
Dar es Salaam. Wakati uchunguzi wa Mwananchi ukibaini namna mtandao wa siri wa utoaji mimba usio salama unavyoendelea kujitanua nchini, wataalamu wa sheria, afya na uchumi wamesema suluhisho la kudumu haliwezi kupatikana kwa kutumia sheria kali pekee, bali kupitia maboresho ya sheria, elimu kwa umma, kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kudhibiti soko haramu linaloendesha biashara hiyo kwa siri.
Katika uchunguzi huo uliochapishwa katika sehemu mbili, Mwananchi ilibaini kuwa wanawake wengi wanaotafuta huduma hizo hulazimika kutumia kati ya Sh40,000 na Sh150,000 kununua dawa zinazohusishwa na utoaji mimba.
Aidha, gharama hizo huweza kuongezeka hadi kufikia Sh1 milioni pindi matatizo makubwa ya kiafya yanapotokea.
Uchunguzi huo pia ulionesha namna mtandao huo wa siri unavyohusisha wapatanishi, baadhi ya wafamasia, wahudumu wa afya wanaofanya kazi kwa siri na vituo visivyo rasmi vya matibabu, huku huduma nyingi zikifanyika kupitia simu na makundi ya WhatsApp.
Baadhi ya wanawake waliozungumza na Mwananchi walieleza namna walivyopoteza fedha nyingi wakitafuta huduma hizo kwa siri, huku wengine wakipata madhara makubwa ya kiafya yaliyowalazimu kukimbizwa hospitalini kwa matibabu ya dharura.
Wataalamu wa afya pia walionya kuwa baadhi ya wanawake hupoteza maisha kabla hata ya kufikishwa hospitalini kutokana na kutokwa damu nyingi, maambukizi makali ya damu na matumizi ya dawa au vifaa visivyo salama.
Ni katika mazingira hayo ambapo wadau mbalimbali wanasema kuna haja ya kutafuta suluhisho la muda mrefu litakalopunguza vifo, madhara ya kiafya na kuendelea kukua kwa soko haramu la utoaji mimba usio salama.
Wataalamu hao wanasema licha ya sheria zilizopo kuendelea kukataza utoaji mimba isipokuwa katika mazingira maalumu ya kuokoa maisha ya mama, hali halisi inaonesha kuwa huduma hizo bado zinaendelea kufanyika kwa siri katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Wakili wa kujitegemea, Peter Majanjala anasema Tanzania inahitaji kupitia baadhi ya sheria zake ili ziendane na mazingira ya sasa ya afya ya uzazi pamoja na wajibu wa kimataifa ambao tayari ilikubaliana nao.
Majanjala anasema Tanzania ilisaini na kuridhia Itifaki ya Maputo mwaka 2007, lakini masharti yake yanayohusu haki za uzazi na utoaji mimba katika mazingira maalumu bado hayajaingizwa kikamilifu katika sheria za ndani.
“Kuna haja ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya kanuni ya adhabu, hususan vifungu vya 150, 151, 152, 219 na 230, ili kuongeza mazingira ambayo mwanamke anaweza kuruhusiwa kutoa mimba kwa mujibu wa sheria,” anasema Majanjala.
Anasema mazingira hayo yanapaswa kujumuisha pale mimba inapotokana na ubakaji, ndoa za maharimu, shambulio la kingono au inapohatarisha afya ya akili na mwili wa mama mjamzito.
Anasema hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza utoaji mimba unaofanyika kwa siri na kuwafanya wanawake wengi kupata msaada wa kitabibu mapema.
“Kama Taifa tayari tuliridhia Itifaki ya Maputo, kuna umuhimu wa kuangalia namna masharti yake yanavyoweza kuendana na sheria za ndani bila kuacha pengo linalowasukuma wanawake kwenda kwenye mazingira hatarishi,”anasema.
Kifungu cha 14(2)(c) cha Itifaki ya Maputo kinazitaka nchi wanachama kuruhusu utoaji mimba katika mazingira maalumu ikiwamo ubakaji, kujamiiana kwa maharimu au pale ambapo mimba inahatarisha afya ya mama au maisha yake.
Hata hivyo, Tanzania inaendelea kutegemea zaidi vifungu vya Kanuni ya Adhabu vinavyokataza utoaji mimba isipokuwa inapofanyika kuokoa maisha ya mama.
Mbali na marekebisho ya sheria, wataalamu hao wanasema elimu kwa jamii ni moja ya hatua muhimu katika kupunguza madhara yanayotokana na utoaji mimba usio salama.
Majanjala anasema wananchi wengi bado hawaelewi kuwa huduma za baada ya kuharibika kwa mimba zinapatikana hospitalini bila kujali mazingira yaliyosababisha hali hiyo.
“Wananchi wanapaswa kufahamu kwamba, hata kama mimba imeharibika au imetolewa, bado wanaweza kwenda hospitalini kupata huduma za baada ya kuharibika kwa mimba ili kulinda afya na maisha yao,” anasema.
Kwa upande wake, mwanasheria wa haki za uzazi nchini, Martha Serengi anasema suluhisho la muda mrefu linahitaji pia kuondoa mazingira ya hofu na sintofahamu yanayowafanya wanawake wengi kushindwa kutafuta msaada wa afya mapema.
