KVZ ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), wana takribani siku 268 za kutetea ubingwa huo kufuatia Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), kutoa kalenda ya mashindano kwa msimu wa 2026-2027.
Katika kalenda hiyo, Ligi Kuu Zanzibar imepangwa kuanza Agosti 29, 2026 na kuhitimishwa Mei 18, 2027, ikichezwa kwa siku 263, sawa na wiki 37 na siku nne ambayo ni miezi minane na siku 21.
Kalenda hiyo imefafanua kuwa Ngao ya Jamii itachezwa Agosti 23, 2026 kati ya mabingwa wa FA, KMKM na wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ.
KMKM ilichukua ubingwa wa Ngao ya Jamii msimu uliopita chini ya Kocha Hababuu Ali ambaye baadaye aliachana na timu hiyo akaenda kushinda Ligi Kuu akiwa na KVZ.
Kwa mantiki hiyo, Ngao ya Jamii itakuwa ni vita kati ya Hababuu anayeinoa KVZ na KMKM.
Mbali na Ligi Kuu, kalenda hiyo inaonyesha michuano ya Mapinduzi 2027, itaanza kuchezwa Januari 1 hadi 14, huku Kombe la Muungano 2027, likichezwa Aprili 20 hadi 29.
Wakati huohuo, Kombe la FA, hatua ya awali itaanza kuchezwa Oktoba 22, 2026, fainali itapigwa Mei 22, 2027, huku vipindi viwili vya usajili kwa maana ya dirisha kubwa limefunguliwa Julai 20, 2026, litafungwa Septemba 5, 2026, huku lile dogo likitarajiwa kufunguliwa Desemba 15, 2026 hadi Januari 31, 2027.
Pia, kalenda hiyo imeonesha ligi hiyo itakwenda mapumziko kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza Februari 8, 2027 hadi Machi 15, 2027.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim Ali amesema mechi ya Ngao ya Jamii itakuwa ishara rasmi ya ufunguzi wa msimu wa 2026-2027.
Amesema, maandalizi ya mchezo huo yanaenda vizuri kwa kushirikiana na wadau kwani wamejipanga kuchezwa katika mazingira yenye usalama na kuvutia mashabiki.
Pia, aliwataka mashabiki wa timu zote na wapenda soka kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo huku wakidumisha amani na utulivu.
Wakati msimu mwingine ukitarajiwa kuanza, takwimu zilizotolewa msimu wa 2025-2026 jumla ya mabao 595 yalifungwa katika Ligi Kuu Zanzibar, asisiti 462, cleansheets 169, kadi za njano 655 na nyekundu 32.