
ar es Salaam. Kukua na kuenea kwa harakati za haki za binadamu kumeendelea kuchochea mjadala kuhusu adhabu ya viboko shuleni, lakini hali imeendelea kuwa tata, ikigonganisha maadili ya jadi ya nidhamu kwa watoto na mitazamo mipya ya haki na ustawi wao.
Ndani ya mvutano huo, historia ya adhabu hii inafungua pazia la safari ndefu, kutoka malezi ya kale, dini, ukoloni hadi mijadala mikali ya sasa duniani.
Kabla ya kuanzishwa kwa shule rasmi, malezi ya mtoto yalikuwa jukumu la familia na jamii.
Katika ustaarabu wa kale wa Roma na Ugiriki, nidhamu ya mtoto ilihusishwa moja kwa moja na mamlaka ya mzazi.
Wanahistoria wa elimu wanaeleza kuwa walimu walipoanza kuibuka, walirithi mamlaka hayo kupitia dhana ya Mwalimu ni kama mzazi kwa mwanafunzi, wakiruhusiwa kuadhibu watoto kama wazazi wao.
Katika mazingira hayo, adhabu ya mwili ilionekana kama njia ya haraka ya kufundisha utii na heshima, mtazamo ulioendelea kutumiwa katika mifumo ya elimu kwa karne nyingi.
Misingi ya kidini
Dini zilitoa uhalali wa kimaadili kwa matumizi ya viboko. Kitabu cha Biblia katika Methali 13:24 inasema: “Yeye asiyetumia fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha.”
Kauli kama hii imekuwa ikitafsiriwa kwa muda mrefu kuonesha kuwa adhabu ya mwili ni sehemu ya malezi sahihi.
Kwa mujibu wa kazi za kitafiti za wanazuoni wa dini, tafsiri hizi zilifanya viboko kuonekana si ukatili, bali wajibu wa mzazi au mlezi katika kumjenga mtoto.
Katika jamii nyingi za Kiafrika kabla ya ukoloni, nidhamu haikutegemea sana viboko kama chombo kikuu, ingawa baadhi ya jamii zilitumia zaidi adhabu ya viboko.
Kwa sehemu kubwa malezi yalikuwa ya kijamii, yakihusisha wazazi, wazee na jamii nzima. Watoto walifundishwa kupitia hadithi, methali na majukumu ya kila siku.
Watafiti wa anthropolojia wanaeleza kuwa viboko vilitumika kwa nadra na kwa tahadhari, lengo likiwa kurekebisha tabia bila kuharibu utu wa mtoto.
Viboko shuleni
Kadiri mfumo wa elimu ulivyokua Ulaya, hasa kuanzia karne za kati hadi karne ya 19, viboko vilianza kuwa sehemu ya kawaida ya nidhamu shuleni.
Kwa mujibu wa tafiti za kihistoria, Uingereza iliongoza kuhalalisha mfumo huu na baadaye kuusambaza katika makoloni yake.
Afrika ilipoingia katika mfumo wa elimu ya kikoloni, viboko vilipokelewa kama sehemu ya kanuni za shule.
Ndani ya darasa, mwalimu alipewa mamlaka makubwa, na viboko vikawa chombo cha kudhibiti nidhamu kwa haraka na kwa nguvu.
Sababu kuu zilikuwa imani kuwa maumivu hujenga nidhamu, pamoja na ukosefu wa uelewa wa kisayansi kuhusu maendeleo ya mtoto.
Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa viboko vilionekana kama njia rahisi na ya haraka ya kudhibiti wanafunzi wengi katika mazingira ya darasa yenye msongamano.
Kuanzia karne ya 20, mabadiliko ya kisayansi na kijamii yalipoanza kuipa kipaumbele saikolojia ya mtoto, mjadala kuhusu viboko ulianza kushika kasi.
Hii ilisababisha baadhi ya taasisi za kimataifa kuanza kuingiza vifungu vya sheria katika mikataba yake kwa nchi wanachama wake vinavyokataza matumizi ya viboko kwa watoto.
Hatua hizo zilianza kujitokeza kwa baadhi ya mataifa ambapo, mwaka 1979, Sweden ilikuwa ya kwanza kupiga marufuku viboko kwa watoto, hatua iliyofuatwa na nchi nyingi za Ulaya.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, hadi sasa zaidi ya nchi 60 zimeondoa kabisa adhabu hiyo. Hata hivyo, katika sehemu nyingi za Afrika na Asia, viboko bado vinaruhusiwa, mara nyingi kwa masharti, huku mjadala ukiendelea kati ya kuvilinda na kuviondoa.
Wanaotetea viboko wanaamini vinaimarisha nidhamu na heshima kwa mamlaka. Lakini wapinzani wake wanasisitiza kuwa vinaongeza hofu na vinaweza kuathiri ustawi wa mtoto.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), adhabu ya mwili ina uhusiano na matatizo ya kisaikolojia na kitabia kwa watoto, jambo linalozidi kuibua mjadala mpana duniani.
Falsafa za elimu na mitazamo ya wanazuoni
Katika machapisho yake mbalimbali, mwanafalsafa John Locke aliwahi kuonya dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi katika malezi, akisisitiza kuwa elimu inapaswa kujenga akili badala ya kuumiza mwili.
Mwanafalsafa mwingine, Jean-Jacques Rousseau katika maandiko yake kuhusu elimu na malezi ya wanafunzi, alikuwa akihimiza malezi yanayozingatia asili ya mtoto na uhuru wake.
Mitazamo hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa mbinu mbadala za nidhamu zisizo za kimwili.
Hali ilivyo Tanzania
Tanzania bado inaruhusu viboko shuleni kwa kufuata taratibu maalum, lakini mjadala unaendelea kuongezeka.
Bado wapo wanaoona viboko ni msingi wa nidhamu ya mtoto, huku wengine wakitaka mabadiliko kwa kuzingatia haki za mtoto.
Kadiri dunia inavyoelekea katika mbinu mbadala za malezi, Tanzania nayo inakabiliwa na uamuzi mgumu; kuendelea na mfumo wa viboko au kubadili mwelekeo wake.
