
NYOTA wa JKT Stars, Jesca Ngisaise ameendelea kudhihirisha ubora wake wa kutupia, baada ya kufunga pointi 94 katika mechi mbili za Ligi ya kikapu Dar es Salaam kwa Wanawake (WBDL).
Ngisaise aliyechipukia katika kituo cha Ukonga Akademy, ligi ya mwaka jana aliibuka mfungaji bora akiwa na pointi 584, akifuatiwa na Elina Sinasega wa Twalipo Queens aliyefunga pointi 353.
Pia nyota huyo aliongoza kwa kufunga mitupo ya pointi tatu na kufikisha 59, akifuatiwa na Irene Gerwin wa DB Troncatti aliyefunga 38.
Katika mechi ya kwanza mwaka huu ya ushindi mnono wa pointi 64-46 dhidi ya DB Troncatti, iliyopigwa Viwanja vya Donbosco, Upanga, alifunga pointi 28, huku dhidi ya UDSM Queens walioshinda 145-28, alifunga pointi 66.
Alifuchua kinachombeba kwenye ufungaji ni mazoezi binafsi ya kufunga anayofanya kabla ya kuanza ya pamoja na timu.
“Kwa kweli kama unataka uwe mfungaji, unatakiwa ujitoe, ni pamoja na kupanga muda wako wa mazoezi, bila ya hivyo huwezi ukafanya vizuri,” alisema Jesca.
