
Songwe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamtafuta mwanamke anayefahamika kwa jina la Queen Mbuba kwa tuhuma za mauaji ya mume wake, Shizya Mwangwale (35), mkazi wa Kijiji cha Igunda, Wilaya ya Mbozi.
Inadaiwa kuwa Shizya alichomwa sindano inayodhaniwa kuwa na sumu begani upande wa kushoto, kisha baadaye kuchomwa kisu tumboni upande wa kulia na mke wake, ambaye alitoroka mara baada ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema tukio hilo limetokea Mei 22, 2026 majira ya saa 9:00 usiku.
Inaelezwa kuwa pindi Shizya alipomuuliza mkewe kuhusu sindano hiyo, mtuhumiwa alidai kuwa ilikuwa ni dawa kwa ajili ya tatizo la miguu iliyokuwa inamsumbua marehemu.
Kamanda Senga amesema baada ya tukio hilo, Shizya alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kwa ajili ya matibabu na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya, ambapo amefariki dunia leo Mei 26, 2026 akiwa anapatiwa matibabu.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu Shizya kuwa na mahusiano na wanawake wengine,” amesema Kamanda Senga.
Amesema Polisi wanaendelea na msako wa kumkamata mtuhumiwa huyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa wito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo, pia linawakumbusha wananchi kuepuka vitendo vya kujichukulia sharia mkononi na badala yake kutumia njia sahihi za sharia na usuluhishi pale wanapokumbana na migogoro ya kifamilia au jamii.
