Wataalamu wataja utafiti, ushirikishwaji wa jamii kukuza uchumi wa buluuWataalamu wataja utafiti, ushirikishwaji wa jamii kukuza uchumi wa buluu

Unguja. Licha ya sekta ya uchumi wa buluu kuwa na fursa nyingi, ili ziweze kufikiwa, imeelezwa kuwa lazima kuwepo na tafiti, ushirikishwaji wa jamii na sekta binafsi.

Pia, kunahitajika miundo ya kitaasisi kuhakikisha inakuwa imara, endelevu pamoja na kufanya mapitio ya sheria na sera ili ziakisi namna ya kutatua changamoto zinazoikumba.

Hayo yamebainishwa Mei 26, 2026 wakati wa maazimio ya warsha ya 29 ya watunga sera, watafiti na viongozi wa sekta binafsi kutoka nchi za Afrika iliyoandaliwa na Taasisi ya utafiti (Repoa) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu, Tume ya Taifa ya Mipango ya Tanzania na Benki ya CRDB.

Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari amesema katika warsha hiyo yameibuka mambo takribani manne ya utafiti, ushirikishwaji ambayo yametiliwa mkazo kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kukuza uchumi.

“Jambo lingine ambalo limeibuka ni ushirikishwaji kati ya sekta binafsi na taasisi za serikali na jumuiya za kimataifa, hivyo lazima zishirikiane katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika,” amesema Dk Mmari.

Amesema lingine lililojitokeza ni namna sekta ya uchumi wa buluu inaweza kupata fedha kuhakikisha sekta hii inapata fedha kutoka taasisi za kifedha kuhakikisha wajasiriamali wadogowadogo wanapata mikopo na dhamana na riba nafuu kutoka kwenye mabenki.

“Tumaona kwamba manufaa ya sekta yanakwenda moja kwa moja kuwanufaisha wanaohusika ikiwa ni pamoja na wavuvi, wakulima wa mwani na bidhaa mbalimbali zinazotokana na uchumi wa buluu,” amesema.

Amesema wamepata uzoefu kwamba nchi zilizofanikiwa katika uchumi wa buluu kama Namibia wametumia zaidi tafiti kutengeneaza sera na mipango yao ambayo inaakisi moja kwa moja na kutoa mapendekezo namna bora kuhakikisha uchumi wa buluu unakua.

Naye, Emmanuel Ringu ambao wanafuga samaki kwa njia ya vizimba Ziwa Victoria mkoani Mwanza, amesema wamesaidiwa kuazisha na kuzalisha samaki kwa vizimba hivyo kupitia Benki ya CRDB.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa ufugaji samaki wamefanikiwa kushirikisha namna walivyoanza na walipofikia katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji.

“Katika ufugaji samaki kuna tunahakikisha una mbegu bora, una mahali utaweka samaki, kwa hiyo tunashukuru CRDB kupata mtaji mkubwa ambao umetuwezesha kufuga vizimba 120 vinaendelea na uzalishaji,” amesema.

Amesema mpaka sasa wanaendelea na uzalishaji na kwamba soko lipo tena kubwa kwa hiyo akahamasisha watu wengine waingie kwenye sekta hiyo kwani inalipa na kuleta tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *