
Kibaha. Shehe wa Mkoa wa Pwani, Khamis Mtupa amesema elimu ya amali ni mkombozi mkubwa wa vijana katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira duniani, akieleza kuwa serikali haiwezi kuajiri wasomi wote wanaohitimu kila mwaka.
Shehe Mtupa amesema pamoja na taasisi binafsi na za umma kutoa nafasi za ajira, bado uwezo wake hauwezi kuwachukua wahitimu wote, hivyo vijana wanapaswa kujikita katika mafunzo ya amali yatakayowasaidia kujiajiri na kuwa wabunifu katika jamii.
Amesema hayo leo Mei 29, 2026 wakati akizungumza baada ya Swala ya mchana katika Msikiti wa Mwanalugali uliopo Kibaha Mkoa wa Pwani.
“Serikali imeendelea kupanua wigo wa elimu ya amali ili kuwafikia vijana wengi zaidi waweze kujifunza stadi mbalimbali zitakazowasaidia kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa,” amesema Shehe Mtupa.
Amesema kupitia elimu hiyo vijana wanaweza kupata maarifa ya ufundi, teknolojia, kilimo, biashara pamoja na shughuli nyingine za uzalishaji zitakazowafanya kuwa tegemeo kwa familia na taifa kwa ujumla.
“Ni muhimu wanafunzi wakawa na hekima, busara na utii. Wasikubali kurubuniwa na baadhi ya wanasiasa wanaotumia fedha kuwashawishi kushiriki migomo na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nch i na badala yake watumie fursa zinazotolewa na serikali ikiwemo mafunzo ya ujuzii,” amesema.
Aidha, amewataka vijana kufanya kazi kwa bidii popote watakapopata nafasi wakiamini kuwa kazi yoyote halali ina thamani katika kujenga maisha bora.
Kwa upande wake, Hadija Msangi ameipongeza serikali kwa kuendelea kuwekeza katika elimu ya amali akisema hatua hiyo itasaidia kuwaandaa vijana kujitegemea badala ya kutegemea ajira za ofisini pekee.
Amesema elimu ya amali inawawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa moja kwa moja unaoweza kutumika kuzalisha kipato mara baada ya kuhitimu masomo yao.
“Elimu ya amali inawajengea vijana uwezo wa ubunifu, kujiamini na kujitegemea kiuchumi. Hii ni njia nzuri ya kupunguza utegemezi kwa wazazi na jamii,” amesema Msangi.
Naye Shedrack Yohana ameishauri serikali kuharakisha zaidi utekelezaji wa mpango wa elimu ya amali nchini akisema ndiyo suluhisho la kudumu la changamoto ya ajira kwa vijana wengi.
Amesema mataifa mengi yaliyoendelea yamefanikiwa kiuchumi kutokana na kuwekeza zaidi katika mafunzo ya ufundi na stadi za kazi kwa vijana wao.
Kwa mujibu wa historia ya elimu nchini, mfumo wa elimu ya amali ulianza kupewa msukumo mkubwa Tanzania katika miaka ya 1960 na 1970 chini ya sera ya elimu ya kujitegemea iliyoasisiwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Hayati Julius Nyerere, ukiwa na lengo la kuwafanya wanafunzi kutumia elimu yao kujenga uchumi na kujitegemea.
Hata hivyo miaka kadhaa iliyopita utekelezaji wake ulienda kwa kusuasua na sasa serikali imeendelea kuweka mazingira stahiki katika kuhakikisha wanafunzi wananufaika na utaratibu huo.
Baadhi ya mataifa yaliyofanikiwa kupitia mfumo huo ni pamoja na Ujerumani, China na Korea Kusini ambayo yamewekeza katika elimu ya ufundi na teknolojia na kufanikiwa kuongeza ajira, uzalishaji viwandani pamoja na ukuaji wa uchumi.