UKISIKILIZA mtaani utasikia taarifa kwamba kiwango cha kiungo wa Simba Clatous Chama kinatokana na Mzambia huyo kutaka mkataba mpya, lakini sasa uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi umetoka hadharani na kueleza mkataba halisi wa fundi huyo.
Simba ilimsajili Chama dirisha la Januari 2026 akitokea Singida Black Stars, akirejea Msimbazi baada ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita 2024-2025.
Baada ya kutua tu kwa Wekundu hao, jamaa ameuwasha moto mkali, akiwa ni mmoja wa wachezaji wanaoibeba Simba hivi sasa katika harakati za kusaka mataji mawili yaliyobaki ambayo ni Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalum aliweka wazi kwamba taarifa kwamba kiwango cha Chama kinatokana na kiungo huyo kutaka mkataba mpya, hazina ukweli.
Magori amesema wakati Wekundu hao wakimsajili Chama kutoka Singida, alisaini mkataba unaofikia tamati mwaka 2027 na kwamba Simba haiwezi kusajili mchezaji kwa mkataba wa miezi sita.
“Chama ana mkataba mpaka 2027, watu wanasema uongo kwamba Chama mkataba wake unamalizika na kwamba eti anacheza vizuri kwasasabu anatafuta mkataba mpya, ukweli ni kwamba yupo hapa mpaka 2017,” amesema Magori kwenye mahojiano maalum na Mwanaspoti.
“Hicho kinachosemwa labda tumuongezee mpaka 2028 lakini Simba hatuwezi kusajili mchezaji kwa miezi sita, hicho kitu hakipo na hakiwezi kutokea, ukimsajili mchezaji kwa miezi sita maana yake siku unamsajili hapohapo unazipa klabu zingine nafasi ya kuzungumza naye, hayo ni makosa.
Aidha Magori ameongezakuwa, wakati Chama anaondoka Simba kwenda Yanga, alilazimika kufanya hivyo baada ya klabu hiyo kutoonyesha umakini wa kutaka kumbakisha akisema kiungo huyo hakuwa na mapenzi ya kwenda kucheza kwa wapinzani wao hao.
“Chama alienda Yanga ni kwasababu pia Simba hatukuonyesha umakini wa kumbakiza, hayakuwa mapenzi yake kwenda Yanga ingawa kule alipewa fedha nyingi na mkataba wa mwaka, zilikuwa nyingi sana.
“Alikuwa tayari kubaki Simba ila sisi wenyewe pia hatukuwa makini kama tungekuwa makini tungembakiza, lakini nafikiri kulikuwa na mambo ya muache aende, akaenda Yanga kwa shingo upande kwasababu mimi niliongea naye sana na kibaya zaidi hata familia yake haikuridhia yeye kwenda Yanga, kwahiyo na kule nako hakukubalika na ukiongea naye anakuambia sababu gani ya kutokubalika.
Nakumbuka nilivyoteuliwa Septemba mwaka jana kuwa mwenyekiti wa bodi alinitumia ujumbe kuwa sasa ana imani kwamba anarudi Simba baada ya hapo yaliyobaki ni historia.”
Magori akasimulia zaidi namna alivyomnasa kiungo huyo kwa mara ya kwanza wakati anatua Simba akitokea Lusaka Dynamo ya Zambia akisema ilibidi utumike umafia mkubwa kumpata Chama wakiwa wanatafuta kiungo mchezeshaji.
“Mwaka 2018 wakati tunatafuta kiungo mchezeshaji mimi ndiye niliyeenda kumchukua Zambia tukiwa tumehangaika sana kupata mchezaji wa aina yake, jamaa yangu mmoja ambaye ni wakala wa wachezaji kutoka Malawi naomba nisimtaje jina akanipigia simu kuniambia kuna mchezaji anaitwa Clatous Chama.
“Huyu ndio kiungo wa kiwango cha juu mchezeshaji yeye anamjua lakini yupo Lusaka Dynamo, hiyo Lusaka Dynamo inamilikiwa na mpwa wa Rais wa Zambia wakati huo na ana pesa nyingi, akaniambia hamtoweza kumtoa pale.
“Mimi nikampigia rafiki yangu mmoja wa Zambia nikamuomba namba ya Chama, nikaongea naye akaniambia anaweza kuondoka pale kwasababu hiyo klabu ilikuwa haijamlipa mishahara kwa miezi minne na ameshawakumbusha mara kadhaa, nikasema miezi minne wakati FIFA inasema miezi miwili unaweza kuondoka kama hujalipwa.
“Nikamwambia Chama sasa sikiliza tunafanya hivi, utaandika barua ya kuacha kazi Lusaka Dynamo lakini hutaipeleka wewe, nitakutumia tiketi ya ndege ukishapanda ndege mpe barua pacha wako (Adrian Chama) aipeleke wakati huo ukiwa angani wakikutafuta hawatakupata, akafanya hivyo.
“Alipofika hapa nchini tukamfanyia utaratibu akaenda Uturuki kuungana na timu ilipokuwa kwenye maandalizi ya msimu mimi nikaenda Zambia kufuatilia hati yake ya uhamisho, tukafanya nao kikao wale jamaa wakataka fedha nyingi sana wakidai kwamba walikuwa wanamdai Chama.
“Nikaachana nao nikarudi hapa, tukawaandikia FIFA tukawaeleza kila kitu, na unajua FIFA kama ukiomba hati ya uhamisho na zikapita siku 14 hamjatoa wanataka maelezo, wale wakasema wanamdai, sisi tukaeleza kwamba mchezaji amevunja mkataba kutokana na sababu hii sasa Fifa ikatoa kitu kinaitwa hati ya uhamisho wa dharura (provisional ITC) wakati wakitaka maelezo, baadaye kila kitu kilimalizika kwa Chama kushinda akaendelea kucheza Simba,” alibainisha Magori.
Tangu arejee Simba, Chama amefanikiwa kufunga mabao sita na asisti sita katika Ligi Kuu Bara msimu huu na kumfanya jumla kuwa nayo nane yakiwemo mawili aliyoyafunga akiwa Singida Black Stars.
Ubora wa Chama ni chachu ya mafanikio ya Simba katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
