Mgomo wa daladala Arusha watikisaMgomo wa daladala Arusha watikisa

Arusha. Wakazi wa Jiji la Arusha wamepata adha ya usafiri kufuatia baadhi ya waendesha huduma za daladala kugoma kuingiza magari yao barabarani kwa kile walichodai manyanyaso wanayopewa na Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) ya kuwatoza faini kati ya Sh250,000 hadi 350,000 kwa kuzidisha kiwango cha nauli kilichowekwa.

Wananchi wamelazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu huku wengine wakipanda maguta kuelekea katikati ya jiji wakilalamikia mgomo huo ambao wamesema unawaumiza wananchi kufika kwenye shughuli za uzalishaji pamoja na wanafunzi ambao wanaendelea na mitihani ya kufunga nusu muhula.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 25, 2026 eneo la Soko la Mrombo wamedai maofisa wa Latra wamekuwa wakiwatoza faini kuanzia Sh250,000 hadi Sh350,000 magari yanayozidisha nauli iliyopangwa na mamlaka hiyo wakati wakifahamu bei ya mafuta imepanda hatua inayosababisha wapandishe nauli ili kumudu gharama za uendeshaji.

Wakazi wa Jiji la Arusha wakitumia guta kusafiri kutoka Mrombo kuelekea katikati ya jiji kufuatia mgomo wa daladala leo Jumatatu Mei 25, 2026. Picha na Filbert Rweyemamu.

Mgomo huo  ulishuhudiwa kwenye barabara za kutoka katikati ya jiji kupitia Mrombo hadi Intel kuelekea  Mapambazuko pia kutoka Soko la Kilombero kupitia Uswahilini, Dampo hadi Mapambazuko na kutoka Soko la Kilombero kuelekea barabara Tengeru yenye vituo vya Mianzini, Sanawari, Mount Meru hadi Ngulelo .

Watoa huduma za usafirishaji waliozungumza na Mwananchi bila kutaka majina yao kuandikwa gazetini wamesema mabadiliko ya nauli walizofanya yanaendana na mabadiliko ya bei ya mafuta ya dieseli na petroli.

“Hatutoi huduma kuwafurahisha Latra na abiria, bali kutokana na gharama ya mafuta kuwa juu; tumelazimika kupandisha nauli ili tuweze kumudu gharama za uendeshaji kwa sababu tuna familia zinazotutegemea kama watu wengine,” amesema.

Wakazi wa Jiji la Arusha wakitumia guta kusafiri kutoka Mrombo kuelekea katikati ya jiji kufuatia mgomo wa daladala leo Jumatatu Mei 25, 2026. Picha na Filbert Rweyemamu.

Latra ilitangaza nauli ya Sh700 kutoka mjini hadi Mrombo ikiwa ni ongezeko la Sh100 wakati watoa huduma wanatoza Sh1,000 jambo linalodaiwa kuzua sintofahamu kati ya watoa huduma  na Latra kwa upande mmoja na abiria kwa upande mwingine.

Kiwango cha nauli kutoka nauli ya Sh600 hadi Sh1,000 ambayo ilikuwa ni kwa safari fupi kimelalamikiwa na abiria wengi huku wakilazimika kulipa Sh1,000 hadi 1,500 hasa nyakati za jioni huku watoa huduma za daladala wakikatisha safari kila mara na kusababisha misongamano nyakati za usiku kwenye vituo vya daladala.

Wananchi walilazimika kutumia usafiri wa maguta ambao walikua wakilipa Sh1,000 kwa safari fupi na Sh2,000 kwa safari ndefu huku bajaji na pikipiki nauli ikiwa kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000 kutoka Mrombo kuelekea katikati ya jiji.

Meneja wa Latra Mkoa wa Arusha, Omar Salehe amesema lengo la maofisa wa mamlaka hiyo kukagua viwango vya nauli wanavyotozwa abiria linalenga kuweka usawa katika ya abiria na watoa huduma za usafirishaji na kuwataka kurejesha huduma za kusafirisha abiria wakati vikao na wawakilishi wao vikiendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *