
Sisi Watanzania tuna utamaduni wa kuchangiana kwenye sherehe au misiba, hivyo ili Tanzania tupate maendeleo ya kweli na endelevu, ni lazima Watanzania tubadilike sio tusichangie sherehe au misiba, bali tubadilike na kuanza kuchangia pia afya, elimu na kuchangiana mitaji.
Kuna msemo wa Kiswahili usemao “chanda chema huvikwa pete” na “mcheza kwao hutunzwa”. Hii ni makala ya kuwahimiza Watanzania, tuichangie Hospitali ya Benjamin William Mkapa (BMH) iliyopo Dodoma.
Kwa jinsi hospitali hii ilivyo, ni mkombozi kwa baadhi ya magonjwa, sio tu ni hospitali mkombozi mkuu wa upandikizaji figo na upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa selimundu, bali Tanzania ndio nchi pekee kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kupandikisa uloto.
Hospitali hii kwa hapa nchini ndiyo hospitali pekee inayotoa huduma hii hapa nchini, hivyo sio tu ni hospitali tegemewa Tanzania, bali ni fursa kwa nchi yetu kuwa kitovu cha utalii wa kimatibabu, badala ya wagonjwa wa bara la Afrika kufurika nchini India kupata tiba za kibingwa, wafurike Tanzania kupata huduma hizo na sio tu kuwatibu watu bali kuinui pato la taifa.
Mimi ni mwathirika wa ajali mbaya ya pikipiki, mjini Dodoma, nikapata tatizo linalojulikana kitaalamu kama brachial plexus injury, kukatika mawasiliano kati ya ubongo na mkono, nikawahishwa hospitali ya Dodoma, flying doctors wakanihamishia Hospitali ya Mifupa (Moi), nikapelekwa Hospital ya Mill Park nchini Afrika Kusini, hatimaye nikaenda kuponea India.
Huko kote, vifaa vya vya Moi na vile vya India, vifaa vyetu ni bora zaidi, tatizo letu lilikuwa ni ubingwa wa kufanya operesheni za ubongo, lakini sasa Tanzania tumepiga hatua kubwa, sio tu kustahili pongezi, bali, juhudi hizo ziungwe mkono kwa Watanzania wote, tuchangishane, kuwaokoa wenzetu kwa sababu huduma za kibingwa ni gharama kwa Mtanzania wa kawaida.
Tofauti kati ya Tanzania na huko kote nilikopita kutibiwa, Tanzania mgonjwa anapokelewa hospitalini kama mgonjwa, mtu wa kuhurumiwa na kusaidiwa, kwa wenzetu mgonjwa anapokelewa kama mteja ni mfalme, watu wanakimbizana!
Japo tatizo langu ni mkono, nilikuwa natembea mwenyewe, kufika india, unaletewa kiti, namweleza mhudumu naweza kutembea mwenyewe, anakugomea, wewe ni mgonjwa, sisi tuko hapa kwa ajili ya kukuhudumia, huna sababu ya kutembea, wakati mimi ndio kazi yangu, kaa tukupeleke.
Hospitali yetu ya BMH imefikia uwezo huo wa kubadilika na kuwa kitovu cha utalii wa kimatibabu mjini Dodoma ikiwa na mipango ya kuanzisha kijiji cha utalii wa kimatibabu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Mipango hiyo iko katika mkakati kabambe wa miaka 10 wa hospitali hiyo unaolenga kuimarisha huduma maalumu za afya, utafiti na mafunzo. Hospitali pia inaanzisha mfuko maalumu wa kusaidia upandikizaji wa uloto kwa watoto wanaougua ugonjwa wa seli mundu na huduma za upandikizaji wa figo kwa watu wenye uhitaji kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Mpango huo unalenga kukusanya Sh7 bilioni ndani ya miaka miwili huku Sh4 bilioni zikiwa tayari zimekusanywa. Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi alifichua mipango hiyo wiki hii alipokuwa akiwapa wahariri taarifa jijini Dar es Salaam kabla ya sherehe za miaka 10 ya hospitali hiyo zilizopangwa kufanyika Julai, mwaka huu.
Profesa Makubi alisema mafanikio ya hospitali katika muongo mmoja uliopita yameiweka katika nafasi ya kupanua utalii wa kimatibabu na kuvutia wagonjwa kutoka nchi jirani wanaotafuta matibabu maalumu.
Alisema BMH kwa sasa ina wafanyakazi 1,073 ikilinganishwa na wafanyakazi 20 pekee wakati hospitali hiyo ilipoanzishwa Oktoba 13, 2015. Alisema hospitali hiyo sasa inahudumia takribani watu milioni 10 kutoka mikoa minane kote nchini.
Aliongeza kuwa hospitali imeendelea kuvutia wagonjwa wa kimataifa kupitia huduma za utalii wa kimatibabu. “Chini ya utalii wa kimatibabu, tumewatibu wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, 526 kutoka Comoro na mgonjwa mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na wagonjwa wengine wa kigeni,” alisema.
Akielezea kwa undani kuhusu upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa seli mundu, Mkurugenzi Msaidizi na Mtaalamu wa Hematology, Dk Stella Mangae alisema upandikizaji uloto (Bone Marrow Transplant) ni utaratibu wa tiba ambapo uloto ulioharibika au kuugua hubadilishwa na kuwekwa uloto wenye afya kutoka kwa mchangiaji. Upandikizaji huu hutibu magonjwa ya Selimundu (Sickle Cell Anemia), kansa ya damu (Leukemia) na matatizo ya kinga ya mwili na magonjwa ya kurithi.
Alisema hadi sasa BMH imewatibu wagonjwa 30 ambapo 12 wamepona kikamilifu na kuendelea na maisha ya kawaida ikiwa ni pamoja na kurudi shuleni. Alisema wagonjwa wawili wamelazwa kwa sasa, akiwemo mmoja kutoka DRC.
Dk Mangae alikiri gharama kubwa ya upandikizaji wa uloto lakini akaipongeza serikali kwa kufidia gharama za matibabu zinazofikia milioni 75 kwa kila mgonjwa.
Ili kupunguza mzigo kwa wananchi, Serikali, wananchi na wadau mbalimbali wajitolee kushiriki harambee hii ya hospitali ya BMH kwa kuchangia chochote walichonacho kuanzia Sh1,000 na kuendelea. Kama Watanzania tuna utamaduni wa kuchangia sherehe kama harusi, lazima sasa tubadilike na kuchangia harambee za afya na elimu.
Jinsi ya kuchangia kwa watu wa kawaida, Michango itumwe kupitia: Namba ya Malipo (Control Number): 986930000001. Jina: BMH Organ Tanzania, kwa mitandao yote ya simu.
Kwa upande wa taasisi, michango itumwe akaunti namba: 102501000407, Benki Kuu ya Tanzania, Jina: BMH Organ Tanzania.
