Haya ndiyo yanayochochea migogoro ya ardhiHaya ndiyo yanayochochea migogoro ya ardhi

Dar es Salaam. Migogoro ya ardhi imeendelea kuwa miongoni mwa malalamiko makubwa yanayowasilishwa na wananchi katika ziara za viongozi wa kitaifa nchini, hali inayoashiria kuwa tatizo hilo bado linaendelea kuisumbua jamii.

Kwenye mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanywa na viongozi wa Serikali mikoani, wananchi wamekuwa wakitumia nafasi hizo kuwasilisha malalamiko yanayohusu umiliki wa maeneo, migongano ya mipaka, fidia, matumizi ya ardhi na migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

 Katika baadhi ya maeneo, migogoro hiyo imekuwa ikisababisha mapigano na mauaji ya watu, hali inayochochea mjadala wa kitaifa kuhusu chanzo na suluhisho la kudumu la matatizo hayo yanayoathiri jamii nchini.

 Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alikiri sehemu kubwa ya malalamiko anayokutana nayo katika ziara zake yanahusu migogoro ya ardhi, hali iliyomsukuma kutoa maelekezo kwa watendaji wa sekta hiyo kuongeza uwajibikaji katika utatuzi wa changamoto hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Dk Mwigulu amekuwa akiwasisitiza mawaziri, wakuu wa mikoa,wilaya pamoja na watumishi wa umma kutenga muda wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao hususani kwenye migogoro ya ardhi.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

Waziri Mkuu aliwahi kuwaagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Waziri wa Tamisemi kukaa kwa dharura na kuja na mapendekezo yatakayomaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.

Alisema viongozi wanapaswa kuwafuata wananchi, kuwasikiliza na kuchukua hatua za haraka za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakiwa katika maeneo yao.

Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Manyara, Machi 2026, Dk Mwigulu alisisitiza umuhimu wa kupanga matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro inayoendelea kujitokeza katika ziara zake, akiwataka viongozi wa mikoa, wilaya na maofisa ardhi kushughulikia migogoro kwa haki, haraka na kwa kuzingatia sheria.

Pia, alionya dhidi ya vitendo vya rushwa na ucheleweshaji wa uamuzi vinavyotajwa kuongeza malalamiko ya wananchi.

 Kuendelea kujitokeza kwa migogoro hiyo katika ziara za viongozi kunaonesha jinsi suala la ardhi lilivyoendelea kuwa nyeti kwa wananchi wengi, hasa katika kipindi hiki cha ongezeko la watu, ukuaji wa miji na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji na uzalishaji.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

Wataalamu wa ardhi, maendeleo ya jamii na wanasheria, wanasema changamoto hiyo inachangiwa na mambo mbalimbali huku wakigusia ukosefu wa mipango ya matumizi ya ardhi katika baadhi ya maeneo, ucheleweshaji wa upimaji wa viwanja pamoja na migongano ya matumizi kati ya kilimo, ufugaji na makazi.

Serikali imekuwa ikisisitiza inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha usimamizi wa ardhi, hata hivyo, kadri viongozi wanavyoendelea na ziara zao za kusikiliza na kutatua kero za wananchi, wanakutana na malalamiko mengi kuhusu migogoro ya ardhi.

Mei 28, 2026, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayoongozwa na Waziri, Dk Leonard Akwilipo inatarajia kuwasilisha bajeti yake kwa mwaka 2026/27 na huenda ikaja na mikakati ya nini kitafanyika kumaliza migogoro hiyo.

Sababu migogoro kukithiri

Akizungumza jana, Mtaalamu wa Mipango Miji na Masuala ya Ardhi, Prince Mwaihojo amesema tatizo si ugumu wa masuala ya ardhi, bali ni uzembe na utapeli unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na  kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

 “Mimi kama mwanataaluma wa mipango miji ninaona tatizo la ardhi nchini hapa ni utapeli tu na uzembe wa mamlaka za usimamizi. Masuala ya ardhi yaliyopo katika nchi yetu yanaweza kutatuliwa kwa utawala tu, kila mtu anajua ardhi yake ipo wapi,” amesema Mwaihojo.

 Amesema katika maeneo mengi ya vijijini wananchi wanafahamu mipaka ya maeneo yao, viongozi wa vijiji na wazee wa kimila wanayajua maeneo hayo, lakini watu kutoka mijini huungana na baadhi ya wachache vijijini kufanya utapeli wa ardhi kwa kutumia mianya ya kisheria na nguvu ya mamlaka.

 “Kitu kinachotokea ni watu wanaotokea mijini wanaungana na watu wachache huko vijijini wanakwenda kutapeli ardhi. Watu wakilalamika wanaambiwa waende mahakamani wakijua hawana uwezo wala uelewa wa masuala ya Mahakama,” amesema.

 Mwaihojo amesema baadhi ya wananchi hasa wanawake wa vijijini na vijana wamekuwa wakiporwa mashamba yao kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufuatilia kesi mahakamani au kupata nyaraka rasmi zinazotakiwa kuthibitisha umiliki wa maeneo yao.

 “Huko vijijini wananchi wanajua ardhi zao, watendaji wa vijiji wanajua maeneo ya watu, lakini wanaokwenda huko wanatumia polisi na kuwaambia wanaolalamika waende mahakamani. Unakuta mama wa kijijini hana uwezo wa kwenda mahakamani, vijana wananyang’anywa mashamba yao huko vijijini,” amesema Mwaihojo.

 Amesema viongozi wengi wamekuwa wakilifumbia macho tatizo hilo na kuliona kama jambo la kawaida, hali inayochochea kuendelea kwa migogoro hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Muonekano wa baadhi ya vyumba zilizoharibiwa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuibuka vurugu kati yao wakazi wa eneo hilo na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zimezotokana na mgogoro wa ardhi na  kusababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

 Wakili Dominic Ndunguru amesema kuongezeka kwa migogoro ya ardhi kunachangiwa pia na kuongezeka kwa uelewa wa thamani ya ardhi katika jamii kutokana na fursa za mikopo na uwekezaji zinazohitaji dhamana ya ardhi.

 “Kilio hiki kinatokana na mshtuko wa jamii kuhusu umuhimu wa ardhi. Watu waliotoka vijijini na kuingia mijini baada ya fursa za sasa za mikopo na masilahi mengine yanayotolewa kwa dhamana ya ardhi, wanaibuka na kurudi vijijini kudai ardhi za maeneo ya ndugu zao.

 “Wananchi wengi wanaishi katika maeneo yao yakiwa hayajapimwa. Akitokea mjanja anaenda analipima eneo kisha anapata hati za eneo hilo na kuja kuwafukuza wenye eneo. Wakishtuka wanakuta yeye ana hati, wanapoteza haki zao na kuibuka mgogoro,” amesema Ndunguru.

Amesema hali kama hiyo imekuwa ikitokea pia katika maeneo yenye madini, baadhi ya watu hununua au kujimilikisha maeneo baada ya kubaini uwepo wa rasilimali hizo, huku wananchi waliokuwa wakimiliki maeneo hayo kwa muda mrefu wakikosa nyaraka za kuthibitisha haki zao.

 “Unakuta mwekezaji anakuja kuwafukuza wananchi sehemu, halafu anakuwa na nyaraka zinazoonesha ana makubaliano yaliyosainiwa na wananchi kwenye mkutano wakati hawakukubaliana hivyo, mgogoro unaibuka,” amesema Ndunguru.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Ardhi, Cuthbert Tomito amesema changamoto kubwa inayochochea migogoro hiyo ni udhaifu wa usimamizi wa sheria na sera za ardhi pamoja na ukosefu wa elimu kwa umma kuhusu haki za ardhi.

 “Ukiangalia viongozi wa Serikali za mitaa wengi hawajengewi uwezo kuhusu masuala ya ardhi huku wakiwa na jukumu la kusimamia na kuidhinisha mauzo ya ardhi,” amesema Tomito.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro

 Pia, amesema hata urasimishaji wa ardhi uliofanyika Dar es Salaam uliolenga kupunguza migogoro bado haujaondoa tatizo hilo katika baadhi ya maeneo.

Tomito amesema kuziachia kampuni binafsi kununua na kuuza ardhi kumeongeza changamoto na migogoro mingi inayoshuhudiwa sasa.

Akizungumzia namna ya kumaliza tatizo hilo, Mwaihojo amesema Serikali inapaswa kuweka mkazo mkubwa katika usimamizi na utekelezaji wa sheria za ardhi badala ya kuacha wananchi wakihangaika mahakamani.

 Amesema halmashauri, viongozi wa vijiji na kata, wazee wa kimila na viongozi wa maeneo husika, wanapaswa kushirikishwa kusimamia umiliki wa ardhi kwa kuwa wanafahamu historia na mipaka ya maeneo ya wananchi.

 “Watumiwe pia viongozi wa Serikali za vijiji na halmashauri zao za maeneo husika, wakiwamo viongozi wa kimila, wahusishwe kwa kuwa wanayajua vizuri maeneo ya watu wao,” amesema Mwaihojo.

 Amesema athari za migogoro hiyo sasa ni kubwa kwa jamii kwa sababu zinasababisha mauaji, zinawapora watu maeneo ya kuishi, kuathiri ndoa, uwekezaji na hata usalama wa chakula kwa wananchi wanaoporwa mashamba yao.

 “Hata dhamira ya kupigania uhuru wa nchi ilikuwa kuhakikisha wananchi wanakuwa huru ndani ya nchi yao kupitia umiliki wa ardhi, ndiyo maana Mwalimu Nyerere aliitaifisha ardhi ili kuzuia wachache wenye nguvu kumiliki maeneo makubwa na kuwanyanyasa wanyonge,” amesema Mwaihojo.

 Kwa upande wake, wakili Ndunguru amesema Serikali inapaswa kuongeza kasi ya kupima maeneo ya wananchi na kuwapatia hati rasmi za umiliki ili kuondoa mianya ya utapeli, akitaka pia kuwepo masijala kuanzia ngazi ya kijiji na kata zitakazosimamia usajili wa mauziano ya ardhi na kuhifadhi taarifa kwenye mifumo rasmi ya Serikali.

 “Hii ya kumtaka mtu aliyepo Tunduru au Mutukula kwenda Dar es Salaam kuhakiki ardhi yake ni tatizo. Huduma zishuke hadi ngazi ya kijiji na kata,” amesema Ndunguru.

Kwa upande wake, Tomito amesema Serikali inapaswa kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji kuhusu sheria na sera za ardhi ili waweze kusimamia vizuri majukumu yao.

 “Haya maeneo ya usimamizi wa sheria na sera, utoaji wa elimu ya ardhi kwa umma na viongozi ngazi ya jamii pamoja na kuweka utaratibu bora wa kampuni binafsi kununua na kuuza ardhi, ni suluhisho muhimu kwenye suala hili,” amesema Tomito.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *