Uganda: Juhudi za kutafuta chanjo dhidi ya Ebola (Bundibugyo) zaimarishwaUganda: Juhudi za kutafuta chanjo dhidi ya Ebola (Bundibugyo) zaimarishwa

Wanasayansi nchini Uganda, wameongeza kasi ya kutafuta chanjo ya virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo vilivyoripotiwa nchini DRC, wakati huu wizara ya afya nchini humo ikisema mgonjwa mmoja kati ya watano walioshukiwa kuwa na Ebola ameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya vipimo kuonesha hana maambukizi.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kwa sasa Ebola aina ya Bundibugyo ambayo imezuka DRC na Uganda haina chanjo lakini kulingana na Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya utafiti wa virusi Profesa Pontiano Kaleebu juhudi zinaendelea kutatua tatizo hili.

Profesa Pontiano Kaleebu, Ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Virusi nchini Uganda.

“Kwa Ebola Bundibugyo, ambayo ni mlipuko wa sasa, kuna chanjo mbili ambazo zinajaribiwa. Moja inatumika sawia na ile chanjo ya Ebola Zaire na nyingine ni Chadox iliyotengenezwa na wenzetu wa Oxford. Pia tunajadili kuchanganya chanjo ya Ebola Zaire na Ebola Sudan. Hii itakuwa kwenye maabara thabiti kuona kama mchanganyiko huu unaweza kukinga watu dhidi ya Ebola aina ya Bundibugyo” Alisema Profesa Pontiano Kaleebu.

Wakati huo huo, wizara ya afya inasema mmoja wa wagonjwa watano wa Ebola waliokuwa wamelazwa ameruhusiwa kuondoka hospitalini.  Mkurugenzi Mkuu wa huduma za afya Dkt Charles Olaro amethibitisha.

“Mgonjwa mmoja anaondolewa kwenye kitengo cha matibabu leo. Hana Ebola tena na tumebaki na wagonjwa wanne katika kitengo cha matibabu. Washiriki wao walio katika hatari kubwa wapo kwenye karantini. Nataka kuuhakikishia ulimwengu kuwa tutadhibiti mlipuko huu haraka iwezekanavyo. ” Alisema Dkt Charles Olaro

Huku mlipuko wa Ebola ukiendelea kuwa tishio katika eneo la Maziwa Makuu, taasisi ya utafiti wa virusi nchini Uganda ina mipango ya kutuma maabara zinazohamishika Mashariki mwa DRC kusaidia kutambua wagonjwa kwa haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *