
Dar es Salaam. Adhabu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia ni moja tu, nayo ni kunyongwa hadi kufa, hayo ni maneno ya Jaji Arnold Kerekiano wakati akimhukumu adhabu ya kifo, mkazi wa Mburahati NHC jijini Dar es Salaam.
Ukisoma namna mauaji ya Maulid Omary (45) yalivyofanyika, unaweza usiamini aliyefanya hivyo alikuwa na akili timamu, lakini ukweli ni kuwa Saimon Ayuke amethibitika ndiye aliyemchinja Maulid kwa kisu shingoni hadi kupoteza maisha.
Lakini wawili hao walikutanaje, kulingana na maelezo yake ya ungamo, Ayuke anadai siku ya tukio Januari 7, 2025 wakati anarejea nyumbani saa 6:20 usiku, huko Mburahati NHC, alimkuta kijana mmoja amelala barazani katika nyumba ya jirani.
“Hapo nyumbani kwetu nyumba ya jirani, nikamkuta kijana mmoja akiwa amelala barazani na mimi nikamchukua na kuingia naye ndani kwetu na nikampeleka mpaka uani, baada ya kufika nikachukua kisu na kumlaza chini,” anaeleza.
“Nikamkanyaga miguu yake na kuanza kumchinja shingo mpaka akafa na mama alikuwa dirishani kwa ndani akaniambia wewe unafanya nini hapo huyo mtu. Baada ya huyo mtu kufa nikamchukua na kumtumbukiza katika shimo la choo,” amesema.
Maelezo hayo ya ungamo aliyoyatoa polisi na baadaye kwa mlinzi wa amani, ni sehemu ya ushahidi ambao Jaji Kirekiano wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, aliyatumia kumtia hatiani mshitakiwa kwa mauaji ya kukusudia.
Kesi hiyo iliendeshwa na jopo la mawakili watatu wa Serikali ambao mawakili waandamizi wa Serikali, Nitike Waisaka na Sofa Bimbiga wakisaidiana na wakili wa Serikali Lucas Makori, huku mshitakiwa akitetewa na wakili Agatha Fabian.
Nini kilitokea NHC Mburahati
Katika hukumu yake aliyoitoa jana Jumatatu Mei 25, 2026, Jaji alisema kabla ya kifo chake, Maulid (45) alikuwa anaishi eneo la Mburahati NHC na aliwahi kuwa dereva lakini mambo hayakumwendea vizuri na kuishia kukusanya chupa zilizotumika mtaani.
Maisha yake yalikatizwa kikatili Januari 7, 2025 saa sita usiku na mwili wake ulitolewa kutoka kwenye shimo la maji taka katika makazi ya mshtakiwa, Mburahati NHC na ulikutwa na majeraha mabaya kwenye shingo yake.
Siku hiyo, shahidi namba 3, Mrakibu wa Polisi (SP), Rumanyika ambaye alikuwa mkuu wa Polisi Buguruni, alipokea taarifa kuwa kuna mwanamke ametoa taarifa katika kituo hicho kuwa mtoto wake wa kumzaa alikuwa amemchinja mtu.
Alipofika kituoni, alimkuta shahidi namba 4, Pamela Ayuke ambaye ni mama mzazi wa mshitakiwa ambaye alimweleza kuwa amemuona mtoto wake aitwaye Simon Ayuke, akimchinja mtu ndani ya uwa katika nyumba wanayoishi.
SP Rumanyika wakiongozana na maofisa wengine wa polisi, walikwenda eneo la tukio na walipofika walimuona mtuhumiwa ambaye alikiri mbele yao kufanya mauaji hayo na kwenda kuwaonyesha eneo la maji taka alipoutupa mwili.
Ushahidi mzito wa mama
Shahidi namba 4, Pamela Ayuke ambaye ni mama mzazi wa mshitakiwa, aliiambia Mahakama kuwa yeye anaishi na kijana wake huyo eneo hilo la Mburahati NHC.
Alieleza siku ya tukio, akiwa nyumbani anaangalia televisheni, alisikia kishindo katika geti lao na kwa msaada wa mwanga wa taa ya umeme, aliona mtu amelala chini na alipomuuliza huyo mtu ni nani, alimtaka aende kulala.
Kutokana na kile alichokishuhudia, aliamua kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi Mburahati, kwamba kuna mtu yuko chini ya udhibiti wa mwanaye na walikuwa na hofu kuwa atampiga, hivyo polisi waliongozana naye hadi eneo la tukio.
Alipofika nyumbani akiwa ameongozana na polisi, hakumuona yule mtu pale chini, na polisi walipofanya ukaguzi katika eneo hilo walikuta mwili wake ukiwa katika mtaro wa majitaka na alimsikia mtoto wake akisema ni yeye alimuua.
Mashahidi wengi wa Jamhuri
Katika ushahidi wake, shahidi namba 1, Dk Robert Malima aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alisema mwili ulikuwa na majeraha shingoni na sababu za kifo ni mshituko wa kukatwa kwa mishipa na sehemu kubwa ya shingo yake.
Kwa upande wake, shahidi namba 9, namba E. 6052 Sajenti Kushoka aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, alisema mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo katika maelezo yake ya onyo aliyoyaandika polisi yaliyopokewa kama kielelezo P4.
Pia ndiye aliyechora ramani ya eneo la tukio ambayo ni kielelezo P3 kinachoashiria kuwa shahidi namba 4 (mama wa mshitakiwa) alikuwa mita chache kutoka eneo mauaji yalipofanyika kiasi cha kuweza kuona kilichokuwa kikitokea pale uani.
Shahidi namba 2, Veronika Mawole ambaye ni mlinzi wa amani na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Magomeni, alieleza namba mshitakiwa alivyopelekwa kwake na kuandika maelezo yake ya ungamo au Extra judicial Statement.
Kulingana na shahidi huyo, mtuhumiwa huyo alikiri kumuua mtu ambaye hakuwa anamfahamu jina, kwa kumkata shingo na kutupa mwili wake shimo la maji taka.
Mshitakiwa alivyojitetea
Katika utetezi wake mahakamani, mshitakiwa alieleza kuwa siku ya tukio usiku wa manane akiwa nyumbani, alisikia sauti ya kishindo nje ya nyumba yao.
“Alipokuwa anashangaa na kujiuliza nini kimetokea, aliona mzigo kama mwili wa binadamu ukitupwa kwenye eneo lao, akarudi kulala. Muda mfupi, timu ya polisi ilifika ilianza kumpiga na kumhoji yeye,” alisema Jaji akunukuu ushahidi wake.
“Alisema polisi walikuta mwili wa binadamu kutoka kwenye shimo la maji taka ambalo halikuwa likitumika wakati huo. Alisema, maofisa wa polisi walianza kumpiga na kumpeleka kituoni cha Polisi pale Mburahati,” aliendele kumnukuu.
Mshitakiwa huyo katika utetezi wake alisema hakuwahi kukiri mbele ya polisi wala mbele ya Hakimu Mawole na kwa hali hiyo, alipelekwa Hospitali ya Mirembe kwa uchunguzi wa akili lakini hakuulizwa lolote na na daktari aliyemhudumia.
Hukumu ya Mahakama
Katika hukumu yake, Jaji Kirekiano alisema kuna ushahidi usiobishaniwa kuwa siku ya tukio, polisi wakiongozana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, waliweza kutoa mwili wa marehemu ukiwa katika shimo la maji taka.
Jaji alisema katika hatua hiyo, mshitakiwa alijiweka kando kabisa na chochote kilichotokea kwa marehemu na hakukuwa na simulizi nyingine na ni kutokana na hilo, hakuna ubishi Maulid Omary ni marehemu na kifo chake hakikuwa cha asili.
“Ni lazima ifahamike kuwa huu mwili ulikutwa katika shimo la maji taka kama ilivyoelezwa na mashuhuda, shahidi namba 4 na maofisa wa Polisi na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walioutoa mwili huo kwenye shimo hilo,”alisema Jaji.
Jaji alisema maelezo ya mshitakiwa yalikuwa hayashawishi kwa sababu kama kulikuwa na mwili ulirushwa kwenye nyumba yao, uliendaje kwenye shimo la maji taka na kwamba sio kawaida mwili wa mwanadamu kutupwa kama taka.
Lakini pia Jaji alisema maelezo yake yalionekana kupingana na yale ya shahidi namba 4 ambaye ni mama yake mzazi ambaye alisema mshtakiwa alikuwa na mtu kwenye bustani uani ambaye mtu huyo alikutwa kwenye shimo la maji taka.
“Hivyo nashikilia kwamba majeraha katika mwili wa marehemu na namna alitolewa kwenye shimo hilo ni kuthibitisha bila shaka kwamba kifo cha marehemu haikuwa ya asili bali ilisababishwa na kitendo kisicho halali na cha kikatili,”alisema.
Jaji alisema katika hatua hiyo, Mahakama inawajibu wa kupima ushahidi na kuamua ni nani alimuua marehemu na kwamba hadithi ilianzia kwa mama yake mzazi, ambaye alisema alimuona mshitakiwa na akiwa na mtu kule uani.
“Aliiambia Mahakama hii kwamba alimwona mshtakiwa akiwa na mtu kwenye nyasi, mshtakiwa alimwambia akalale, lakini yeye alikimbilia polisi kuripoti.”
“Wakati yeye hakuiambia Mahakama hii wazi kwamba alimwona mshtakiwa akikatakata koo la marehemu. Matukio yaliyotokea eneo la tukio baada ya polisi kufika kuthibitisha wasiwasi wake, yanaunga mkono mashaka yake,” alisema Jaji.
Mashahidi waliokuwepo eneo la tukio wakiwamo maofisa wa polisi na wale wa Zimamoto na Uokoaji, walieleza kuwa mshitakiwa alikiri kufanya mauaji hayo na mama yake mzazi ndio mtu wa kwanza kutoa taarifa polisi juu ya mauaji hayo.
“Nina shawishika kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuhitimisha kuwa mtuhumiwa alikuwa muuaji. Utetezi wake kuwa mwili ulitupwa na yeye akaenda kulala umezingatiwa lakini haushawishi,” alisema Jaji Kirekiano.
Jaji Kirekiano alisema upo ushahidi wa maelezo ya onyo ya mshitakiwa ambayo alikiri kutenda kosa hilo na kuoanisha na ushahidi mwingine ikiwamo taarifa ya uchunguzi wa daktari, inaoana na yale ambayo mshitakiwa aliyaeleza.
Katika hoja ya mwisho, Jaji alisema Mahakama imethibitisha alitenda kosa hilo akiwa na nia ovu kutokana na dhamira yenyewe ya kufanya mauaji au kudhuru mwili wa mtu ama iwe ni mtu mwenyewe aliyekufa au mtu mwingine.
Pia yeye kufahamu kuwa amesababisha kifo au madhara mwilini kwa mtu, aina ya silaha aliyoitumia, maeneo hatari ya mwili aliyoshambulia, kunathibitisha uwapo wa nia ovu hivyo Mahakama inamtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo.
