
Umoja wa Wasomi wa Kiislamu Duniani umetangaza upinzani wake kamili kwa tishio lolote linaloelekezwa kwa nchi za Kiislamu au mataifa yao kutoka upande wowote ule, na kuonya kuhusu matokeo mabaya ya kunzisha uhusiano na utawala wa Tel Aviv.
Muungano huo umesisitiza kwamba kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel kuna madhara kwa nchi za Kiislamu.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Wasomi Waislamu Duniani imeonya dhidi ya majaribio ya kulazimisha mipango ya kisiasa na ya kikanda ambayo inadhoofisha mamlaka ya kujitawala ya nchi za Kiislamu, na imetaja mradi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv kuwa unalenga kuunga mkono uvamizi wa utawala wa Kizayuni unaoikalia Palestina kwa mabavu.
Muungano huo umezitaka nchi za Kiislamu kuchukua msimamo wa pamoja na wenye maamuzi dhidi ya mashinikizo ya aina yoyote yanayolenga kuzisukuma nchi za kikanda upande wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.
Ikiashiria mwendelezo wa sera za utawala wa Kizayuni huko Gaza, Lebanon na maeneo mengine, taarifa hiyo imevitaja vitendo hivyo kuwa ni mauaji ya kimbari na uharibifu uliopangwa, na kuilaumu jamii ya kimataifa kwa kumyamaza kimya na ushiriki wake katika suala hilo.
Muungano huo umeonya dhidi ya kuunganisha makubaliano yoyote ya kimataifa au ya kikanda na suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel.
Umoja wa Wasomi Waislamu Duniani umesema sera hizi ni kinyume na sheria za kimataifa, kanuni za maadili na mamlaka ya kujitawala ya nchi, na kusisitiza udharura wa kukataliwa njia yoyote inayohalalisha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala uvamizi wa Israel ambao unashutumiwa kwa kutenda uhalifu mkubwa dhidi ya watu wa Palestina.