Wacheza upatu wanavyopigwa na vijumbe WhatsAppWacheza upatu wanavyopigwa na vijumbe WhatsApp

Dar es Salaam. Miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la watu wanaopoteza fedha kupitia makundi sogozi wa WhatsAp’ yanayoundwa kwa ajili ya kucheza upatu.

Makundi hayo huanza kwa mtindo wa kuaminiana, ambapo wanachama huchangia fedha wanazokubaliana kila siku, wiki au mwezi; ambapo mtu mmoja mmoja huchangiwa kwa kila mzunguko.

Hata hivyo, muda unavyosonga, migogoro huanza kujitokeza baada ya baadhi ya wahusika kushindwa kuwachangia wanachama wengine, hasa baada ya wao kupokea fedha kwenye mizunguko ya mwanzo.

Upatu huo wa aina hii hufanywa kwa makundi yoye; kipato cha chini, kati n ahata cha juu kulingana na shughuli zao.

Kwa mazingira kwa uswahilini huanzia kiwango kidogo cha Sh1, 000 ambapo mchangiaji hutakiwa kutoa Sh1,200 zikiwezo Sh200 gharama za kijumbe (mkusanyaji, ambaye mara nyingi anakuwa mwanzishaji).

Mbali na hao wa kiwango kidogo, wapo ambao wanalipishana hadi Sh5 milioni na wao hujikuta katika kadhia hiyo ya kutapeliwa.

Kauli ya wachangiaji

Akizungumza na Mwananchi, mama lishe wa Buguruni, Dar es Salaam, Swaumu Mkoloni amesema amekuwa akishiriki katika michezo ya mtandaoni kwa kutoa kila siku Sh2,200.

“Nimeshiriki michezo saba hadi sasa, miwili nilitapeliwa mitano nimemaliza vizuri, hiyo niliyodhulumiwa kuna watu waliishia njiani kwa kisingizio kuwa mambo yao yamekuwa mabaya,” amesema Swaumu.

Katika watu 50 alitarajia kupata Sh200, 000 kila baada ya siku mbili, lakini hakuambulia chochote na kujikuta anakata tamaa baada ya malengo ya fedha hizo kutokutimia.

Upatu huo uliharibika baada ya ndugu wa kijumbe kupewa fedha na kushindwa kulipia majina mengine, na hata mdhamini wake alipoambiwa, aliishia kusema atalifanyia kazi lakini hawakulipwa.

“Nilikosa sehemu ya kushikia kwa sababu mchezo huo niliwekwa na mfanyabiashara mwenzangu, hivyo sikuwa na wasiwasi na alisema anafahamiana na hao watu kwa hiyo niliwaamini,” amesema.

Jambo lingine amesema asilimia kubwa ya vijumbe huweka majina yao yakiwa kwanza ili wapate fedha kwanza. Wanapoombwa kwenye mzunguko unaofuata ili wengine watangulie, hudai kuwa tayari kuna watu wamekwishaomba.

Amesema mfumo huo unakuwa mgumu, pale baadhi ya majina yaliyopo yanaposhindwa kulipiwa kwa wakati, ndipo migogoro huanza na hatimaye mzunguko kuvunjika.

Mfanyabiashara wa vifaa vya magari Machinga Complex, Sixtus Titus amesema amewahi kuingia katika upatu wa kuchangiana Sh2 milioni kila mwezi ukiwa wa watu 20 akiwa na malengo yake, lakini katika watu hao waliokuwa wanatoa fedha ni watu 12 na majina mengine yalikuwa hewa.

“Yule dada Mungu ataendelea kumuonyesha namna alivyokula majasho ya watu, maana tulikuwa tunajinyima kumpa pesa kumbe alikuwa anatuiba na tulishituka baada ya kufika jina halisi na mwenzetu kutopewa pesa yake kamili, akapokea Sh22 milioni badala ya Sh38 milioni,” amesema Titus.

Amesema baada ya malalamiko hayo waligundua majina ya awali yote yalikuwa ya kijumbe na hakuwa na uwezo wa kuyalipia yote manane yaliyokuwa yamechangiwa Sh16 milioni.

Titus amesema kuingia kwenye huo upatu aliunganishwa na rafiki wa binamu yake aliyetambulishwa ni mfanyabiashara wa nguo Kariakoo na alimweleza amekuwa kwenye huo mchezo kwa zaidi ya miaka miwili na amefanikiwa kuagizia mizigo kutoka China.

Maelezo hayo, amesema yalimpa hamasa ya kuingia huko kwa sababu ya uwepo wa kijana huyo ambaye hadi sasa hapatikani kwenye simu pamoja na kijumbe wao.

“Baada ya kupigwa hizo pesa tulimzonga huyo dada ili atulipe pesa zetu hatutaki kuendelea na alisema atatulipa kwa kuwa kipindi hicho hakuwa na pesa na hii ilikuwa mwaka 2024.

Amesema pesa hizo zilikuwa zinatumwa katika laini tatu tofauti kwa kugawanywa mafungu kwa madai kuwa zikiwa nyingi katika laini moja ni vigumu kuzituma kwa mpokeaji.

Amesema wameshindwa kwenda polisi kwa sababu hawakujua jina halisi la muhusika na watu wamekuwa wakiwaeleza hawatapata haki kwa kuwa hakuna mahali waliandikishiana, hivyo wamemwachia Mungu.

Mkakati wa Takukuru

Kutokana na kukithiri kwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Songwe kupitia Mkuu wake, Frida Wikesi ametangaza mkakati maalumu wa kudhibiti utapeli na wizi wa kidijiti unaofanyika kupitia vikundi vya mitandao ya kijamii (WhatsApp) katika mji wa Tunduma, wilaya ya Momba mkoani Songwe.

Hatua hiyo inalenga kulinda fedha za wananchi pamoja na kukomesha utitiri wa vikundi vya kifedha visivyo rasmi vinavyotuhumiwa kuendesha mifumo haramu ya ukusanyaji fedha kinyume cha sheria za nchi.

Wikesi amesema taasisi imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi waliodhulumiwa kupitia vikundi vya mitandao ya kijamii vinavyojulikana kama vya kusaidiana kimaisha au kufa na kuzikana.

Amesema baadhi ya vikundi hivyo hukusanya fedha kutoka kwa wanachama lakini baadaye hugeuka chanzo cha migogoro, udanganyifu na dhuluma kwa wananchi waliowekeza fedha zao.

Sheria inasemaje

Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 inahusika moja kwa moja na makosa yanayofanyika kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano kama simu na mitandao ya kijamii.

Sheria hii inakataza mtu kutumia mtandao kwa lengo la kudanganya, kuiba au kuwalaghai wengine fedha au taarifa zao.

Kwa mujibu wa sheria hii, mtu anayefungua au kuendesha kikundi cha mtandao kwa nia ya kuwatapeli wanachama anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo au faini kulingana na uzito wa kosa.

Kwa mujibu wa sheria hizi zote kwa pamoja, mtu yeyote anayebainika kuendesha, kupanga au kushiriki katika mpango wa udanganyifu kupitia makundi haya anaweza kufikishwa mahakamani.

Endapo atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa adhabu ya kifungo, faini au zote kwa pamoja, pamoja na kulazimishwa kurejesha fedha za waathirika waliopoteza mali zao kutokana na udanganyifu huo.

Licha ya kuwepo sharia hiyo, Mtaalamu wa masuala ya fedha, Sophia Mussa amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakifanya makosa ya kuwaamini watu binafsi kuwahifadhia fedha kupitia makundi ya WhatsApp, badala ya kutumia benki na taasisi rasmi za kifedha zinazotambulika kisheria.

“Tatizo kubwa ni watu kuamini urafiki au maelewano ya kawaida kuliko mifumo rasmi ya fedha, hapo ndipo migogoro na wizi huanza pale pesa zinapopotea,” amesema Sophia.

Amesema hali hiyo inatokana na baadhi ya watu kuona mifumo ya upatu ni rahisi na yenye kutoa fedha kwa haraka, jambo ambalo limewafanya wengi kuingia kwenye hasara kubwa baada ya vijumbe kutoweka na pesa zao.

Sohia amesema taasisi rasmi za kifedha zina sheria, usimamizi na ulinzi wa fedha za wananchi na mifumo ya ufuatiliaji miamala na uwajibikaji tofauti na makundi hayo ambayo hayana uwazi wala usajili rasmi ambayo yanaendeshwa kwa mazoea na kuaminiana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *