
PARIS, UFARANSA. Akiwa na bao au pasi ya bao katika michezo saba mfululizo ya hatua ya mtoano, hakuna mchezaji aliyeathiri zaidi hatua za mwisho za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu kuliko winga wa kimataifa wa Georgia na PSG, Khvicha Kvaratskhelia maarufu kama Kvaradona.
Kwa mabilioni ya watazamaji watakakuwa wakifuatilia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya shisi ya Arsenmal inayopigwa leo usiku katika dimba la Puskas Arena, Hungary. Tangu aanze kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa PSG, Kvaratskhelia amekuwa sehemu muhimu ya mashambulizi ya timu hiyo na katika msimu wa 2025-26, anashika nafasi ya juu pamoja na Harry Kane na Kylian Mbappe kwa kuhusika kwenye mabao mengi zaidi kwenye mashindano hayo (16)
Muhimu zaidi ni kwamba ameonyesha kiwango bora katika mechi kubwa zaidi, akiwa na mabao au asiti 10 katika hatua ya mtoano msimu huu kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kwenye mashindano na pia amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga au kutoa pasi ya bao katika mechi saba mfululizo za hatua ya mtoano ndani ya msimu mmoja wa michuano hiyo.
Kvaratskhelia hashiriki tu katika kujenga mashambulizi ya PSG, bali ndiye anayepanga kasi ya mashambulizi kupitia uwezo kushambulia kwa nguvu. Ingawa takwimu zake za kushambulia ni za kawaida, tukio moja katika nusu fainali dhidi ya Bayern Munich kwenye Uwanja wa Allianz Arena lilionyesha uwezo wake.
Bao la kwanza la PSG lililofungwa baada ya dakika tatu tu ni mfano bora wa kasi binafsi ndani ya mfumo wa timu. Shambulizi hilo lilianza na pasi kutoka kwa Willian Pacho na akiwa katika nusu ya uwanja amegeuzia mgongo langoni, Kvaratskhelia hakujaribu kugeuka kwenye msongamano wa wapinzani. Badala yake, alitoa pasi ya haraka kwa mguso mmoja kwenda kwa Fabian Ruiz.
Kabla hata mpira haujatoka mguuni mwake, tayari alikuwa akizunguka na kuanza kukimbia. Alimwacha beki wa Bayern Munich, Dayot Upamecano nyuma hadi kuwa tishio. Ruiz aliendana na kasi hiyo kwa kumpasia mpira mzuri kwenye nafasi wazi na Kvaratskhelia huyohuyo ndani ya sekunde tatu tayari alikuwa amevuka mstari wa kati akikimbia kwa nguvu kuelekea lango la Bayern.
Baada ya miguso minne tu kuusafirisha mpira hadi eneo la mwisho la ushambuliaji alitulia kuangalia pa kupasia na badala ya kupiga krosi ya haraka alitoa pasi ya nyuma iliyomkutaa Ousmane Dembele ambaye alifunga kwa urahisi.
Ingawa bao hilo lilitegemea maono ya Ruiz na mwendo wa Dembele, Kvaratskhelia ndiye aliyekuwa injini ya shambulio. Ndani ya sekunde tisa tu, aligusa mpira mara tano na kukimbia zaidi ya mita 60, akibadilisha tukio la kawaida la kuokoa mpira katika nusu yao kuwa bao muhimu.
Maendeleo makubwa zaidi ya Kvaratskhelia chini ya Luis Enrique ni namna alivyoimarika katika ulinzi na kocha huyo akimzungumzia anasema, “ana uwezo mkubwa wa kucheza kama mlinzi; tunahitaji wachezaji wote 11 walinde.”
Hali hiyo ilionekana katika mchezo wa marudiano dhidi ya Bayern ambapo PSG walilazimika kucheza muda mwingi bila mpira.
“Kiufundi nilikuwa bora hata nikiwa Napoli,” anasema Kvaratskhelia na kuongeza:
“Lakini nimeimarika sana katika ulinzi chini ya Luis Enrique. Ukiwa na kocha huyu, lazima ushambulie kama mshambuliaji na ulinde kama beki.”
Takwimu zinaonyesha kwamba Kvaratskhelia ni mmoja wa mawinga wawili waliotoa presha kali zaidi mara 800 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu hatua za mtoano za msimu uliopita. Ingawa maeneo anayocheza zaidi bado ni upande wake wa kushoto, hivi sasa jukumu lake limekuwa la kuleta uwiano wa kimfumo na kubadilishana nafasi mara kwa mara na wachezaji kama Desire Doue na Bradley Barcola.
Mbali na kiungo Vitinha ambaye ndiye moyo wa timu, Kvaratskhelia mara nyingi zaidi hucheza pasi na mabeki wa pembeni Nuno Mendes pamoja na Achraf Hakimi na bila mpira uwezo wake wa kurudi nyuma kusaidia ulinzi na kuingia ndani huwapa uhuru mabeki hao wawili kupanda mbele kushambulia.
Kujitoa huko kumembadilisha Kvaratskhelia kutoka mchezaji wa burudani kuwa mmoja wa washambuliaji waliokamilika zaidi Ulaya. Hilo linaweza kuwa jambo muhimu katika fainali dhidi ya Arsenal, wakati PSG ikisaka kuwa klabu ya pili tu katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutetea ubingwa wake.