Jumla ya wafugaji wadogo 92,831 na wadau wa mnyororo wa thamani wa maziwa wa Tanzania Bara na Visiwani-Zanzibar wamenufaika na Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa (TI3P) tangu ulipoanzishwa mwezi Machi mwaka 2022, ambapo asilimia 30 ya wanufaika hao ni wanawake.
Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania – TADB pamoja na Bill & Melinda Gates Foundation huku ukitekelezwa kwa kushirikiana na Heifer International, Land O’Lakes Venture37 pamoja na Tanager.
Akiongea wakati wa Maonesho ya Wiki ya Maziwa Mkoani Iringa, Mratibu wa Mradi wa TI3P, Joseph Mabula amesema mradi huo unalenga kutatua changamoto mbali mbali zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ndogo ya maziwa ili kuongeza uzalishaji, na kuboresha kipato cha wafugaji wadogo wa maziwa nchini huku akiishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa uzito mkubwa sekta ndogo ya maziwa.
Mabula amesema tangu kuanza kwake, mradi umewezesha utolewaji wa mikopo wa Zaidi ya shilingi bilioni 42 kwenye sekta ndogo ya maziwa ikiwalenga wasindikaji wa maziwa, wafugaji, wasambazaji wa pembejeo, pamoja na wadau wengine kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa.
Fedha hizo zimewezesha uanzishwaji wa viwanda vipya vya kuchakata maziwa pamoja na upanuzi na maboresho kwa jumla ya viwanda 17 vya usindikaji vimefikiwa kwa uwekezaji wenye thamani ya shilingi bilioni 22.8.
Aidha, mradi umewezesha ununuzi wa mitamba 3,330 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11.09, hatua iliyochangia kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa nchini.
Kupitia mradi huo, wafugaji wameendelea kupata huduma za ugani, pembejeo bora, masoko, pamoja na huduma za kifedha kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ndogo ya maziwa, jumla ya wasindikaji 19 wa maziwa wamenufaika na programu za kuongeza uwezo, huduma za ugani, na ufanisi katika uzalishaji.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *