
Sweden imekuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kujitangaza kuwa iko “huru kutoka kwenye tumbaku.” Kulingana na ripoti iliyochapishwa siku ya Jumatatu na Baraza la Habari kuhusu Pombe na Dawa za Kulevya la Sweden, chini ya 5% ya Wasweden huvuta sigara kila siku. Kizingiti hiki cha mfano pia kimewekwa na Shirika la Afya Duniani. Hata hivyo, kupungua kwa uvutaji sigara hakuhusiani kabisa na kupungua kwa matumizi ya nikotini.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Stockholm, Ottilia Ferey
Katika miaka ishirini, idadi ya wavutaji sigara kila siku nchini Sweden imeshuka kutoka 16% hadi 4.8%. Lakini nyuma ya ushindi huu kuna ukweli mwingine: mmoja kati ya Wasweden wanne bado hutumia nikotini kila siku.
Maelezo ya msingi ni “snus,” tumbaku ya mdomoni (aina ya tumbaku ambayo haivutwi, bali inatumika mdomoni), ambayo ni maarufu sana nchini Sweden. Imepigwa marufuku katika Umoja wa Ulaya tangu mwaka 1992, lakini Sweden iliruhusiwa kwa matumizi ya aina hiyo ya tumbaku ilipojiunga na EU miaka mitatu baadaye. Na katika miaka ya hivi karibuni, “snus nyeupe,” isiyo na tumbaku lakini yenye nikotini nyingi na mara nyingi yenye ladha, imekuwa maarufu sana miongoni mwa vijana na wanawake.
Kulingana na ripoti hiyo, karibu 19% ya Wasweden hutumia snus kila siku, ikilinganishwa na 12% mwaka wa 2007. Miongoni mwa wanawake, matumizi haya yameongezeka hata mara tatu katika kipindi cha chini ya miaka ishirini.
Mamlaka ya afya inasema kwamba ingawa hatari za sigara zinajulikana, athari za muda mrefu za bidhaa mpya za nikotini bado hazijarekodiwa vizuri. Mauzo ya snus nyeupe yameongezeka kwa 180% katika kipindi cha miaka mitatu nchini Sweden, na mauzo ya bidhaa za uvutaji sigara kwa 640%.