“Tunapokuwa na mfumo unaojengwa zaidi kwenye hofu, wanawake wengi wanaogopa kwenda hospitali au kuomba ushauri mapema. Mwisho wake wanajikuta wakitafuta msaada sehemu zisizo salama,” anasema Serengi.
Pia, anasema elimu ya sheria na afya ya uzazi inapaswa kupewa uzito mkubwa ili wananchi waelewe haki zao pamoja na huduma zinazopatikana katika vituo vya afya.
“Watu wengi hawaelewi hata huduma za baada ya kuharibika kwa mimba zinapatikana hospitalini na kwamba lengo lake ni kuokoa maisha.
Elimu hiyo inaweza kusaidia kupunguza vifo na madhara ya muda mrefu,” anasema.
Serengi anasema pia kuna haja ya kuweka mazingira yanayowawezesha wahudumu wa afya kufanya kazi zao bila hofu au mkanganyiko wa kisheria.
“Sheria inapokuwa ngumu au isiyoeleweka vizuri hata kwa baadhi ya wataalamu, matokeo yake ni wananchi kubaki kwenye sintofahamu na wengine kukimbilia soko la siri,” anasema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake, Isaya Mhando anasema kwa mtazamo wa afya ya umma, sheria kali pekee hazijafanikiwa kuzuia utoaji mimba, bali zimechangia huduma hizo kufanyika kwa siri katika mazingira yasiyo salama.
Anasema wanawake wengi hujikuta wakitumia dawa bila usimamizi wa kitaalamu au kufuata maelekezo kutoka kwa watu wasio na ujuzi wa afya.
“Sheria inapokuwa ngumu na watu wakihofia kufika hospitalini, wengi hujikuta wakikimbilia kwa watu wasio wataalamu au kutumia dawa kiholela bila vipimo muhimu,” anasema Dk Mhando.
Anasema kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni (2025) kwenye Jarida la BMC Public Health, kiwango cha ujauzito unaoishia kutolewa ni asilimia 14.3 Kitaifa.
Anasema matumizi holela ya dawa za kutoa mimba bila uchunguzi wa kitabibu yanaweza kuwa hatari zaidi kwa wanawake wenye mimba zilizotunga nje ya mfuko wa uzazi.
“Bila vipimo kama Utrasound, mwanamke anaweza kutumia dawa bila kujua kuwa mimba ipo nje ya mfuko wa uzazi na hali hiyo inaweza kuhatarisha maisha yake,” anasema.
Anasema baadhi ya wanawake wanaopata madhara makubwa hushindwa hata kufika hospitalini kutokana na hofu ya kukamatwa au kunyanyapaliwa.
Akinukuu tafiti mbalimbali za afya ya uzazi, Dk Mhando anasema wanawake wengi wenye matatizo yanayotokana na utoaji mimba hubaki majumbani badala ya kutafuta matibabu mapema.
“Hofu ya sheria na unyanyapaa imeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika kuwafanya wanawake wafike hospitalini kwa wakati,” anasema.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo anasema kudhibiti soko haramu ni sehemu nyingine muhimu ya suluhisho la muda mrefu.
Anasema biashara nyingi haramu huendelea kukua pale ambapo mahitaji bado yapo lakini hakuna mfumo rasmi unaoweza kuyasimamia kwa uwazi.
“Serikali inafanya udhibiti na kusimamia masoko halali pekee. Katika hili inatakiwa ifuate sheria zake kuhakikisha hospitali bubu na maeneo yote yanayojihusisha na vitendo hivi haramu yanafungiwa,” anasema Profesa Kinyondo.
Anasema mazingira ya usiri na uharamu yameifanya biashara hiyo kuwa na gharama kubwa huku wanawake wakiendelea kubeba mzigo wa kiafya na kifedha.
“Kadri huduma zinavyofanyika kwa siri, ndivyo hata uwezekano wa kukosekana kwa ubora wa huduma unavyoongezeka kwa sababu hakuna usimamizi wa wazi,” anasema.
Kwa mujibu wa wadau wa afya, suluhisho la kudumu linahitaji pia uwekezaji mkubwa katika elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ili kupunguza mimba zisizotarajiwa.
Wanasema ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu uzazi wa mpango, afya ya uzazi na huduma za ushauri umeendelea kuwaacha vijana wengi kwenye mazingira ya kufanya maamuzi kwa hofu na usiri.
Aidha, wataalamu hao wamependekeza kuimarishwa kwa huduma za afya ya uzazi katika hospitali na vituo vya afya ili wanawake waweze kupata ushauri wa mapema bila kuogopa hukumu kutoka kwa jamii.
Mjadala kuhusu utoaji mimba usio salama umeendelea kushika kasi nchini huku wadau mbalimbali wakisisitiza kuwa, changamoto hiyo haiwezi kutatuliwa kwa mkazo wa sheria pekee bila kuangalia hali halisi ya afya ya umma.
Kwa mujibu wa wataalamu, kupunguza vifo na madhara yanayotokana na utoaji mimba usio salama kutahitaji mchanganyiko wa elimu, maboresho ya sheria, huduma bora za afya pamoja na kupunguza hofu inayowafanya wanawake wengi kubaki kimya hadi wanapopata matatizo makubwa kiafya.
