
Katika kuelekea Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani tarehe 31 Mei, WHO imesema zaidi ya watoto milioni 40 wenye umri wa miaka 13 hadi 15 duniani tayari wanatumia bidhaa za tumbaku. Shirika hilo linaonya kuwa kampuni za tumbaku na nikotini zinaendelea kubuni bidhaa zenye ladha na vifungashio vinavyowavutia vijana ili kuwafanya waathirike na uraibu mapema.
“Hata wakati tumbaku ikiendelea kuua mamilioni ya watu, kampuni kubwa za tumbaku zinaendelea kubadilisha mbinu zao za biashara kwa kuhamasisha matumizi ya sigara za kielektroniki, vifuko vya nikotini na bidhaa nyingine zinazolenga kuvuta kizazi kipya,” amesema Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa Idara ya Vichocheo vya Afya, Uhamasishaji na Kinga wa WHO.
Madhara ya tumbaku kwa watoto
WHO imeeleza kuwa nikotini ina madhara makubwa kwa watoto, kwa sababu ubongo wao bado unaendelea kukua. Shirika hilo limezitaka serikali kupiga marufuku bidhaa zenye ladha, kuzuia matangazo na udhamini wa bidhaa hizo, pamoja na kuhakikisha maeneo ya umma yanakuwa huru dhidi ya moshi na matumizi ya sigara za kielektroniki.
WHO pia imeonya kuwa vifuko vya nikotini, ambavyo ni miongoni mwa bidhaa zinazoongezeka kwa kasi sokoni, vinaendelea kutangazwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kutumia watu maarufu na mbinu zinazowavutia vijana. Shirika hilo limesema takribani nchi 160 bado hazina sheria maalumu za kudhibiti bidhaa hizo licha ya matumizi yake kuongezeka duniani.
Katika juhudi za kudhibiti matumizi ya bidhaa hizo, WHO imeipongeza Rio de Janeiro nchini Brazil kwa kuimarisha ukaguzi dhidi ya uuzaji na matangazo ya sigara za kielektroniki pamoja na kuendesha kampeni za uhamasishaji kwa umma.
Kwa mujibu wa WHO, matumizi ya tumbaku husababisha zaidi ya vifo milioni 7 kila mwaka duniani na ni miongoni mwa sababu kuu za vifo vinavyoweza kuzuilika, yakiwemo magonjwa ya moyo, matatizo ya mfumo wa hewa na aina zaidi ya 20 za saratani.
WHO imewahimiza watumiaji zaidi ya bilioni moja wa tumbaku na bidhaa za nikotini duniani kuanza safari ya kuacha matumizi hayo ifikapo tarehe 31 Mei.
