RC Manyara aagiza maboresho ya WASH kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi woteRC Manyara aagiza maboresho ya WASH kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote

Hanang. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ametoa wito kwa halmashauri na wadau wa maendeleo kuimarisha mifumo ya maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH) ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote, hususan katika shule, vituo vya afya na maeneo ya umma.

Sendiga alitoa wito huo jana Mei 27,2026 katika hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya mradi wa WASH wilayani Hanang, ambapo aliipongeza na kuishukuru Shirika la WaterAid Tanzania kwa kusaidia utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, vyoo bora na maeneo ya kunawia mikono katika Shule ya Msingi Gidamula.

Alisema ushirikiano huo umeonesha mfano bora wa utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji na mazingira salama.

Alisema upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na miundombinu bora ya vyoo ni msingi muhimu wa kulinda afya ya jamii, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kikubwa katika sekta hiyo.

“Tunahitaji maji safi na salama katika kaya, shule, vituo vya afya na maeneo ya umma ili kulinda afya za wananchi wetu,” alisema Sendiga.

Akitaja hali ya Mkoa wa Manyara, alisema kuwa asilimia 66 ya kaya zina vyoo bora huku asilimia 5.4 hazina kabisa, hali aliyoitaja kuwa bado inahitaji juhudi za pamoja za Serikali na wadau ili kuhakikisha kila kaya inapata choo bora na salama.

Kwa upande wa Wilaya ya Hanang, alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 83 ya kaya zinatumia vyoo bora, lakini akasisitiza umuhimu wa kuweka mikakati ya muda mfupi, kati na mrefu ili kufikia asilimia 100.

Katika sekta ya elimu, Sendiga alisema changamoto za miundombinu ya WASH bado ni kubwa, ambapo ni asilimia 30 tu ya shule za msingi zilizo na miundombinu ya hedhi salama, huku asilimia 52 ya wanafunzi wakipata elimu na taulo za kike.

Aliongeza kuwa baadhi ya shule bado hazina maji ya uhakika, licha ya kuwa asilimia 95 ya vyoo vya shule za msingi vipo, akibainisha kuwa changamoto kubwa ni uwiano wa wanafunzi na vyoo pamoja na ukosefu wa miundombinu rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu.

Sendiga alisema usafi wa hedhi ni haki ya msingi inayopaswa kuzingatiwa katika kila shule.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali imejenga miundombinu ya maji, vyoo na unawaji mikono katika zaidi ya shule 500 mkoani Manyara, na kwamba lengo ni kuhakikisha shule zote zinapata huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 100 ifikapo Desemba 2026.

Aidha, alisema kuwa karibu asilimia 90 ya vituo vya afya katika Wilaya ya Hanang vimeunganishwa na huduma za maji, huku akisisitiza haja ya kuboresha uwezo wa uhifadhi wa maji katika vituo vilivyosalia.

Katika maeneo ya umma kama masoko, vituo vya mabasi na minada, alisema bado kuna changamoto ya miundombinu ya vyoo na unawaji mikono, na kuagiza halmashauri kutenga bajeti maalumu kwa maboresho hayo.

Alihitimisha kwa kuwataka wananchi na taasisi kuhifadhi na kutunza miradi hiyo kwa kufanya matengenezo madogo mara kwa mara ili kuhakikisha uendelevu wake.

Mkurugenzi wa Nchi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga  alisema WaterAid imekabidhi mradi wa maji, wenye thamani ya Sh648.8 milioni kwa jamii ya eneo hilo.

Alisema mradi huo una vipengele tisa vilivyounganishwa vinavyolenga kubadili maisha ya zaidi ya wakazi 2,440 wa Kijiji cha Gidamula kwa muda mrefu.

Alisema miongoni mwa yaliyojumuishwa kwenye mradi huo ni vyumba maalumu vya kubadilishia taulo za kike na maeneo salama ya kutupia taka za hedhi, hatua inayolenga kuongeza heshima, usiri na usafi kwa wanafunzi wa kike.

“Vifaa hivi sio tu miundombinu ya matofali na saruji, bali ni ishara ya heshima na utu kwa wasichana shuleni,” alisema.

Alisema, “Uwekezaji huu ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kujifunza katika mazingira salama, yenye heshima na yanayozingatia afya.”

Pia alisema mradi umejumuisha  mfumo wa maji unaostahimili mabadiliko ya tabianchi wenye tanki la chini ya ardhi, pampu za nishati ya jua na miundombinu ya kuvuna maji ya mvua iliyoundwa kudumu kwa angalau miaka 15.

Aidha, mradi huo umejumuisha ujenzi wa vyoo 17 vinavyozingatia jinsia na ujumuishi kwa wanafunzi na walimu, pamoja na vifaa vya kunawa mikono ili kudhibiti maambukizi ya magonjwa shuleni hapo.

Aliongeza kuwa mradi pia umehamasisha uboreshaji wa vyoo vya nyumbani ambapo familia 20 tayari zimeboresha miundombinu ya usafi, huku zaidi ya wakazi 2,004 wakifikiwa kupitia elimu ya usafi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *