Dar es Salaam. Wakati sekta ya huduma za usafiri kwa njia ya mtandao zikiendelea kukua, wadau wametaka kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji, usalama wa huduma, ustawi wa madereva pamoja na matumizi ya teknolojia rafiki kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
Hoja hizo zimeibuliwa leo Alhamisi, Mei 28, 2026 jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa Bolt Tanzania Mobility Dialogue 2026 uliofanyika kupitia Mwananchi Jukwaa la Fikra, uliobebwa na mada:“Uendelevu, Uaminifu na Ukuaji Barani Afrika.”
Akizungumza katika mkutano huo, Mchambuzi wa Sera wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Lois Kassana amesema wawekezaji wengi hukosa uhakika sera na sheria zinapobadilishwa bila ushirikishwaji wa kutosha wa wadau.
Amesema mazingira yasiyotabirika ya sera yanaweza kuathiri uaamuzi wa uwekezaji, hasa kwa wawekezaji wanaowekeza kwa mtazamo wa muda mrefu katika sekta mbalimbali za uchumi kwa kuwa, mara zote wanahitaji mazingira yenye utulivu na uhakika wa kisheria ili wapange biashara zao kwa muda mrefu bila hofu ya mabadiliko ya ghafla ya sheria au kanuni.
Mkurugenzi wa Kamouni ya Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole akizungumza katika mdahalo wa Jukwaa la Fikra ulioandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications,jijini Dar es Salaam. Picha na Said Powa
Kassana amesema ni muhimu kwa wadau mbalimbali, wakiwamo wataalamu na washauri wa sera kuendelea kuishauri Serikali kuhusu umuhimu wa kufanya mazungumzo na wadau kabla ya kufanya mabadiliko makubwa ya sera au sheria.
Maneno yake yaliungwa mkono na Mkurugenzi wa Bolt Afrika Mashariki, Demetrius Kanyankole akisema ukuaji wa sekta hiyo unahitaji uwekezaji mkubwa pamoja na mazingira yenye uhakika kwa wawekezaji.
Amesema kampuni nyingi huendesha shughuli zake kwa kuzingatia mwenendo wa soko, mahitaji ya wananchi pamoja na uwezo wa kuhakikisha huduma zinapatikana kwa uhakika.
“Biashara hii inahitaji uwiano kati ya mahitaji ya abiria na upatikanaji wa madereva. Ili huduma iwe bora lazima kuwe na uwekezaji mkubwa katika teknolojia, huduma kwa wateja na mifumo ya uendeshaji,” amesema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole akizungumza katika mdahalo wa kujadili huduma za usafiri kwa njia ya Tax mtandao. ulioandaliwa kupitia Mwananchi Jukwaa la Fikra lililofanyika jijini Dar es salaam. Wengine ni Lois Kassana Mchambuzi wa Sera kutoka TPSF (kushoto), Jumanne Mtambalike kutoka kampuni ya Sahara Ventures (wa pili kushoto) na Abdallah Mhagama Mkurugenzi wa Uchumi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Aridhini (LATRA). Picha na Said Powa
Amesema kampuni nyingi huendesha shughuli zake kwa kuzingatia taarifa za soko, uchambuzi wa mahitaji pamoja na mwenendo wa sekta kwa jumla.
Jambo hilo huzifanya kampuni za teknolojia kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kila mwezi katika mifumo ya uendeshaji, matangazo, teknolojia pamoja na huduma kwa wateja ili kuhakikisha huduma zinaendelea kuwa thabiti na za kuaminika.
Hiyo ni kwa sababu biashara ya majukwaa ya kidijitali, mafanikio hutegemea zaidi uwezo wa kuweka uwiano mzuri kati ya mahitaji ya wateja na upatikanaji wa huduma kutoka kwa madereva au watoa huduma wengine.
“Leo tunapozungumzia biashara hii, tunazungumzia suala la uwiano kati ya mahitaji na huduma zinazotolewa. Ili kupata matokeo mazuri, ni lazima kuwe na uwekezaji wa kuhakikisha huduma zinapatikana kwa uhakika na kwa ubora unaotakiwa,” amesema.
Amesema hayo wakati takwimu zinaonesha kuwa, madereva wa Bolt wanaotumia gari wana uhakika wa kuingiza hadi Sh1.1 milioni kwa mwezi huku wanaoendesha bajaji wakiwa na uhakika wa kuingiza hadi Sh1.06 milioni.
Kwa upande wa madereva pikipiki maarufu bodaboda wanao uwezo wa kuingiza hadi Sh913,000 kwa mwezi wakifanya kazi zao kikamilifu.
Amesema tangu Bolt iingie Tanzania mwaka 2017 zaidi ya madereva 30,000 kutoka miji minane wamekuwa wakitumia jukwaa hilo kama sehemu ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha.
“Madereva 500 wanaofanya vizuri hupata zaidi ya Sh3.5 milioni kwa mwezi. Asilimia 70 ya madereva hupata mapato yanayozidi wastani wa mshahara nchini Tanzania,” amesema.
Mbali na yanayopaswa kufanyika, Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Venture, Jumanne Mtambalike amesema kwa sababu sasa teknolojia ni nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi, uzalishaji na ushirikishwaji wa wananchi katika uchumi ni vyema kuwapo na mfumo wa ‘sandbox’ katika kukuza ubunifu na uwekezaji nchini.
Amesema mfumo huo unaweza kuwa nyenzo muhimu kwa Serikali na wadau wa sekta binafsi kupima teknolojia, huduma na mawazo mapya katika mazingira salama kabla ya kuanzishwa rasmi sokoni.
“Mfumo wa sandbox unatoa nafasi ya kutathmini faida, changamoto na hatari zinazoweza kujitokeza kabla ya kutungwa kwa sera au sheria za kudumu,” amesema.
Ili hili lifanikiwe amesema ni lazima kuwapo na sera bora kuzingatia ushahidi halisi na uzoefu wa vitendo.
“Badala ya kutegemea tafiti pekee, Serikali inaweza kujifunza kupitia majaribio ya moja kwa moja pamoja na kuangalia namna mataifa mengine yanavyosimamia ubunifu na teknolojia mpya,” amesema.
Kichocheo cha maendeleo
Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa njia ya Barabara Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana amesema usafiri kwa njia ya mtandao ni kichocheo cha maendeleo endelevu na muhimu hasa wakati huu ambao idadi ya watu maeneo ya mijini wanaongezeka.
“Tanzania inashuhudia ongezeko kubwa la watu wanaohamia mjini jambo linalofanya mahitaji ya haraka na salama kuongezeka mara dufu jambo linalohitaji kujenga majukwaa yanayodumu ili kuhimili ongezeko hili,” amesema.
Amesema hali hiyo inafanya usafiri wa kidijitali kuwa si anasa tena, bali ni hitaji la msingi la kiuchumi kwa kuwa katika miji mikubwa barani Afrika usafiri huu umesaidia kurahisisha upatikanaji wa bima na huduma za kifedha.
“Usafiri huu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo endelevu miongoni mwake ni kazi zenye staha, kuna lengo linazungumzia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, wazungumzaji waliongelea magari ya umeme lakini sisi Tanzania tumeanza na matumizi ya gesi asilia,” amesema.
Amesema utafiti unaonesha kuwa karibu asilimia 70 ya bajaji za kukodi zinatumia gesi asilia huku magari madogo yakiwa takribani asilimia 40.
Ilichokisema Latra
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Uchumi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Abdallah Mhagama amesema kuongezeka kwa majukwaa ya usafiri wa kidijitali kumesaidia kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo, hasa katika utambuzi wa madereva, ufuatiliaji wa usalama na udhibiti wa huduma.
Amesema huduma za usafiri mtandaoni zimekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa madereva wengi nchini, huku sekta hiyo ikibadilika kutoka kazi ya ziada na kuwa chanzo kikuu cha maisha kwa watu wengi.
“Nchini Tanzania, usafiri wa mtandaoni si kazi ya ziada tu, kwa wengi imekuwa chanzo kikuu cha kipato,” amesema.
Pia, amesema jukumu kuu la Latra ni kulinda masilahi ya watumiaji na kuhakikisha uwepo wa bei elekezi katika soko linaloendelea kukua kwa kasi.
MCL yanena
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Kadambara Maita amesema sekta ya usafiri wa kidijitali imeendelea kukua kwa kasi na kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya wananchi wengi, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.
Amesema kupitia teknolojia, wananchi wanapata huduma za usafiri kwa urahisi zaidi, vijana wanapata ajira na fursa za kipato, biashara zinaunganishwa kwa ufanisi huku shughuli za kiuchumi zikiendelea kwa kasi zaidi.
