Dodoma. Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Said Ali Mbarouk amesema mahusiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi si mazuri kwa sasa huku akiitaka Serikali kuchukua hatua za kurejesha imani kati ya pande hizo mbili.
Mbarouk amesema hayo leo Jumatatu Mei 25, 2026 wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka 2026/27 ya Sh2.4 trilioni iliyopitishwa na Bunge.
Amesema ripoti ya Haki Jinai ya Julai 2023 ilipendekeza kuwepo mkakati wa kuboresha mahusiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama, lakini hali bado haijabadilika.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, wananchi wengi wanaona baadhi ya askari polisi hawana weledi na wakati mwingine hujihusisha na vitendo vya ubaguzi hata katika masuala ya kawaida ya kijamii na biashara.
“Juhudi zifanyike kurejesha mahusiano haya. Hali siyo nzuri, hata kuna askari polisi mstaafu anauza samaki lakini wananchi wanaogopa kununua kwake kutokana na namna alivyokuwa akiwatendea zamani,” amesema Mbarouk.
Mbunge wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha ACT Wazalendo, Said Ali Mbarouk, akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bungeni jijini Dodoma.
Ameiomba Serikali kuhakikisha inaweka mazingira yatakayorejesha imani kwa wananchi dhidi ya jeshi hilo.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kiwani (CCM), Hija Hassan Hija amesema wizi wa mitandao umeongezeka lakini hatua zinazochukuliwa hazileti matokeo ya kuwabaini wahalifu.
Hija amesema yeye binafsi amekuwa mwathirika wa wizi huo tangu Januari mwaka huu licha ya taarifa kupelekwa Polisi kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Naomba niweke wazi kuwa mimi ni mhanga wa jambo hili. TCRA wanafanya kazi kubwa ya kubaini wahalifu lakini changamoto ipo kwenye ufuatiliaji,” amesema Hija.
Amesema aliwahi kutumiwa ujumbe wa ulaghai uliosababisha zaidi ya Sh260,000 kutolewa kwenye akaunti yake ya benki, jambo lililomshangaza kutokana na siri za akaunti hiyo kutofahamika hata kwa watu wake wa karibu.
Naye Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Yagi Kiaratu amesema chanzo kikubwa cha wizi wa mitandao ni uzembe wa kampuni za simu, huku lawama nyingi zikielekezwa kwa Polisi.
“Mlitusajili laini mara mbili lakini bado utapeli unaendelea. Hapa wa kulaumiwa ni kampuni za simu, siyo Polisi,” amesema Kiaratu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema usajili holela wa laini za simu unaofanywa mitaani ni moja ya sababu zinazochochea uhalifu wa mtandao, akitaka mfumo huo ufanyiwe marekebisho.
Mbunge wa Viti Maalum, Aziza Ali amesema wizi wa mtandao umeongezeka mkoani Tabora huku akihoji kwa nini wahusika hawakamatwi wakati laini zote zimesajiliwa.
Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu amehoji mkakati wa Serikali kuhusu matukio ya utekaji na watu kupotea, akitolea mfano tukio lililomhusu David Djumbe, msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Akijibu hoja za wabunge, Waziri wa Mambo ya Ndani, Parobas Katambi amesema matukio ya utekaji yana sababu tofauti zikiwemo migogoro ya biashara, siasa na sababu nyingine binafsi.
Amesema baadhi ya taarifa zipo mikononi mwa Polisi lakini haziwezi kuwekwa wazi kwa sasa kutokana na hatua za uchunguzi zinazoendelea.
Kuhusu wizi wa mitandao, Katambi amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Amesema hatua hizo pia zinalenga kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao ikiwemo kusambaza uzushi na kudhalilisha watu kupitia majukwaa ya kidijitali.
“Kwa sasa kila mtu ni msemaji na baadhi wanatumia akili unde (AI) kueneza taarifa za uongo. Haya nayo ni matishio kwa amani ya nchi,” amesema Katambi.
