Dar es Salaam. Waswahili husema ahadi ni deni. Licha ya kuwa mwanamuziki wa Bongo Fleva Diamond amefanya mengi yenye mafanikio kwenye muziki wa Bongo bado kuna deni kubwa analodaiwa na mashabiki wake. Twende pamoja
Busta Ryhmes, Akon & Wiz Khalifa
Baada ya kuhudhuria hafla ya utoaji wa tuzo za BET 2021 ambapo aliwaniwa kipenge cha Best International Act, Diamond alionekana studio na wasanii wakubwa Marekani kama Busta Ryhmes, Akon na Wiz Khalifa.
Walichofanya studio hadi sasa hakijasikika, mashabiki wengi walitarajia kolabo hizo zingesikika kwenye EP yake, First of All (FOA) iliyotoka Machi 2022 lakini haikuwa hivyo hata kwa ngoma zilizofuata baadaa ya hapo.
Hata hivyo, Meneja wake, Sallam SK alisema walipanga Diamond asimshirikishe msanii yeyote katika EP hiyo. Hivyo hata waliopata nafasi hiyo kama Zuchu na Mbosso ilikuwa basi tu!, ila kolabo zaidi zitakuwa kwenye albamu yake ijayo.
WCB Wasafi Kenya
Ni miaka nane sasa tangu Diamond kutangaza atafungua tawi la WCB Wasafi nchini Kenya kwa lengo la kuinua vipaji vipya katika muziki lakini hadi sasa bado hilo halijatimia, hili ni deni lingine kubwa kwa mashabiki wake wa 254.
“Kama mnavyofahamu mwaka huu (2018) WCB Wasafi tunafungua tawi jipya nchini Kenya maalumu kwa ajili ya kuendelea kunyanyua vijana wenzetu wenye vipaji tokea mtaani, tafadhali nisaidie kuwatag vijana wote wenye vipaji Kenya,” alisema Diamond.
Diamond alitoa kauli hiyo Februari 2018 kupitia Instagram ikiwa ni muda mfupi tangu aliyekuwa mpenzi wake na mzazi mwenziye, Zari The Bosslady kutangaza kuachana naye ikiwa tayari wamejaliwa watoto wawili.
Swahili Fest
Septemba 2021 Diamond alitangaza ujio wa tamasha lake jipya, Swahili Festival baada ya kuendesha Wasafi Festival kwa miaka zaidi ya mitano kwa mafanikio, lakini hadi sasa tamasha la Swahili Fest halijafanyika hata mara moja!.
Tangu awali Diamond alieleza lengo lake kuu ni siku moja kuja kuwa na tamasha kubwa litakaloweza kuutangaza vizuri muziki wa Bongofleva ndani ya Tanzania na kimataifa, hilo ni deni ambalo bado hajalilipa!.
Ikumbukwe ujio wa tamasha hilo uliambatana na kaulimbiu ‘Swahili Nation’ ambayo Kings Music, lebo yake Alikiba na hasimu wake kimuziki, walidai wao ndio waanzilishi rasmi wa Swahili Nation.