
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imedhamiria kuwawezesha viongozi wa sekta ya elimu, kuwa na maarifa ya uongozi yanayoendana na muundo wa sasa wa elimu nchini.
Katika kutimiza dhamira hiyo, imezindua Mpango wa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu, utakaowalenga wakuu wa shule za sekondari, wakuu wasaidizi pamoja na Maofisa Elimu Kata kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Mei 28, 2026 na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, wakati wa uzinduzi wa mpango huo.
Amesema mpango huo unalenga kujenga viongozi bora wa elimu wenye uwezo wa kusimamia kwa ufanisi ufundishaji, ujifunzaji na maendeleo ya shule nchini.
Profesa Nombo, amesema shabaha ya Serikali ni kuhakikisha mpango huo unawawezesha viongozi wa shule kupata maarifa ya kisasa ya uongozi, usimamizi wa taasisi za elimu na utawala bora.
Amesema Serikali imeamua kuanzisha mpango huo baada ya kubaini kuwa kwa muda mrefu wakuu wa shule za sekondari wamekuwa hawapati mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya elimu.
Katibu Mkuu huyo, ameeleza tofauti na walimu wakuu wa shule za msingi ambao wanapata mafunzo hayo mara kwa mara, wakuu wa shule za sekondari wamekuwa wakikosa fursa hiyo kwa muda mrefu hali iliyosababisha umuhimu wa kuwaandalia mpango maalumu wa kuwajengea uwezo.
“Mpango huu ni fursa muhimu kwa viongozi wa elimu kupata maarifa na mbinu mpya zitakazowawezesha kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pamoja na kuboresha matokeo ya wanafunzi,” amesema Profesa Nombo.
Amesema kupitia mafunzo hayo viongozi wa shule watajengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, uongozi wa taasisi za elimu, usimamizi wa rasilimali na namna ya kujenga mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Profesa Nombo amesema ndani ya miaka mitano 2025/30, jumla ya viongozi wa elimu 16,000 wanatarajiwa kufikiwa kupitia mpango huo, wakiwemo wakuu wa shule na wasaidizi 12,000 na Maofisa Elimu Kata 4,000.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dk Maulid Maulid amesema mafunzo hayo yatawasaidia viongozi wa shule kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shule na kuchangia kuboresha ubora wa elimu nchini.
