
Unguja. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeomba kuhidhinishiwa Sh1.8 trilioni kutekeleza vipaumbele vinane kwa mwaka 2026/27, vikiwemo kuanzisha kampuni ya ndege ya Zanzibar pamoja na kuanza maandalizi ya uanzishwaji wa usafiri wa umma kwa njia ya reli.
Akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika mkutano wa bajeti wa Baraza la Wawakilishi Mei 26, 2026, Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk Khalid Salum Mohamed amesema kati ya fedha hizo, Sh1.7 trilioni ni kwa ajili ya maendeleo na Sh1.2 trilioni zitatolewa na SMZ.
Miundombinu ya barabara
Katika kuimarisha usafiri wa ardhini, Wizara imepanga kujenga barabara zenye jumla ya kilomita 445.25 Unguja na Pemba. Katika kilomita hizo, kilomita 159.5 ni barabara kuu, kilomita 82.73 ni barabara za mjini, kilomita 156.82 ni barabara za vijijini na kilomita 46.2 ni barabara zinazounganisha maeneo ya utalii ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika kwa urahisi pamoja na kuvutia wawekezaji.
Pamoja na ujenzi huo, pia wataendelea kuzifanyia matengenezo barabara mbalimbali kwa kuziba mashimo, kuzifanyia usafi pamoja na kununua mashine na vifaa vya kusafishia.
Usafiri wa anga
Katika kipaumbele hiki, wizara inapanga kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga kwa kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, kuendelea na ujenzi wa jengo la pili la abiria (Terminal 2 awamu ya pili) pamoja na ujenzi wa maegesho ya ndege (Apron) katika uwanja wa AAKIA.
Kwa upande wa bandari, Waziri Khalid amesema wataendeleza miundombinu ya bandari ikiwemo ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, bandari ya abiria na mizigo katika eneo la Mpiga Duri pamoja na bandari nyingine ili kuimarisha huduma za usafiri wa baharini.
Kwa upande wa usalama barabarani, wizara inatarajia kuweka kamera za usalama barabarani za kisasa, uwekaji wa taa za barabarani, udhibiti wa maeneo ya hifadhi ya barabara na uwekaji wa alama za usalama barabarani.
“Pia, tutajenga njia za watembea kwa miguu na kujenga madaraja ya kuvukia watembea kwa miguu katika maeneo ya msongamano wa watu ili kupunguza ajali za barabarani,” amesema Waziri Khalid.
Amesema pia watatayarisha sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali itakayowezesha kusimamia na kutoa huduma bora kwa jamii katika sekta ya ujenzi na uchukuzi kisiwani hapa.
Akisoma maoni ya Kamati ya Miundombinu, Ardhi na Tehama, mwenyekiti wa kamati hiyo, Mihayo Juma N’hunga, amesema mbali na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa barabara, Serikali iangalie uwezekano wa kuwafikia wananchi walipo katika maeneo ya barabara kwa kuwajengea barabara na njia za kutembea kwa miguu.
Pia, imeishauri wizara kupitia Wakala wa Barabara kuweka alama za barabarani na kingo za barabara pamoja na kuweka taa za barabarani ambazo zitasaidia kupunguza ajali za barabarani.
“Kamati inashauri Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wanaoharibu miundombinu kwa mujibu wa sheria kwani hawana lengo jema kwa nchi yetu katika suala zima la maendeleo,” amesema.
Michango ya wawakilishi
Wakichangia bajeti hiyo, baadhi ya wawakilishi wamesema licha ya kazi nzuri iliyofanywa na wizara katika ujenzi wa miundombinu hususani ya barabara, lakini utunzaji wake umekuwa na changamoto.
Mwakilishi wa Mkwajuni, Sulubu Kidongo Amour (CCM), amesema barabara zimejengwa, lakini zinatakiwa kulindwa.
“Haiwezekani barabara zimejengwa nzuri na vigae vizuri pembeni, lakini unakuta zimeegeshwa magari pembeni mwa barabara hizo. Pia, anayeamua kujenga asishushe kifusi kwenye barabara,” amesema.
Pia, ameitaka wizara kusimamia na kuzuia watu wanaojenga kumwaga vifusi vya ujenzi kwenye barabara hizo kwani vinaharibu na kuondoa taswira ya barabara hizo.
Mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar, amesema bado kuna wananchi wanadai fidia walipoisha ujenzi wa uwanja wa ndege.
Amesema wananchi wanaogopa kuendeleza nyumba zao kwa sababu tayari Serikali imeenda kufanya tathmini. “Kwa hiyo tunataka kupata mustakabali wa wananchi hao kuwalipa baada ya kuongeza maeneo ya kupisha mradi huo.”
Mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali (ACT Wazalendo), amesema barabara zinajengwa lakini nyingi hazina mitaro hivyo kusababisha kero kwa wananchi.
Pia, amesema Mamlaka ya Usalama na Usafiri Barabarani imekuwa kero kwa faini inazotoza wananchi, hivyo kuitaka wizara kuangalia upya utaratibu wake.
Mwakilishi wa Gando, Said Ali Mbarouk, amesema tatizo la Serikali ni namna ya kuchagua wakandarasi wa kutengeneza barabara.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, wapo wakandarasi wasio na uwezo wa kujenga na wakipewa kazi wanaharibu, lakini bado Serikali inaendelea kuwakumbatia na kuwatumia hao hao.
