
Dar es Salaam. Kwa miaka mingi mjadala kuhusu matumizi ya adhabu ya viboko shuleni na majumbani umekuwa ukiibuka mara kwa mara nchini.
Wakati wanaharakati wa haki za watoto, wanasaikolojia na baadhi ya wadau wa elimu wakitaka adhabu hiyo iondolewe wakidai ina madhara kwa makuzi ya mtoto, bado kundi kubwa la wazazi, walimu na jamii linaamini viboko ni sehemu ya malezi na nidhamu.
Licha ya Serikali kuweka miongozo ya namna ya utoaji wa adhabu hiyo, utekelezaji wake bado una changamoto kubwa, huku matukio ya wanafunzi kuadhibiwa kupita kiasi yakiendelea kuripotiwa.
Swali kubwa linalobaki ni kwa nini adhabu ya viboko inaonekana kuwa ngumu kukomeshwa Tanzania?
Kwa jamii nyingi za Kiafrika, Tanzania ikiwemo, viboko vimekuwa sehemu ya kawaida ya malezi kwa muda mrefu. Wazazi wengi waliadhibiwa kwa viboko walipokuwa watoto na wanaamini ndiyo njia iliyowasaidia kuwa na nidhamu.
Mwalimu mstaafu wa shule ya msingi, Athuman Mallya, anasema kizazi cha zamani kililelewa kwa ukali na adhabu za viboko zilikuwa sehemu ya maisha ya kawaida.
“Sisi tulipigwa viboko sana, lakini tuliheshimu wazazi na walimu. Leo watoto wengi wana haki nyingi lakini nidhamu inapungua. Ndiyo maana watu wengi wanaona viboko bado vina nafasi,” amesema.
Halima Omary ambaye ni mzazi, anaamini viboko vya kiasi vinaweza kusaidia kumrekebisha mtoto.
“Mtoto akikosea mara nyingine anatakiwa kuonyeshwa ukali. Ukimlea kwa kumuacha tu anaweza kuharibika. Tatizo si viboko, tatizo ni kupitiliza,” amesema Halima.
Mitazamo kama hiyo imeendelea kuwepo katika jamii nyingi, hali inayofanya juhudi za kukomesha adhabu hiyo kukutana na upinzani.
Kwa nini bado ni vigumu kukomeshwa?
Zipo sababu kadhaa zinazofanya adhabu ya viboko iendelee kuwepo, mazingira ya sasa ya ufundishaji yakitajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa adhabu hiyo kuendelea kutolewa.
Mwalimu wa shule ya sekondari jijini Mwanza ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wakati mwingine walimu hujikuta wakikosa mbinu mbadala za haraka za kudhibiti nidhamu.
“Unaweza kuwa na wanafunzi zaidi ya 80 darasani. Ukianza kufuatilia kila mwanafunzi mmoja mmoja kwa ushauri pekee inakuwa ngumu. Hapo ndipo baadhi ya walimu wanaona viboko ni njia ya haraka ya kurejesha nidhamu,” amesema mwalimu huyo.
Sababu nyingine ni changamoto za mfumo wa elimu wenye msongamano mkubwa wa wanafunzi, uhaba wa walimu wa ushauri nasaha na mazingira yanayowapa walimu mzigo mkubwa wa kusimamia nidhamu.
Pia, baadhi ya wazazi wenyewe huwapa walimu ruhusa ya kuwaadhibu watoto wao kwa viboko, jambo linaloonyesha jamii bado inaamini katika mfumo huo wa malezi.
Mwongozo wa Serikali
Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002 inampa mamlaka waziri wa elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa sheria hiyo. Moja wapo ya kanuni zilizotungwa ni The Education Corporal Punishment Regulation G.N. 294 ya mwaka 2002 ambazo zinatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani.
Kanuni ya 3(1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatoke utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.
Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne.
Sheria hiyo inampa mamlaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyoye kutoa adhabu hiyo.
Wadau wa elimu watofautiana
Ndani ya sekta ya elimu yenyewe, bado kuna mjadala mkubwa kuhusu uhalali wa adhabu ya viboko wapo wanaoamini kuondoa viboko kabisa kunaweza kuongeza utovu wa nidhamu mashuleni.
Rachel Muhina ambaye ni mwalimu wa sekondari mkoani Dodoma, Emmanuel Lusekelo, amesema kabla ya kuondoa viboko ni lazima kuwe na maandalizi ya kutosha.
“Huwezi kusema viboko vikome wakati shule nyingi hazina wataalamu wa ushauri nasaha wala mazingira ya kufuatilia watoto mmoja mmoja. Walimu wengi tayari wana mzigo mkubwa,” amesema.
Lakini kwa upande mwingine, baadhi ya wanaharakati wa elimu wanaamini muda umefika wa Tanzania kuachana na adhabu hiyo.
Mkurugenzi wa Save the Children Tanzania Angela Kauleni, amesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo hivyo, hasa katika mazingira ya kujifunzia.
“Adhabu za viboko, ikiwamo kupiga kwa fimbo, makofi na kudhalilisha kwa maneno, zinaendelea kuwaathiri watoto shuleni, madrasa na majumbani nchini Tanzania,” amesema Kauleni.
Amesema licha ya kuenea kwake, ushahidi unaonesha adhabu hizo haziboreshi nidhamu wala matokeo ya elimu, bali husababisha madhara makubwa kwa watoto na kuharibu mustakabali wao pamoja na ndoto zao.
Angela ambaye pia ni mwenyekiti wa muungano wa asasi za kiraia zinazopinga adhabu ya viboko amesema kulingana na utafiti walioufanya, zaidi ya asilimia 70 ya watoto nchini hupitia ukatili wa kimwili, huku walimu wakitajwa miongoni mwa wahusika wakuu katika mazingira ya shule.
Kauleni amesema tafiti zinaonesha adhabu za viboko husababisha hofu, kujitenga, kupungua kwa ushiriki darasani, kushuka kwa ufaulu pamoja na madhara ya muda mrefu ya kihisia na kisaikolojia.
“Adhabu za viboko zinadhoofisha utu wa mtoto na uwezo wake wa kujifunza na kufanikiwa. Kuzikomesha ni hatua muhimu katika kujenga mazingira salama na yenye ufanisi ya kujifunzia,” amesema Angela.
Mkurugenzi wa shirika Watoto Leo, Agnes Mhando, amesema dunia imebadilika na watoto wanahitaji malezi yanayozingatia haki zao.
“Tunapaswa kujenga nidhamu kwa mazungumzo, ushauri na mifumo bora ya shule. Viboko vinaweza kuacha majeraha ya kimwili na kisaikolojia,” amesema Mhando.
Hiki karibuni akizungumzia hilo, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania, (CWT), Suleiman Ikomba alisema adhabu hiyo ni nyepesi inayotolewa na mwalimu kwa utaratibu kwa mwanafunzi mwenye makosa.
“Nawaomba hao wadau wanapokuja na jambo wafikirie kwa kina, kulikuwa na maana kubwa ya kuwa na adhabu ya viboko, kwetu adhabu hii ina ufanisi mkubwa kwanza kumpunguzia mwalimu kazi, ya kufanya shughuli yake kwa ufanisi. Kusema atumie mbinu mbadala ni kumuongezea mwalimu mzigo kwa sababu ili iwe adhabu lazima usimamizi uwepo,” anasema Ikomba.
Kamishna wa Elimu Dk Lyabwene Mtahabwa aliwahi kulieleza gazeti hili kuwa kinachofanywa na Serikali ni kufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha mwongozo unatekelezwa kama ulivyotolewa.
Kulingana na mwongozo huo adhabu ya viboko kwa mwanafunzi inapaswa kutolewa na mwalimu mkuu au mkuu wa shule na havipaswi kuzidi vitatu.
“Kusema kwamba adhabu ya viboko itaondoka kabisa sio kweli, hilo linaweza kutokea huko siku za usoni lakini tunachofanya ni kuimarisha ufuatiliaji kuhakikisha adhabu hii inatolewa kulingana na mwongozo.
“Ufuatiliaji wetu utaongezeka maradufu, watakaokiuka watachukuliwa hatua. Hakuna kitu muhimu kwetu kama usalama wa mtoto hivyo wanajamii tunapaswa kushirikiana kwa kutoa taarifa pale unapofanyika ukatili ili hatua zichukuliwe,” amesema Dk Mutahabwa.
Kamishna huyoa aliongeza kuwa ufuatiliaji huo utaenda kuongezeka maradufu kwa wathibiti ubora wa elimu akifafanua kwamba wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuhojiwa yanapotokea matukio ya ukatili wa wanafunzi shuleni.
“Kama mthibiti ubora upo na shule yako ina kawaida ya kutoa adhabu kali basi wewe hufai, ni lazima kuwe na ufuatiliaji wa karibu kujua kinachoendelea shuleni,”.
Mtazamo kisaikolojia
Wanasaikolojia wanaonya kuwa matumizi ya viboko yanaweza kuathiri afya ya akili na maendeleo ya mtoto kwa muda mrefu.
Mwanasaikolojia wa elimu, Joyce Mrema, amesema watoto wanaopigwa mara kwa mara wanaweza kukua wakiwa na hofu, msongo wa mawazo au tabia ya kutumia ukatili wanapokutana na changamoto.
“Mtoto anapoadhibiwa kwa kipigo, anaweza kutii kwa sababu ya kuogopa, lakini si lazima awe ameelewa kosa lake. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa viboko vya mara kwa mara vinaweza kuathiri kujiamini kwa mtoto,” anasema Joyce.
Amesema pia baadhi ya watoto huanza kuwa wakorofi zaidi au kujenga chuki dhidi ya walimu na wazazi.
Kwa upande wake, mwanasaikolojia wa watoto, Lina Kibona, anasema jamii inahitaji kuwekeza zaidi katika malezi chanya na mawasiliano.
“Wazazi na walimu wengi hawajafundishwa mbinu mbadala za nidhamu. Ndiyo maana viboko vinaendelea kuonekana suluhisho rahisi. Lakini kuna njia nyingi za kumrekebisha mtoto bila kumuumiza,” amesema Lina.
