Kama kuna ubongo makini nyuma ya mafanikio ya Serengeti Boys hadi kufika fainali ya AFCON 2026, basi ni mtu wa kuitwa Oscar Mirambo.

Huyu jamaa ndio mchora ramani ya safari yote ya mafanikio haya, na ndio mnemba maono ya kiufundi ya shirikisho la soka hapa nchini, TFF.

Kwa sasa anakaimu nafasi ya katibu mkuu wa TFF, lakini kabla ya hapo alikuwa mkurugenzi wa ufundi wa TFF.

Akiwa msomi wa elimu zote, ya shule ya kawaida na mpira, Mirambo ndiye aliyeanzisha na kuisimamia kwa umakini mkubwa program maalumu ya vijana pale Mnyanjani.

Kituo hiki kinachofahamika kama TDS au TFF Akademi, ndicho kilicholea vijana hawa kwa muda mrefu sana hadi haya matunda yanayotokea.

Ili kutimiza malengo, yeye mwenyewe alihamishia ofisi yake Tanga kutoka makao makuu ya TFF, Karume Ilala Dar es Salaam.

Zaidi ya kusimamia kituo hicho, Mirambo ambaye ni mkufunzi wa CAF na FIFA, na pia mkufunzi wa Wakufunzi wa CAF na FIFA (CAF & FIFA Coach Educators’ Developer) amekuwa akiendesha kozi za makocha kituoni hapo.

Akishirikiana na makocha wengine kadhaa ambao amekuwa akiwazalisha, Mirambo akaweka nguvu, akili na maarifa yake yote kwenye kusaka vipaji nchi nzima na kuvipeleka Tanga kuvilea.

Leo Serengeti Boys wanaandika historia, sio dhambi kuliweka mbele jina la Oscar Mirambo kama mshika ufunguo wa milango hii inayolifungukia soka la Tanzania kwa sasa.

Hata hivyo, hakuna namna yoyote unayoweza kumuweka pembeni Rais wa shirikisho la soka hapa nchini TFF bwana Wallace Karia.

Oscar ni mwajiriwa wa TFF iliyo chini ya Rais Wallace Karia.

Oscar Mirambo.

Maana yake kila anachokifanya kina baraka zote za Rais Karia.

Maono na mipango yote ya Oscar inahitaji uwezeshwaji wa kisera na kifedha kutoka TFF ya Karia.

Endapo Karia angekuwa sio mwelewa, angeweza kukataa mawazo ya Mirambo na kujaribu namna nyingine.

Kuweka wale watoto pale Tanga kwa miaka yote hiyo ni gharama kubwa sana.

Hakuna kiongozi anayependa kuendesha mradi wa gharama kubwa ambao kwanza mafanikio yake hayaonekani moja kwa moja, na pili ipo njia mbadala.

Njia mbadala ni kwamba duniani kote kulea vipaji kupitia akademi sio jukumu la moja kwa moja la shirikisho.

Ni jukumu la vilabu mbalimbali ambavyo ndivyo vina akademi.

Shirikisho majukumu yake ni kuchagua tu vijana walio bora kutoka hizo akademi na kwenda kuwatumia.

Lakini Oscar Mirambo alipokuja na wazo la kuanzisha akademi ya TFF na kuwalea vijana, Karia akakubali…licha ya kuyajua yote hayo.

Hapo lazima Karia apewe maua yake.

Lakini hata hivyo, zaidi ya haya yote, kuna mtu ambaye hapaswi kabisa kusahaulika, naye ni Rais wa pili wa TFF, Jamal Malinzi.

Malinzi ambaye aliiongoza TFF kuanzia 2013 akichukua kijiti cha uongozi kutoka kwa Rais wa kwanza, Leodeger Tenga, alitawala hadi 2017, ndipo akaingia Wallace Karia.

Chini ya utawala wa Malinzi ndio Oscar Mirambo aliingia TFF, kama chaguo la Rais Malinzi mwenyewe.

Mirambo alikuwa mwalimu wa shule ya sekondari Makongo, iliyopo Lugalo, katikati ya Mwenge na Kawe Dar es Salaam.

Alikuwa mwalimu mkali sana wa Hisabati, lakini pia na michezo…hasa mpira.

Kama ambavyo inajulikana, Makongo ni shule ya kulea vipaji vya wanamichezo tangu zamani.

Kwa hiyo Oscar Mirambo akawa anaendeleza kazi ya miaka mingi, tangu zama za akina Tambwe Leya (marehemu), Juma Matokeo, (marehemu), Joseph Kanakamfumu na makocha wengine wakubwa waliopita pale.

Lakini baadaye mambo hayakumuendea sawa, alipishana mtazamo na wamiliki wa shule, akaacha kazi.

Ndipo simu ya Jamal Malinzi ikaita, akimtaka aisaidie TFF kulea watoto kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2017 Gabon.

Wakati huo TFF ya Malinzi ilikuwa ikilea vipaji katika shule ya Alliance ya Mwanza.

Mirambo akachukuliwa awe kiungo kati ya TFF na shule ile katika kusimamia maendeleo ya vijana wale.

Hivyo ndivyo Oscar Mirambo alivyoingia TFF.

Mambo yakaenda kasi, AFCON ya Gabon ikafika na kupita, Tanzania ikaishia makundi… Oscar akiwa kocha chini ya Kim Poulsen, kocha wa zamani wa Taifa Stars.

Malinzi akatoka na kuingia Karia…naye akaendelea kumuamini Oscar Mirambo.

Ikaja AFCON ya 2019 ambayo Tanzania ilikuwa mwenyeji, Oscar akawa kocha mkuu.

Hata hivyo timu ikaishia tena hatua ya makundi, na Oscar Mirambo akaondolewa kwenye nafasi ya ukocha na kupelekwa kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Watu wengi, hasa wachambuzi walibeza sana uteuzi huu wakisema mtu aliyefeli na Serengeti Boys anaweza kuwa mkurugenzi wa ufundi, nafasi ya kubeba maono ya taifa kisoka?

Lakini Karia alifumba macho na kumpa nafasi Mirambo.

Baada ya kuwa mkurugenzi wa ufundi, kazi yake ya kwanza ilikua kuitafsiri dira (vision) ya shirikisho kwenye falsafa ya kucheza na kufundishia mpira wa miguu kuanzia ngazi ya awali (curriculum philosophy).

Dira ndio ramani inayotasfiri hatua kwa hatua maendeleo ya mpira wa miguu, vipaumbele vikiwa;

Kwanza maendeleo ya mpira wa vijana na mafunzo kwa makocha (Youth Football Development and Coach Education Pathway).

Pili muunganiko wa dira ya TFF katika elimu ya makocha na falsafa ya mpira (integration of TFF vision in Coach Education and football philosophy).

Sasa hapo ndipo alipokuja na wazo tofauti kabisa, kwamba TFF iandae vijana badala ya kuviachia vilabu kufanya kazi hii.

Vilabu vinajitahidi sana lakini kuna kitu cha msingi vinakosa; kwanza kuzingatia umri na pili kuwekeza kwenye maendeleo halisi ya hawa vijana.

Vilabu vingi zinafanya kazi hii juu juu kukwepa gharama.

Vingine hata akademi havina…lakini kwa kuwa akademi ni sharti la kikanuni, basi vilabu huutua mzigo wa akademi kwa vituo vya mtaani na kuvipa baraka ya kutumia jina.

Kwa hiyo kuvitegemea vilabu hivi ili vikuzakishie vijana wa kushindana kimataifa, tungechelewa sana na kuona makocha hawafai, kama alivyoonekana yeye mwenyewe.

Ndipo kikaanzishwa kituo cha Tanga…kilichofuata baada ya hapo ni historia, Serengeti Boys wale pale kwenye fainali.

Tuwapongeze vijana wetu kwa jitihada zao, tumpongeze kocha wao Elieneza Nsanganzelu na benchi lake lote.

Tuwapongeze TFF na Rais Wallace Karia kama mbeba dhamana.

Tusimsahau Jamal Malinzi, aliufungua huu mlango.

Lakini kipekee kabisa tumpongeze Oscar Mirambo kama mbeba maono.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *