Kumng’oa Fadlu kwa Waarabu ngoma ngumuKumng’oa Fadlu kwa Waarabu ngoma ngumu

SIKU chache baada Yanga kuhusishwa na aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids, imefichuka kuwa mabingwa hao wa Tanzania watalazimika kumwaga mkwanja mrefu ili kuipata saini ya raia huyo wa Afrika Kusini anayeifundisha Raja Casablanca.

Awali Yanga ilikuwa ikihusishwa na Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze ambao walikuwa wakiinoa Kaizer Chief ya Afrika Kusini kabla ya kuhamia kwa Fadlu ambaye aliifanya Simba msimu wa 2024-2025 kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa sasa Fadlu ambaye anahusishwa na Yanga ana mkataba wa Raja Casablanca baada ya kusaini dili la miaka miwili mwaka 2025, jambo linalomaanisha kuwa bado ana majukumu rasmi ndani ya miamba hiyo ya soka la Morocco hadi 2027.

FADL 01

Hali hiyo imeifanya Yanga kukutana na ukuta wa kwanza katika mpango wao wa kumshusha Jangwani, kwani taarifa zinaeleza kuwa klabu yoyote itakayohitaji huduma yake kabla ya mkataba wake kumalizika italazimika kulipa fidia ya kuvunja mkataba.

Inaelezwa kuwa kiwango hicho kinafikia Dola 600,000 ambazo ni zaidi ya Sh1.5 bilioni za Tanzania, fedha zinazotajwa kuwa sehemu ya kipengele maalumu cha ‘buyout clause’ kilichowekwa kwenye mkataba wake.

Kipengele hicho kina lengo la kulinda maslahi ya Raja Casablanca dhidi ya klabu yoyote itakayojaribu kumchukua kocha huyo kabla ya muda wake wa mkataba kuisha, hivyo kufanya dili hilo kuwa gumu kuliko ilivyodhaniwa awali.

FADL 02

Maana yake ni kwamba, Yanga haitahitaji tu makubaliano binafsi na Fadlu, bali pia italazimika kufanya mazungumzo ya kina na Raja Casablanca pamoja na kujiandaa na gharama kubwa za kimkataba.

Mbali na gharama ya fidia, mshahara wa Fadlu nao unaongeza uzito wa uamuzi ndani ya Yanga.

Taarifa zinaeleza kuwa kocha huyo kwa sasa analipwa takribani Dola 45,000 kwa mwezi nchini Morocco, kiwango kinachokadiriwa kuwa zaidi ya Sh117 milioni za Tanzania kabla ya bonasi na marupurupu mengine.

FADL 03

Iwapo Yanga itafanikisha dili hilo, basi italazimika pia kubadili mipango yake ya matumizi ili kuhimili mzigo wa mshahara wa kiwango hicho, jambo ambalo linaweza kuifanya klabu kuingia kwenye moja ya uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanywa kwa benchi la ufundi katika soka la Tanzania.

Ndani ya klabu hiyo tayari kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu kama ni sahihi kutumia fedha nyingi kiasi hicho kwa kocha mmoja au kama kuna umuhimu wa kutafuta chaguo lingine la gharama nafuu lakini lenye uwezo wa kuifikisha timu katika malengo yake ya kimataifa.

Licha ya ugumu wa dili hilo, jina la Fadlu bado linaendelea kubaki juu kwenye orodha ya makocha wanaovutiwa na Yanga kutokana na falsafa yake ya soka la kisasa, uwezo wa kujenga timu yenye ushindani pamoja na uzoefu wake katika mazingira ya soka la Afrika.

FADL 04

Fadlu alipotafutwa na Mwanaspoti, aligoma kuzungumzia taarifa hizo zaidi amesema nguvu zake ameelekeza katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Morocco ambapo Raja inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 42, moja zaidi ya Maghreb Fez ambayo inanolewa pia na kocha wa zamani wa Simba, Pablo Franco.

Tangu ajiunge na miamba hiyo ya soka la Morocco, Fadlu ameiongoza Raja kushinda mechi 12 katika ligi, sare sita na kupoteza tatu huku wakifunga mabao 26 na kuruhusu manane, ndio timu iliyoruhusu mabao machache zaidi.

Kwa sasa Yanga inaendelea na mchakato wa kusaka kocha mkuu wakati huu ambao kikosi hicho kinaongozwa kwa muda na Abdihamid Moallin akisaidiana na Patrick Mabedi baada ya Pedro Goncalves kusitishiwa mkataba Mei 6, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *