Akutwa amefariki dunia chumbani kwake kwa kukosa hewaAkutwa amefariki dunia chumbani kwake kwa kukosa hewa

Makete. Mkazi wa Kijiji cha Ikonda kilichopo Wilaya ya Makete mkoani Njombe, Nestory Mbilinyi (43), amefariki dunia baada ya mwili wake kukutwa ndani ya chumba alichokuwa amejiwekea kufuli kwa siku kadhaa huku chanzo cha kifo kikielezwa kuwa ni kukosa hewa kutokana na matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo.

Tukio hilo limeelezwa leo Mei 25, 2026 na Ofisa Tabibu wa Hospitali ya Wilaya ya Makete, Frank Nyato, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Nyato amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mapafu pamoja na moyo kutanuka, hali iliyochangiwa na matumizi ya pombe na sigara kwa muda mrefu.

“Sababu ya kifo ni kukosa hewa. Pembeni yake kulikuwa na dawa nyingi alizokuwa akitumia. Pia, picha ya X-ray inaonyesha alikuwa na matatizo ya mapafu na moyo wake ulikuwa umetanuka sana,” amesema Nyato.

Baadhi ya wananchi wakishiriki msiba wa Nestory Mbilinyi, aliyefariki akiwa nyumbani kwake wilayani Makete, mkoani Njombe.

Amesema matatizo hayo yanaweza kumpata mtu ghafla na kusababisha kuanguka bila kupata msaada wa haraka, hasa kwa watu wanaoishi peke yao kama ilivyokuwa kwa marehemu huyo.

Kutokana na tukio hilo, Nyato amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara pamoja na kuepuka matumizi ya pombe na sigara kupita kiasi.

Akizungumzia tukio hilo, kaka wa marehemu, Justin Mbilinyi amesema alipigiwa simu na dada yake Mei 23, 2026 akiombwa kuwasiliana na marehemu kwa simu, lakini jitihada hizo hazikufanikiwa.

Amesema alipokwenda nyumbani kwa marehemu alikuta mazingira yasiyo ya kawaida na baada ya kuuliza majirani walimweleza kuwa hawajamuona kwa siku kadhaa.

“Nilifungua mlango wa nje ukafunguka, lakini nilipoingia ndani nikakuta mlango wa chumbani umefungwa na kulikuwa na harufu nzito. Nikapata wasiwasi na kwenda kuwaambia majirani,” amesema Justin.

Naye, Joseph Mbilinyi, ambaye alikuwa akimuita marehemu baba mdogo, amesema familia imepata pigo kubwa kutokana na kifo hicho.

“Ni majonzi makubwa kwetu kwa sababu alikuwa mtu muhimu sana kwenye familia yetu na alipenda watu,” amesema Joseph.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gongonti, Angelina Mbilinyi amesema alipata taarifa za tukio hilo saa 2 asubuhi na kufuata taratibu za kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

“Tulipewa taarifa kuwa kuna wasiwasi katika nyumba aliyokuwa akiishi. Baada ya kufika tulishirikiana na wananchi na polisi kuingia ndani mwili ulikutwa ukiwa umelala kitandani,” amesema Angelina.

Ameongeza kuwa marehemu hakuwa ameoa wala kuwa na mtoto.

Diwani wa Tandala, Egnatio Mtawa ametoa pole kwa familia na kuwataka kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.

“Tunatoa pole kwa familia. Taratibu zote za mazishi na kuhifadhi mwili zitafanyika kama ilivyo kawaida,” amesema Mtawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *