
Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura ametoa maelekezo matatu kwa watendaji wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi akisema yataimarisha ubora wa utendaji na ufanisi wa kazi zao.
Maelekezo hayo ni kuzingatia nidhamu ya kitaaluma, kuwa na uadilifu binafsi pamoja na kujenga utamaduni wa kujifunza kila wakati ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
IGP Wambura amtoa maelekezo hayo leo Jumatatu, Juni mosi, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha watendaji wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi kilichofanyika Shule ya Polisi Moshi, mkoani Kilimanjaro
Akizungumza katika kikao hicho, amesema uchunguzi wa sayansi ya jinai unahitaji umakini mkubwa, weledi wa hali ya juu na uzingatiaji wa taratibu katika kila hatua ya kazi.
“Kosa dogo katika ukusanyaji, uhifadhi au uchambuzi wa ushahidi linaweza kuathiri mwelekeo wa uchunguzi na hata mwenendo wa shauri mahakamani,” amesema.
Amesema watendaji wa kamisheni hiyo wanapaswa kuhakikisha kila hatua wanayochukua, inazingatia viwango vya kitaaluma na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa taaluma zao.
“Uaminifu wa matokeo ya uchunguzi wenu utaamuliwa na namna mlivyozingatia misingi hiyo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kazi husika,” amesema.
Akizungumzia uadilifu binafsi, IGP Wambura amesema huo ndiyo mtaji mkubwa wa mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi wa jinai na kwamba, ushahidi haupaswi kupotoshwa wala kuathiriwa kwa sababu binafsi au ushawishi wa mtu au kundi.
Amesema wataalamu hao ni sauti ya ukweli kwa waathirika wa uhalifu, watuhumiwa na jamii kwa jumla.
“Ukweli ndio unaojenga uaminifu wa wananchi kwa uchunguzi wa kisayansi na kwa Jeshi la Polisi, wanapolinda ukweli wanalinda haki,” amesema.
Kuhusu kujifunza, IGP Wambura amesema sayansi na teknolojia hubadilika kila siku huku wahalifu wakibadilisha mbinu zao sambamba na maendeleo hayo, hivyo watendaji hawapaswi kuridhika na maarifa waliyonayo.
“Jengeni utamaduni wa kujifunza kila wakati, fanyeni tafiti someni majarida ya kitaaluma na fuatilieni maeneo mapya ndani ya taaluma zenu,”amesema.
Amesema uimara wa kamisheni hiyo utategemea kiwango ambacho watendaji wake wataendelea kujiendeleza kitaaluma na kushirikishana maarifa katika vituo vyao vya kazi.
Awali, IGP Wambura amesema ushahidi hauzungumzwi kwa maneno bali kupitia ukweli uliopo, na ukweli huo huhitaji wataalamu wenye ujuzi wa kuusoma, kuuchambua na kuutafsiri kwa usahihi.
Katika uchunguzi wa jinai, amesema Jeshi la Polisi haliwezi kutegemea hisia, mazoea au dhana, bali ushahidi wa kitaalamu unaoweza kusimama mahakamani bila kuacha shaka.
“Hatuwezi kukabiliana na changamoto hizi bila kuwekeza kikamilifu katika sayansi ya uchunguzi wa jinai. Jeshi la Polisi litaendelea kuipa kipaumbele kamisheni hii kwa vifaa, teknolojia na rasilimali watu,” amesema.
Pia, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanashirikisha wenzao maarifa watakayopata ili kuongeza uwezo wa pamoja ndani ya kamisheni.
Mahitaji yaliyoibuliwa
Akiwasilisha taarifa mbele ya IGP Wambura, Kamishna wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai, Shaban Hiki ameomba ofisi mpya za makamanda wa polisi wa mikoa zinazojengwa nchini, kutengewa maeneo maalumu ya kuhifadhi vielelezo, hususan sampuli za uchunguzi.
Amesema ukaguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali umebaini baadhi ya maeneo ya kuhifadhi sampuli yamepitwa na wakati na hayakidhi mahitaji ya sasa.
“Unakuta kielelezo kimehifadhiwa pamoja na vifaa vingine visivyohusiana, tunaomba kila kituo kipya kinachojengwa kiwe na eneo maalumu la kuhifadhi sampuli,” amesema.
Kamishna Hiki ameomba kuimarishwa kwa usalama wa watendaji wa uchunguzi wa kisayansi wanapokwenda kukagua maeneo ya matukio ya uhalifu.
Amesema uzoefu wa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, umeonesha umuhimu wa kuwawezesha magari maalumu ya ukaguzi kwa matukio yenye uwezo mkubwa wa ulinzi.
“Tunaomba idara ya ukaguzi wa matukio, hususan ya makao makuu, ipatiwe gari maalumu la ukaguzi wa matukio lenye uwezo mkubwa wa ulinzi,” amesema.
Aidha, amesema baadhi ya mikoa, vikosi na vitengo vya uchunguzi wa kisayansi bado vinaongozwa na askari wasio maofisa, hali inayopunguza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu.
Amesema baadhi ya maeneo muhimu ya kimkakati ikiwamo viwanja vya ndege na mipaka ya nchi bado hayana watendaji wa kutosha wa uchunguzi wa kisayansi.
Naibu Kamishna wa Polisi, Mwamini Rwantale, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa kamisheni katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesema mafunzo hayo yanahusu udhibiti wa matukio ya uhalifu, ukaguzi wa maeneo ya matukio, utambuzi wa vielelezo, uchukuaji wa sampuli pamoja na utunzaji, ufungashaji na usafirishaji wa ushahidi.
“Baada ya mafunzo haya washiriki wataweza kutekeleza majukumu yao ya msingi kwa ufanisi zaidi,” amesema.