Dar es Salaam. Mwimbaji Diamond Platnumz amezaa na Zari The Bosslady watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016), Hamisa Mobetto mtoto mmoja, Dylan (2017) na Tanasha Donna mtoto mmoja, Naseeb Jr (2019).
Ukitazama wanawake hao watatu pamoja na shughuli zao hasa katika kiwanda cha burudani, utakuja kubaini kuwa Baby Mama wa Diamond wana sifa zinazofanana kama ifuatavyo.
Wote ni wanamuziki
Warembo wote aliozaa nao Diamond ni wasanii wakiwa wamewahi kufanya muziki kwa kurekodi nyimbo lukuki kwa nyakati tofauti, pengine hiki ni moja ya kigezo muhimu pale anapochagua Baby Mama.
Zari ana nyimbo zake kama Oliwange, Jukila, Kangume na Kikooma alizoimba kwa lugha ya nyumbani kwao Uganda, nyingine ni Hotter Than Them, In Love With The Dance Floor na Falling In Love.
Ingawa Hamisa nyimbo zake nyingi zilitoka baada ya kuzaa na Diamond ila tayari alisharekodi awali, ameshatoa EP, Yours Truly (2022) ikiwa na nyimbo sita.
Kwa upande Tanasha hakuna asiyejua uwezo wake wa kuimba, ana ngoma kubwa kama Radio, Gere, Liar na La Vie, huku akitoa EP moja, Donna Tella (2020) akiwashirikisha Diamond, Mbossso na Khaligraph Jones.
Wakali wa mitindo, urembo
Urembo na mitindo ni sifa nyingine anayoizingatia Diamond, ikumbukwe Zari, Hamisa na Tanasha wote wana sifa hizo.
Hakuna asiyejua ukali Zari upande wa urembo na mitindo na mara kadhaa amesimama kama Jaji kwenye mashindano ya urembo Uganda, pia amesomea masuala ya urembo akiwa na Diploma ya Cosmetology iliyoipata Uingereza.
Kabla ya muziki Hamisa alikuwa anafanya mitindo na ndio fani iliyomtangaza zaidi, ameshinda tuzo Tanzania, Afrika Kusini na Nigeria kama Mwanamitindo Bora, huku akishinda taji la Miss XXL, After School Bash 2010.
Naye Tanasha kabla ya muziki alikuwa akifanya mitindo katika ya Dominique Model’s Agency huko Brussels nchini Ubelgiji, huku akitumia jina la Zahara Zaire kwenye kazi zake ili kujitambulisha kuwa anatokea Afrika.
Wana ushawishi mitandaoni
Wakati Diamond anaanzisha uhusiano na Wema Sepetu hakuwa na maarufu kama mrembo huyo, baada ya kuachana naye Diamond alijenga utamaduni wa kuwa na uhusiano na wanawake maarufu na wenye nguvu ya ushawishi na ndio alikuja kuzaa nao.
Hadi sasa ni wanawake saba pekee Afrika Mashariki ambao wamefikisha followers zaidi ya milioni 10 Instagram, watatu kati yao Diamond amewahi kuwa na mahusiano nao, huku wawili akizaa nao ambao ni Zari na Hamisa.
Kipindi anaanzisha uhusiano na Tanasha mwaka 2018 tayari mrembo huyo alikuwa maarufu Afrika Mashariki kama Mtangazaji wa Radio, Mwanamitindo na Msanii, huku wengi wakiwa wamemfahamu tangu mwaka 2015 alipotokea kwenye video ya wimbo wa Alikiba, Nagharamia.