Natamani maprofesa wangekuwa wavuviNatamani maprofesa wangekuwa wavuvi

Dar es Salaam. Kuna wakati ukikaa ufukweni mwa bahari alfajiri, ukawaangalia wavuvi wakivuta nyavu zao huku jasho likiwatoka, unaweza kujifunza uchumi kuliko kusoma ripoti ya kurasa 200 ya “Sera Shirikishi ya Uwezeshaji wa Jamii katika Muktadha wa Mabadiliko ya Kidijitali.” 

Wavuvi hawana semina za hoteli za nyota tano. Hawavai makoti yenye tai zinazobana shingo kama mtu anayesubiri hukumu ya kunyongwa. 

Hata hivyo, kila siku wanafanya jambo ambalo Taifa linahitaji kuliko hotuba nyingi: wanazalisha ajira.

Ndiyo maana wakati mwingine natamani maprofesa wetu wangekuwa wavuvi.

Mvuvi akiamka saa tisa usiku kwenda baharini, hafanyi utafiti wa “athari za mwanga wa mwezi katika saikolojia ya dagaa.” 

Anaenda kuvua samaki. Akirudi, shughuli zinaanza kama sikukuu ya uchumi wa watu wa kawaida. Kuna anayepokea samaki bandarini. Kuna anayebeba kwenye toroli. 

Kuna mama anayekaanga samaki pembeni ya barabara. Kuna wauzaji wa barafu. Kuna mafundi wa nyavu. Kuna wenye bodaboda wanaosambaza mzigo sokoni. 

Kuna wanawake wanaouza kwa rejareja. Kuna hadi paka wa mtaani wanaopata ajira ya kusubiri mifupa.

Samaki mmoja anaweza kuajiri watu 10 kabla hajafika kwenye sahani. Mvuvi hana PhD ya Marekani wala ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Lakini anajua kitu kimoja muhimu: kazi yake lazima ionekane kwenye maisha ya watu.

Leo ukienda  Kigamboni, Bagamoyo, Kilwa, Mwanza au Mafia, utakuta uchumi wa watu wengi umezunguka sekta ya uvuvi. 

Hata yule kijana aliyeshindwa kidato cha nne,  anaweza kupata hela ya kula kwa kuuza samaki wawili wa kukaanga jioni. Hakuna anayemuuliza “umechapisha makala ngapi kwenye majarida ya kimataifa” Wanamuuliza: “Samaki wameingia?”

Shida yetu

Hapo ndipo ninapopata shida kidogo na mfumo wetu wa elimu ya juu.

Vyuo vikuu vimejaa maprofesa wenye vyeo virefu kuliko foleni ya magari barabarani. 

Ona cheo hiki: Profesa Mshiriki wa Utafiti Shirikishi wa Mabadiliko ya Tabianchi katika Jamii Zinazoathiriwa na Uchumi wa Bahari na Maziwa.

Ukimsikiliza dakika tano unaweza kudhani kesho asubuhi Tanzania itakuwa kama Dubai. Lakini ukiangalia nje ya geti la chuo, utakuta vijana ‘wanachana mikeka’

Tatizo si kwamba maprofesa hawana akili. Hapana. Wengi ni watu wenye uwezo mkubwa sana. Tatizo ni kwamba akili zao mara nyingi zinaishia kwenye makabrasha, semina na kupanda vyeo na madaraja ya kitaaluma.

Leo hii maprofesa wengi wanakimbizana na “research grants” kama vile wafanyabiashara wanavyokimbizana na zabuni. Ukienda vyuoni utakuta watu wanahangaika kuandika proposal kuliko kutafuta suluhisho la maisha ya wananchi. 

Kila mwezi kuna warsha kuhusu “capacity building”, “stakeholder engagement”, na “policy dialogue.” Lakini kijana wa mtaani bado hajui atakula nini kesho.

Wakati mvuvi akitupa nyavu baharini, profesa anatupa proposal kwa wafadhili.

Tofauti ni kwamba nyavu za mvuvi hurudi na samaki. Proposal nyingi hurudi na ‘mshiko’

Hii si dharau kwa elimu. Taifa lisilo na wasomi ni taifa lililofumba macho gizani. Lakini elimu ambayo haiwezi kugusa maisha ya watu wa kawaida nayo ni kama mwamvuli wenye matundu wakati wa mvua. Unavutia kuutazama, lakini haumkingi mtu.

Tuwe wakweli kidogo

Ni  kazi za kitafiti ngapi zimewahi kubadilisha maisha ya mama lishe wa Kariakoo? Ni miradi mingapi ya vyuoni imezalisha ajira zinazoweza kuonekana kwa macho? 

Mara nyingi tunasikia kuhusu uzinduzi wa utafiti, makongamano ya kimataifa na machapisho kwenye majarida ya nje. Lakini hatuoni viwanda vipya. Hatuoni vijana wakiajiriwa. Hatuoni ubunifu unaoshuka mpaka kwenye mitaa ya kawaida.

Ukimuuliza profesa yeyote kwa nini vijana hawana ajira, atakuonyesha wasilisho lenye grafu za rangi na majedwali yaliyosheheni namba. Ukimuuliza mvuvi swali hilo hilo, anaweza kukuambia: “Njoo kesho saa kumi alfajiri, twende baharini.”

Hii ndio tofauti ya nadharia na maisha.

Wavuvi wana changamoto nyingi. Wanakosa mitaji, vifaa vya kisasa, hifadhi ya samaki, masoko ya uhakika na wakati mwingine hata usalama.

Lakini pamoja na hayo, bado wanaendelea kuzungusha uchumi wa watu wadogo. Serikali ikiwekeza vizuri kwenye uvuvi, maelfu ya ajira zinaweza kuzalishwa ndani ya muda mfupi sana.

Lakini sisi tunaonekana kupenda zaidi mikutano kuliko matokeo.

Nchi yetu imejaa ripoti kuliko viwanda. Tuna makabrasha mengi kuliko ajira. Kuna watu wanaweza kuandika kurasa 100 kuelezea umaskini bila hata kumwajiri maskini mmoja.

Hapa ndipo ninaposema: natamani maprofesa wangekuwa na roho ya wavuvi.

Mvuvi akiona samaki wamepungua, hubadili mbinu. Profesa akiona mradi hauleti matokeo, huandika repoti nyingine kuelezea kwa nini matokeo hayakuonekana kutokana na “logistical constraints.”

Mvuvi anafanya kazi kwa matokeo. Bahari haidanganyi; ama umepata samaki au hujapata.

Lakini kwenye mfumo wa kitaaluma unaweza kufanya semina miaka mitano kuhusu kilimo cha nyanya bila hata kupanda mti mmoja wa nyanya.

Tatizo jingine ni kwamba kazi nyingi za kitafiti zinaonekana kuandaliwa kwa ajili ya wafadhili, si wananchi. Mada zinafuata fedha zilipo.

 Leo kukiwa na fedha za mabadiliko ya tabianchi, kesho kila mtu anafanya utafiti wa eneo hilo. Kesho kutwa kukiwa na fedha za uchumi jumuishi  ghafla kila pendekezo linahamia huko.

Wakati huo kijana wa Tandale anatafuta mtaji wa Sh50,000 wa kuanzisha biashara.

Nchi haiendi kwa makaratasi

Nchi haiwezi kuendelea kwa makaratasi peke yake. Tunahitaji elimu inayotengeneza suluhisho halisi. Tunahitaji vyuo vikuu vinavyotoa teknolojia rahisi kwa wakulima, wavuvi na wafanyabiashara wadogo.

 Tunahitaji maprofesa wanaoshuka mashambani, sokoni na viwandani;  si wale wanaojua zaidi viwanja vya ndege vya ughaibuni kuliko vijiji vya hapa nchini.

Fikiria kama kila chuo kikuu kingekuwa na mradi mmoja mkubwa wa uzalishaji unaoajiri vijana moja kwa moja. 

Fikiria kama tafiti zingelazimika kuonyesha matokeo ya kiuchumi kwa wananchi ndani ya miaka miwili. 

Fikiria kama profesa angepimwa si kwa idadi ya machapisho pekee, bali kwa idadi ya watu aliowasaidia kujiajiri.

Pengine tungeanza kuona maana ya elimu.

Kwa sasa, wakati mwingine hali inachekesha kidogo.Mvuvi anayetumia mashua ya mbao anaweza kuwa na mchango mkubwa wa moja kwa moja kwa uchumi wa mtaa kuliko mtu mwenye ofisi yenye kiyoyozi na cheo kirefu cha kitaaluma.

Mvuvi akifanikiwa, mtaa mzima unanuka samaki. Profesa akifanikiwa kupata ruzuku, tunahesabu magari na majumba!

Hata lugha zao ni tofauti. Mvuvi akisema “leo tumepata sana,” watu wanaona samaki kwa macho. Profesa akisema “tumepata fund” mara nyingi kinachoonekana kwanza ni safari kwenye makongamano.

Bado nina imani

Lakini bado nina matumaini. Vyuo vikuu vinaweza kuwa injini kubwa ya maendeleo kama vitaamua kutoka kwenye ulimwengu wa makabrasha na kuingia kwenye maisha ya wananchi. Wasomi wetu wana uwezo mkubwa wa kubuni teknolojia za kuongeza thamani ya mazao, kuboresha shughuli za kiuchumi, kufungua viwanda vidogo, na kuanzisha mifumo ya biashara inayowawezesha vijana.

Tatizo si ukosefu wa akili. Tatizo ni ukosefu wa mwelekeo.

Bahari inamfundisha mvuvi ukweli mmoja muhimu: huwezi kula nadharia.

Nchi yetu inahitaji zaidi matokeo kuliko majina makubwa ya miradi. Tunahitaji kuona tafiti zikigeuka ajira. Tunahitaji kuona elimu ikizalisha uchumi. 

Tunahitaji kuona profesa anayewaza jinsi kijana wa kawaida atapata kipato, si jinsi ya kuongeza ‘citation’ kwenye ‘journal’

Ndiyo maana bado narudia:

Natamani maprofesa wangekuwa wavuvi.

Si kwa sababu kuvua ni rahisi kuliko kufundisha. Hapana. Bali kwa sababu wavuvi wana uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya watu. 

Kila wanachofanya kinaonekana mezani, sokoni na mifukoni mwa wananchi.

Labda siku moja tutafika mahali ambapo chuo kikuu kitakuwa kama bandari ya samaki;  sehemu ambayo watu hawaondoki na vyeti pekee, bali pia matumaini ya maisha bora.

Nisisitize: Maprofesa katika makala haya,  ni kiwakilishi tu cha wasomi wetu kwa jumla walio vyuoni,  ambao tunawategemea kujenga mustakabali mzuri wa Taifa.

0754990083

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *