Wizara ya Afya ya Kongo: Idadi ya watu wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola imepindukia 1,000Wizara ya Afya ya Kongo: Idadi ya watu wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola imepindukia 1,000

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa idadi ya watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola nchini humo imepindukia 1,000 huku kukiwa na ongezeko la maambukizi katika majimbo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti ya Wizara ya Afya ya Kongo imeleeza kuwa, idadi ya watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola imefikia 1,077, na kwamba watu 121 wametibitishwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.  Aidha hadi sasa kumeripotiwa vifo 17 tangu kutangazwa mlipuko wa homa hiyo hatari, Mei 15 mwaka huu.

Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongeza kuwa, ugonjwa wa Ebola umeathiri maeneo 13 ya afya katika majimbo matatu, ikiwa ni pamoja na Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

“Operesheni za ufuatiliaji, uchunguzi na uhamasishaji wa jamii bado zimeimarishwa licha ya changamoto za kiutendaji zilizoripotiwa katika uwanja huo” imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya ya Kongo.

Mamlaka husika za Kongo tayari zimesitisha shughuli za kijamii huko Ituri, ambako ni kitovu cha mlipuko huo, zikiwemo shughuli za michezo, ili kuzuia kuenea kwa Ebola.

Roger Kamba Waziri wa Afya ya Umma wa Kongo ameeleza kuwa, karibu watu 3,600 waliwasiliana kwa karibu na wagonjwa wa Ebola.

Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kimetangaza kuwa nchi kumi ikiwa ni pamoja na Rwanda, Kenya, Tanzania, Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Ethiopia, Sudan Kusini na Zambia zinakabiliwa na hatari ya mlipuko wa Ebola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *