Dar es Salaam. Msanii wa Hip Hop Bongo, Rosa Ree, (31), ifikapo Novemba 2026 atasherehekea kutimiza miaka 10 tangu alipoianza rasmi safari yake ya muziki, na sasa ni miongoni mwa wanaofanya vizuri katika rap.
Rosa Ree alitoka kimuziki chini ya The Industry kupitia ngoma yake, One Time (2016) ambayo ilitayarishwa na Nahreel, kisha baadaye Khaligraph Jones kutokea Kenya akisikika katika remix yake.
The Industry ni lebo ya muziki ambayo ilianzishwa na wanamuziki wa kundi la Navy Kenzo (Nahreel & Aika), ambapo Rosa Ree alikuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzoni kabisa kusainiwa.
Rosa Ree na wenzake wawili, Seline na Wildad walitambulishwa na The Industry hapo Mei 2016, ambapo kila mmoja aliachia kazi yake baada ya maandalizi ya kutosha ambayo yalianza mwaka mmoja kabla ya tukio hilo.
“Nilitoa wimbo wangu wa kwanza ‘One Time’ mnamo Novemba 2016, na mwaka huu Novemba 2026 nitakapotimiza miaka 10 ya safari yangu ya muziki, nina mambo mengi sana niliyopanga tusherehekee pamoja,” ameeleza Rosa Ree.
Baada ya kufanya vizuri na wimbo wake, One Time (2016), Rosa Ree alikuja kufunika zaidi kupitia ngoma yake ya pili iliyotayarishwa na Nahreel pia, Up In The Air (2017) iliyofanya vizuri hadi kuingia tano bora chati za Sound city, African Rox Countdown.
Hata hivyo, Oktoba 2017, Rosa Ree alitangaza kuachana na The Industry, hivyo akaanza kufanya kazi peke yake ambapo ngoma yake ya kuanza kuachia wakati huo ni Dow (2017) ukitayarishwa na Luffa.
Kisha ikafuata kolabo yake ya kwanza na msanii kutokea Bongo, ambaye ni Billnass aliyesikika katika ngoma yake, Marathon (2018) chini utayarishaji wake Brezzy.
Baadaye Rosa Ree alirejea katika lebo, awamu hii alisaini mkataba wa miaka mitatu na Dimo Production ya Afrika Kusini hapo Mei 2018, lakini mkataba huo haukutekelezeka hadi mwisho kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
Kazi yake ya kwanza chini ya Dimo Production ni Way Up (2018), akimshirkisha rapa kutokea Afrika Kusini, Emtee ambaye baadaye alikuja kufanya kazi na wasanii wengine wa Hip Hop Bongo kama Country Wizzy na Young Lunya.
Kwa ujumla akiwa na Dimo Production alitoa nyimbo tatu na mkataba wao ukawa umekomea hapo. Rose Ree aliendelea kutoa nyimbo zake za rap pamoja na dancehall, miondoko ambayo ndio hasa anaipatia mbele ya maiki.
Novemba 2019, kazi yake ilikumbana na changamoto kubwa baada ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kumfungia kujihusisha na sanaa kwa miezi sita!.
Adhabu hiyo ilikuja baada ya kurekodi video isiyo na maadili akishirikiana na rapa wa Kenya, Timmy TDat, pamoja kufanya kazi nje ya nchi bila kuwa na kibali cha Basata.
Hata hivyo, mwezi mmoja baada ya msanii huyo kukiri makosa yake na kuomba radhi, Basata ilimuondolea adhabu hiyo na kutakiwa kulipa faini ya Sh2 milioni pekee.
Miaka miwili mbele, Rosa Ree akaachia albamu yake ya kwanza, Goddess (2022) yenye nyimbo 17, huku akiimiliki kwa asilimia 100 kutokana gharama zote za uandaaji zilitoka kwake na sio katika rekodi lebo au kampuni yoyote ya usambazaji muziki.
Wimbo wake, Blueprint (2022) ulimuwezesha kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kwa mara ya kwanza. Tuzo hizo zilizofanyika Machi 2023, Rosa Ree aliibuka mshindi katika vipengele vya Msanii Bora wa Kike wa Hip Hop na Wimbo Bora wa Hip Hop (Blueprint).
Mbali na TMA, ameshinda tuzo nyingine kama Entertainment Arts Excellence Awards (EAEA) 2022, The Orange Awards 2022 na Magic Vibe Awards 2023, kote aking’aa kipengele cha Msanii Bora wa Hip Hop.
“Leo nataka tu kusema asanteni kwa kuniunga mkono katika safari yangu, kwenye nyakati za furaha na changamoto, kupanda na kushuka, pamoja na mabadiliko yote niliyopitia kwa 10 iliyopita,” amesema Rosa Ree.
Kwa miaka hii 10, Rosa Ree amefanya kazi na wasanii wengi wakubwa, mmoja wao ni staa wa Hip Hop Bongo, Fid Q ambaye wameshirikiana katika nyimbo nne – Ole Chizza (2018), Korasi (2019), Trust (2022) na Bigman (2023). Rapa wa Marekani, Rick Ross katika moja ya Podcast zake alimtaja Rosa Ree kuwa miongoni mwa wasanii wa Hip Hop anaowakubali kutokea barani Afrika na sio ajabu akija kumsaini Maybach Music Group.
