CEOrt kushirikiana na GGML Kili Challenge katika mapambano ya VVUCEOrt kushirikiana na GGML Kili Challenge katika mapambano ya VVU

Dar es Salaam. Mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yameungwa mkono na Jukwaa la Wakurugenzi Wakuu wa Kampuni Tanzania (CEOrt), likisema sekta binafsi inashiriki kikamilifu kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa wanaoishi na virusi hivyo.

CEOrt imeungana na Taasisi ya GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS Trust katika kuandaa kampeni mpya ya matembezi ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi nchini.

Uzinduzi huo utafanyika Mei 30, 2026, Dar es Salaam kupitia matembezi ya kujiandaa ya GGML Kili Challenge 2026, yatakayowakutanisha wananchi, kampuni binafsi, taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo katika harakati za kuhamasisha mchango wa jamii kwenye vita dhidi ya VVU.

GGML Kili Challenge 2026 na CEOrt zinashirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) katika mpango huo ambao umetajwa kuwa miongoni mwa miradi ya muda mrefu zaidi ya sekta binafsi nchini inayochangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Mei 26, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Majengo Benson amesema afya ya jamii ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa, hivyo sekta binafsi ina nafasi muhimu ya kusaidia juhudi za kitaifa dhidi ya VVU/UKIMWI.

“Ushirikiano huu unaipa sekta binafsi nafasi ya kushiriki kwa karibu zaidi katika kuunga mkono juhudi za taifa kupitia uongozi, uhamasishaji na mchango endelevu,” amesema Santina.

Kwa upande wake, Meneja wa Trust wa GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS Trust, Stephen Mhando amesema kampeni ya mwaka huu inalenga kuongeza ushiriki wa jamii katika kusaidia mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya “Ni Jukumu Letu Sote” inalenga kuwakumbusha Watanzania kuwa mapambano dhidi ya Ukimwi hayawezi kuachiwa serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa kila mmoja.

Mbali na matembezi ya kilomita tano na 10 yatakayofanyika katika maeneo ya Masaki na Oysterbay, kampeni hiyo pia itatoa elimu kuhusu umuhimu wa kupima VVU kwa hiari, kupunguza unyanyapaa na kusaidia wanaoishi na virusi hivyo kupata huduma stahiki.

Msimu wa Kili Challenge 2026 utahitimishwa kwa washiriki kupanda Mlima Kilimanjaro pamoja na shughuli za baiskeli katika maeneo ya mlima huo ikiwa ni sehemu ya kuendeleza kampeni ya uhamasishaji na uchangishaji fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *