Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi kurejesha imani yake kwa wananchi, sekta binafsi na jumuiya za kimataifa zilizopo hapa nchini.
Mkuu huyo wa nchi, ameeleza hayo huku akirejea matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Afro Barometer uliohusisha baadhi ya wananchi wa Afrika juu ya imani yao kwa majeshi ya polisi katika mataifa husika.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 28, 2026 wakati akifunga mafunzo ya kozi ya maofisa na wakaguzi wasaidizi wa Polisi, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, Dar es Salaam.
“Hapa tunazungumzia uhalali wa Jeshi la Polisi kukubalika kwake, nilikuwa naangalia clip moja inazungumza kukubalika kwa majeshi ya polisi ya nchi mbalimbali Afrika na walitoa asilimia za kukubalika kwao,” amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi, wananchi pamoja na Maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi kabla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, kozi namba 1 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mei 28, 2026.
“Nchi iliyofanya vizuri zaidi ina asilimia 25 ya kukubalika kwake na maswali yalikuwa kama unapata shida imani yako ni kiasi gani kukimbilia polisi ili ukasaidiwe,” amesema Rais Samia.
Amefafanua nchi iliyofanya vizuri zaidi katika utafiti huo, jawabu lilikuwa asilimia 25, huku Tanzania ikipata asilimia 12 ya wananchi ambao wakipata shida watakimbilia kituo cha polisi kupata msaada.
“Wengine hatujui wanakwenda wapi? Hizi ni taarifa ambazo hatuwezi kuzibeza IGP (Camillius Wambura). Ni taarifa ambazo tuangalie pengo liko wapi, kwa nini wananchi wanajibu hivyo, turekebishe,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema ni wakati mwafaka kwa Jeshi la Polisi kuwashirikisha wananchi kupitia polisi jamii ili wawe sehemu ya kusimamia usalama wao huku wakiamiani jeshi hilo ndilo kimbilio lao kwa shida zao.
Mkuu huyo wa nchi, amesema ni kutokana na hayo na mengine mwaka 2023 aliunda Tume ya kuangalia mifumo ya haki jinai ambayo ilikuja na mapendekezo mbalimbali kwa jeshi hilo.
Miongoni mwa mapendekezo ya tume hiyo ni mageuzi ya mfumo na muundo wa jeshi hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Polisi kabla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi hilo, Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mei 28, 2026.
Mapendekezo ya mageuzi hayo kwa mujibu wa tume hiyo, yalitokana na kubaini jeshi hilo linatumia nguvu kupita kiasi, linakamata bila kufuata sheria, udhaifu wa upelelezi na utunzaji duni wa vielelezo.
Hata hivyo, baadhi ya mageuzi ikiwemo mabadiliko ya jina na muundo wa Jeshi la Polisi bado hayajatekelezwa kikamilifu, huku mageuzi yakiendelea kujadiliwa.
Jambo lingine, Rais Samia amesema anangependa kuona matokeo ndani ya Jeshi la Polisi ukiwemo uwezo wa kutambua mapema iwezekanavyo viasharia vya hatari vya usalama kwa nchi.
“Mfano tulikuwa tunapokea ripoti ya matukio ya Oktoba 29, 2025, walisema labda uzoefu, mila na desturi zetu kwamba Tanzania ni nchi ya amani, nchi ya usalama na kwamba vikitokea vitisho hatuvipi uzito wake, tunasema aah watatukuta asubuhi tunapiga mswaki, kwa hiyo wakija sisi tupo bwana,” amesema na kuongeza.
“Yaliyotokea yametupa funzo, tulijaribiwa na kwa dhati nishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, majaribio yale waliweza kuyaondoa ndani ya muda mfupi sana,”ameezeleza.
Msisitizo wa Rais Samia, ni kuona Jeshi la Polisi lisilodharau taarifa yeyote, kiashiria chochote cha hatari kinafanyiwa kazi kwa haraka.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa kwenye uwanja wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mei 28, 2026.
Amebainisha kuwa hayo yote, yatafanikiwa endapo Jeshi la Polisi likiwa na mawasiliano ya karibu na vyombo vingne vya usalama katika kubadilishana taarifa za viashiria vya hatari.
“Wito wangu kwa Jeshi la Polisi ni kujenga imani kwa jamii ili kutimiza dhamira aliyoisema IGP Wambura kuwa, Jeshi la Polisi lina dhamira ya kuhakikisha linakuwa karibu na wananchi katika kubaini na kuzuia uhalifu kabla ya kutokea,”
Katika hatua nyingine, Rais ameeleza kufurahishwa kwake na kauli ya IGP Wambura, kuhusu maboresho ya mfumo, muundo na sheria ya Jeshi la Polisi, kama ilivyopendekezwa na Tume ya Haki Jinai.
Kwa mujibu wa Rais Samia, maboresho hayo yamegusa matumizi ya Tehema na kuimarisha mfumo wa polisi jamii na kuendesha mafunzo na kujenga nidhamu ya utendaji wa jeshi hilo.
Hatua hizo, Rais Samia amesema lazima ziendelee kupimwa kupitia matokeo na si kuahidi kuchukua hatua, bali matokeo lazima yaonekane kwa namna jeshi hilo linavyotumia rasilimali zinazotolewa kuimarisha masuala ya ulinzi wa raia na mali zao, yaani kujenga uwezo wa utendaji ikiwemo mafunzo.
“Tumezoea huko nyuma tukiona askari wakisimamisha magari na kufanya mambo ambayo hayakubaliki, sasa hizo ndio nyanja za medani mwende kurekebisha hayo, yale tunayoyaona video zinazorushwa rushwa yasirushwe, askari wetu msimame kwenye mambo yenu,” amesema.
Aidha, Rais Samia amewataka wahitimu wa kozi hizo kuendelea kuijenga taswira njema ya Jeshi la Polisi pindi watakaporejea katika vituo vya kazi, huku wakitambua wameongezewa dhamana ya uongozi ndani ya jeshi hilo.
“Uongozi huo hatutaupima kwa urembo wa mabegani (vyeo) hapana, bali kwa nidhamu, uadilifu, weledi na uwezo wa kusimamia matokeo na kudhihilisha matokeo sahihi ya ulinzi wa raia na mali zao,” amesema Rais Samia.
Uwezeshajiwa Polisi
Awali, IGP Wambura ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu, vitendeakazi na bajeti.
Amesema Serikali ya Rais Samia imeonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha utendaji wa jeshi hilo kwa kutatua changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikilikabili.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura akiwa katika hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi iliyofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam.
“Kwa upande wa majengo tumetekeleza jumla ya miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo 320, tumekamilisha majengo 174 na tunaendelea na miradi mingine 146 ambayo ipo katika hatua mbalimbali,” amesema.
IGP Wambura amesema Jeshi la Polisi halitavumilia ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu za kazi ndani ya jeshi hilo na kwamba askari wachache watakaokiuka misingi ya jeshi hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu haraka bila upendeleo wala uonevu.
“Kwa wachache watakaokengeuka hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa kwa haraka bila upendeleo, uonevu wala muhari,” amesema IGP Wambura.
Kustaafu majukumu
Akimkaribisha Rais Samia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobasi Katambi amesema viapo vya askari wa Jeshi la Polisi havina ukomo, hivyo hata wakistaafu wanatakiwa kuishi navyo na si kwenda kinyume na kiapo walichokiapa.
“Mheshimiwa Rais (Samia) tukuahidi tutaendelea kusimamia suala la kiapo, lakini pia iwe ahadi yetu ya utii katika kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na tukaendelee kuishi katika viapo.
“Tumeapa kwa Mungu, tumeapa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tumeapa kwa mamlaka ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Mheshimiwa Rais kiapo cha askari hakina ukomo, hata pale utakapostaafu, na kutoka nje ya majukumu viapo bado vipo hai,” amesema Katambi.
Katambi amesisitiza askari polisi akistaafu huwa anastaafu majukumu tu na sio viapo, hivyo amekumbusha kuzingatia suala ambalo ni jukumu la msingi kwao.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa nidhamu na wale watakaokwenda kinyume na maadili watachukuliwa hatua na vitakuwa na utii kwa amiri jeshi mkuu.
Mbali na hilo, Waziri Katambi amesema watahakikisha wakati wote vyombo vya ulinzi na usalama vinatenda haki, bila upendeleo wala kumuonea mtu.
