
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Uapisho huo umekamilisha uteuzi wake wa majaji tisa aliowateua hivi karibuni kujiunga na Mahakama hiyo ya juu zaidi nchini.
Akizungumza leo Jumanne Mei 26, 2026 katika hafla hiyo muda mfupi baada ya kuwaapisha, Rais Samia amesema majaji hao wamepata uteuzi huo kutokana utumishi wao uliotukuka ndani ya Mahakama, akiwataka kwenda kuimarisha utendaji wa haki na kulinda uhuru wa mhimili huo.
“Nendeni mkaitumikie nchi kwa uzalendo, werevu bila upendeleo, huba na chuki katika kutoa maamuzi ya hukumu zenu.
“Mna dhima kubwa kwa nchi hii katika kutenda haki kuhakikisha haki za wananchi zinatimia,” amesema.
Rais Samia amesema kutimiza haki ni kutimiza kusudi la Mungu akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutaongeza ufanisi katika mhimili wa Mahakama nchini.
“Uteuzi wenu ni kuongeza uwezo wa watu wa kufanya kazi katika kusimamia haki,” amesema Rais Samia.
Aidha, amewataka majaji hao kwenda kulinda heshima na uhuru wa mahakama, akisisitiza ufanisi na weledi katika utumishi wao ambao amesisitiza uzingatie utu, taifa na nchi.
“Uamuzi wenu uzingatie utu kwanza, Taifa kwanza, nchi kwanza,” amesisitiza.
Hafla hiyo iliyofanyika saa nne asubuhi, imehusisha viapo vya majaji wote tisa ambao ni Jaji Imani Aboud, Jaji Rabia Mohamed na Jaji Dk Yose Mlyambina.
Wengine ni Jaji Immaculata Banzi, Jaji Cyprian Mkeha, Jaji Yohane Masara na Jaji Dk Juliana Masabo, Jaji Abdi Kagomba na Jaji Mzee Ibrahim.
Uapisho huo umehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka serikalini akiwemo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi na viongozi wengine kutoka kwenye mhimili wa Mahakama.
