Mamilioni ya Waethiopia watapiga kura kote nchini lro Jumatatu Juni 1, 2026, kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge, ambao utatoa nafasi ya kuchaguliwa Waziri Mkuu. Isipokuwa huko Tigray, eneo la kaskazini lililoharibiwa na vita vilivyomalizika mwaka wa 2022, ambapo uchaguzi hautafanyika.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu huko Addis Ababa,

Kwa wiki chache zilizopita, malori yaliyopambwa kwa rangi za Chama tawala cha Prosperity yamekuwa yakipita kaika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Vipaza sauti vilikuwa wikisikika kwa muziki, ukikatizwa na sauti inayowahimiza wakazi kwenda kupiga kura.

Leo Jumatatu, Juni 1, wapiga kura milioni 50 wameitwa kupiga kura kuwachagua wajumbe 547 wa Baraza la Wawakilishi, bunge la shirikisho. Wabunge hawa watamchagua Waziri Mkuu, kiongozi wa serikali nchini Ethiopia, ambapo rais ana jukumu tu la heshima..

Lakini mwaka huu tena, kama ilivyokuwa mwaka wa 2021, uchaguzi hautafanyika katika maeneo 38 ya Tigray. Miaka mitano iliyopita, jimbo hilo lilikumbwa na vita. Lakini leo, miaka mitatu na nusu baada ya Mkataba wa Pretoria uliositisha mapigano na vita kumalizika, “kufanyika kwa uchaguzi bado bado ni ndoto huko Tigray, kutokana na hali mbaya ya usalama na kuanguka kwa mfumo wa kisiasa,” anasema Muauz Gidey, mtafiti katika Taasisi ya Mafunzo ya Siasa ya Tigray.

Hakika, mvutano kati ya serikali na jimbo hilo umeongezeka kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni. Mwishoni mwa mwezi Januari, mapigano ya moja kwa moja kati ya jeshi la shirikisho na vikosi vya Tigrayan (TDF) yalitokea katika eneo la mbali la Tsemlet, mapigano ya kwanza kama hayo tangu vita kumaliika mnamo mwezi Novemba 2022.

Kulingana na mtafiti, uwezekano wa mgogoro mpya umefanya hata Kikosi cha Ukombozi wa Watu cha Tigray (TPLF), ambacho kinatawala eneo hilo, “kulazimisha kuandikishwa kwa lazima” na “kuhamasisha maelfu ya vijana wa Tigray.” Na mwanzoni mwa mwezi Mei, ndege za kivita za jeshi la shirikisho zilionekana mara mbili juu ya Mekele, “kama onyesho la nguvu,” ameongeza.

Tigray “imetengwa”

Mazungumzo ya kisiasa kati ya Addis Ababa na Mekele pia yamekwama. Mnamo Aprili 8, kuteuliwa tena kwa Jenerali Tadesse Werede kama mkuu wa Utawala wa muda wa Tigray na serikali ya shirikisho kuliwakasirisha viongozi wakuu wa TPLF, akiwemo rais wa chama hicho Debretsion Gebremichael.

Akijibu uteuzi huo, katikati ya mwezi Aprili, Gebremichael alirejesha bunge la kikanda la kabla ya vita, ambalo Addis Ababa inaliona kuwa si halali. Bunge hili lilifanya uchaguzi mara ya mwisho mwaka wa 2020, baada ya serikali ya Ethiopia kukataa ombi lake la kuahirisha uchaguzi wa wabunge kwa mwaka mmoja. Uchaguzi huo, uliokataliwa wakati huo na serikali ya shirikisho, ulikuwa mojawapo ya vichocheo vya vita, ambavyo vilisababisha vifo vya watu wasiopungua 600,000 kati ya mwaka 2020 na 2022.

Kurejeshwa kwa bunge la kabla ya vita ni “mapinduzi ya kweli, yenye matokeo mabaya,” anasema Muauz Gidey. “Kwa kudhoofisha taasisi zilizowekwa na Utawala wa muda, kwa lengo la kulinda utawala wao wa kisiasa na kijeshi, wanachama wa zamani wa TPLF wameitenga Tigray kutoka kwa mfumo wa katiba wa shirikisho. Katika muktadha huu, haiwezekani kuwashirikisha Watigray katika mchakato wowote wa uchaguzi.” 

Kwa Kinge Hadush Belay, rais wa chama cha upinzani cha Tigray Salsay Weyane Tigray (Sawet), wakazi wa eneo hilo kwa sasa “wanashikiliwa mateka” “kati ya chama kinachopigania uhai wake” na serikali ya shirikisho, ambayo “haitoi mazingira yanayofaa kwa uchaguzi na mazungumzo.”

“Tunapigania kuishi”

Kwa mtazamo wa vifaa, kuandaa uchaguzi katika eneo ambalo zaidi ya watu 750,000 waliohamishwa na vita bado wanasubiri katika kambi nyingi, haiwezekani.

Watu hawa wanatoka Tigray Magharibi, ambapo, kulingana na shirika la Human Rights Watch, miongoni mwa wengine, uhalifu dhidi ya ubinadamu na kampeni ya utakaso wa kikabila vilifanywa wakati wa mzozo. Tangu vita, eneo hili limebaki chini ya utawala wa mamlaka ya eneo jirani la Amhara, ambao, kulingana na ripoti kadhaa, hutekeleza sera za kibaguzi dhidi ya Watigray.

Hata hivyo, eneo hilo linakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi tangu mwanzo wa mwaka. Usambazaji wa pesa taslimu umesitishwa, na utoaji wa bajeti ya kikanda kutoka kwa serikali ya shirikisho umecheleweshwa sana.

Matatizo haya hufanya maisha ya kila siku kuwa magumu sana kwa wakazi na kuchochea uchovu mkubwa wa siasa. Semhal (jina limebadilishwa kwa ombi lake) aliondoka Mekele miezi minne iliyopita na kwenda kufanya kazi katika mgahawa huko Addis Ababa. “Maisha yamekuwa magumu sana huko Tigray, kila kitu ni ghali, na tunajitahidi kuishi,” anasema. “Kwa hivyo, kufikiria kuhusu uchaguzi, kujihusisha na siasa, hilo si kipaumbele kwa watu hata kidogo. Ni anasa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *