilipatikana katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza likiwa la kujifunga la Sabelo Nkomo.
Ndumiso Ngiba naye amejifunga katika dakika ya 50 na kuihakikishia ushindi na taji, Pirates.
Baada ya kichapo cha leo, Orbit College imeshuka rasmi daraja.
