RABAT, MOROCCO: WAKATI Tanzania ikijiandaa kwa mechi kubwa zaidi katika historia ya soka lake la vijana, kuna jina moja ambalo limekuwa nguzo muhimu katika safari ya ajabu ya Serengeti Boys kufika fainali ya Mataifa ya Afrika U-17.

Kipa Haji Abdallah aliyekulia katika Kituo cha Ufundi cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ameibuka kuwa mmoja wa wachezaji waliotulia na kuonyesha kiwango bora zaidi katika mashindano hayo huku Tanzania U-17 ikitinga katika fainali yao ya kwanza Afrika.

Leo Tanzania itakutana na mabingwa wa zamani wataji hilo Senegal U-17 ikiwa na nafasi ya kuhitimisha safari yake ya kihistoria kwa kutwaa taji la kwanza.

Ingawa mara nyingi sifa nyingi huenda kwa wafungaji wa mabao, utulivu na uwezo wa Haji Abdallah wa kuokoa michomo ya hatari vimekuwa muhimu sana katika kuifikisha Tanzania hatua ambayo haijawahi kufikiwa hapo awali.

KIP 01

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 16, ambaye pia ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kihere, amekuwa ishara ya mafanikio ya mfumo wa maendeleo ya soka la vijana nchini Tanzania.

Licha ya ukubwa wa tukio hili na matarajio makubwa ya taifa zima, Abdallah ameendelea kuwa mnyenyekevu na mwenye utulivu.

“Asante. Hii si mafanikio yangu pekee, ni ya timu, benchi la ufundi na taifa lote. Kama mchezaji, lazima niwe mtulivu ili kusaidia kushinda mechi.”

Kauli hiyo inaonyesha fikra zake za kuweka timu mbele ya maslahi binafsi, jambo ambalo limekuwa moja ya siri za mafanikio ya Serengeti Boys katika mashindano haya.

KIP 02

Kipa Williams ndiye mfano wake Abdallah amesema kuwa mtu anayemvutia zaidi ni golikipa na nahodha wa Mamelodi Sundowns pamoja na timu ya taifa ya Afrika Kusini, Ronwen Williams.

“Napenda kumuangalia Ronwen Williams kwa sababu akiwa uwanjani anafanya kazi yake vizuri ili timu yake ishinde. Hachezi akiwa na presha.”

Kiwango bora ya Williams katika AFCON iliyopita hasa uwezo wake wa kuokoa penalti, yalimuacha Abdallah akiwa na hamasa kubwa ya kufuata nyayo zake.

Sifa za utulivu na kujiamini ambazo Williams ameonyesha kwa miaka mingi zimeonekana pia kwa Abdallah katika mashindano haya, hasa katika ushindi wa nusu fainali dhidi ya Misri U-17 ambapo aliokoa michomo muhimu na kusaidia Tanzania kufuzu fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *