Arusha. Kundi la wanafunzi sita wa kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari ya Arusha Sayansi wamebuni mfumo wa kidijitali wa kibiashara unaowaunganisha wakusanya taka na warejelezaji wa taka kimtandao.
Mfumo huo unaoitwa “Cyclo- Geuza Taka Kuwa Utajiri” ni soko la kidijitali na mfumo wa usimamizi wa taka unaowaunganisha wazalishaji wa taka, wakusanyaji na kampuni za urejelezaji kupitia jukwaa moja, kwa lengo la kufanya biashara.
Lengo ni kubadili changamoto ya taka inayoongezeka nchini na kuwa fursa za kiuchumi huku ukichangia uhifadhi wa mazingira
Ubunifu huo unakuja wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na ongezeko la taka ngumu.
Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), nchi huzalisha kati ya tani milioni 14.4 hadi milioni 20.7 za taka ngumu kila mwaka.
Hata hivyo, chini ya asilimia 50 ya taka hizo hukusanywa rasmi, huku asilimia 5 hadi 10 pekee zikirejelewa.
Akizungumza jijini Arusha leo Juni Mosi, 2026 wakati wa maonyesho ya kwanza ya mahafali ya ubunifu wa kisayansi chini ya programu ya Science-to-Use (SITU), mmoja wa wabunifu wa mradi huo, Shawn Mareale, amesema Cyclo inalenga kuziba pengo la taarifa lililopo kati ya wazalishaji wa taka, wakusanyaji na kampuni za urejelezaji.
“Cyclo ni jukwaa la kidijitali linalorahisisha usimamizi wa taka kwa kuwaunganisha wazalishaji, wakusanyaji na warejelezaji katika mfumo mmoja ulioratibiwa.
Amesema mfumo huo una huduma za kuomba ukusanyaji wa taka, ufuatiliaji wa kidijitali wa mzunguko wa taka, uratibu wa uchambuzi na urejelezaji wa taka, soko la bidhaa zinazoweza kurejelewa pamoja na zana za uchambuzi wa takwimu zinazosaidia mikakati ya muhitaji na muuzaji kukutana na kufanya biashara.
Kwa mujibu wa Mareale, ubunifu huo unatarajiwa kupunguza kiasi cha taka kinachopelekwa dampo, kuzalisha ajira za kijani, kukuza sekta ya urejelezaji, kuboresha usafi wa miji na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga uchumi wa kijani na endelevu.
Mwanafunzi mwingine katika timu hiyo, Janelle John Dominick, amesema ukuaji wa haraka wa miji na shughuli za viwanda umeongeza kwa kiasi kikubwa taka za plastiki na viwandani, huku mifumo duni ya usimamizi wa taka ikiendelea kuhatarisha mazingira na afya ya jamii.
“Vifaa vingi vyenye thamani vinavyoweza kurejelewa kama nguo, chupa, vifaa vya umeme na elektroniki pamoja na plastiki hutupwa badala ya kutumika tena kutokana na kukosekana kwa mfumo madhubuti unaowaunganisha wazalishaji wa taka na wakusanyaji pamoja na warejelezaji,” amesema.
Mwanafunzi Theo Mwalekwa Kikula amesema mtumiaji hutuma ombi la kukusanya taka kupitia programu hiyo, ambapo mfumo huunganisha moja kwa moja ombi hilo na mkusanyaji aliyethibitishwa na aliyepo karibu.
“Baada ya hapo, mkusanyaji huratibu usafirishaji na ukusanyaji wa taka huku miamala yote na taarifa za maendeleo ya huduma zikisimamiwa kidijitali ndani ya mfumo,” amesema.
Mbali na kurahisisha ukusanyaji wa taka, Cyclo pia inahamasisha ubadilishaji wa taka kuwa bidhaa zenye thamani zaidi, ikiwemo vifaa rafiki kwa mazingira vya ujenzi, na hivyo kufungua fursa mpya za biashara kutoka kwenye rasilimali ambazo zingetupwa damponi.
Ubunifu huo uliwasilishwa katika mahafali ya kwanza ya miradi ya wanafunzi chini ya programu ya SITU, inayolenga kuhamasisha ubunifu wa kisayansi wenye matumizi ya moja kwa moja katika jamii pamoja na ujasiriamali.
Mkuu wa Idara ya Sayansi shuleni hapo, Ally Msangi, amesema programu hiyo inalenga kujenga kujiamini, uwezo na ubora kwa wanafunzi kwa kuwahamasisha kutambua changamoto za kijamii na kubuni suluhisho za vitendo.
“Miradi hii inaonesha uwezo wa wanafunzi kufikiri kwa kina, kufanya ubunifu na kutatua changamoto za jamii. Lengo letu ni kuhakikisha mawazo yao yanatoa mchango chanya kwa jamii huku yakifungua fursa za kiuchumi,” amesema.
Msangi amesema programu ya SITU ilianzishwa mwaka 2025 ambapo wanafunzi wa kidato cha tano hupatiwa mafunzo ya ubunifu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema kati ya miradi 28 iliyobuniwa katika awamu ya kwanza, miradi 19 imekamilika kwa mafanikio.
Miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali zikiwemo sayansi, teknolojia, nishati jadidifu, ujasiriamali, uhifadhi wa mazingira na afya.
Aliongeza kuwa shule imejipanga kuendelea kuunga mkono ubunifu hata baada ya wanafunzi kuhitimu ili kuhakikisha unakuwa bidhaa au huduma zinazoweza kutatua changamoto za jamii huku zikiwaingizia kipato wabunifu hao vijana.
“Tunataka ubunifu huu ufungue milango kwa wanafunzi, uzalishe ajira na kuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi. Tunatoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono miradi ya wanafunzi kupitia ufadhili na ushauri wa kitaalamu,” amesema.
Mkuu wa Shule ya sekondari Arusha Sayansi, Profesa Nuhu Habibu, amesema changamoto kubwa inayowakabili wabunifu wengi wa wanafunzi ni mwendelezo wa miradi yao baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.
Amesema miradi mingi yenye uwezo mkubwa hupoteza mwelekeo baada ya wanafunzi wanaounda timu kujiunga na vyuo na taasisi tofauti, jambo linalofanya ushirikiano wao kuwa mgumu.
“Wanafunzi wanaweza kubuni miradi mizuri wakiwa shuleni, lakini kuendeleza ubunifu huo baada ya kuhitimu huwa changamoto pale wanapotengana.”
Amewataka wazazi kushirikiana na shule kuhakikisha wabunifu wanaendelea kuwasiliana na kushirikiana ili waweze kuendeleza mawazo yao ya kampuni.
Profesa Habibu ameongeza kuwa makampuni mengi makubwa duniani yalianza kama miradi ya ushirikiano kati ya vijana wabunifu, akisisitiza umuhimu wa kudumisha ushirikiano huo ili kubadili ubunifu wa shuleni kuwa biashara endelevu.
Mbali na Cyclo, wanafunzi hao pia waliwasilisha ubunifu mwingine mbalimbali unaolenga kutatua changamoto za kila siku kwa kutumia teknolojia.
Miongoni mwa ubunifu huo ni mfumo wa taa unaotumia Akili Mnemba (AI), unaowawezesha watumiaji kuwasha na kuzima taa za umeme kwa kutumia simu za mkononi wakiwa mbali.
Mwanafunzi Mohamed Abubakari, mmoja wa wabunifu wa mfumo huo, alisema programu hiyo inaweza kuunganishwa na mifumo ya umeme ya kisasa (smart electrical systems), hivyo kumwezesha mwenye nyumba kuzima au kuwasha taa hata akiwa nje ya makazi yake.
“Teknolojia hii inaokoa muda kwa kuondoa ulazima wa kwenda kuwasha au kuzima taa moja kwa moja. Pia ni msaada mkubwa kwa watu wenye ulemavu ambao wanaweza kudhibiti taa kupitia simu zao bila kutumia swichi za ukutani,” amesema.
Ameongeza kuwa mfumo huo unapunguza upotevu wa umeme unaotokana na watumiaji kusahau kuzima taa wanapotoka nyumbani.
Kundi jingine la wanafunzi lilibuni Mfumo wa Kadi Mahiri ya Maji ‘Smart Water Card System’ unaolenga kuboresha usimamizi wa matumizi ya maji na kupunguza upotevu wake kupitia mfumo wa malipo ya awali.
Kwa mujibu wa mwanafunzi Constantine Dominic, mtumiaji hununua kiwango maalumu cha maji kama ilivyo kwa vocha za simu na kiasi hicho huhifadhiwa kwenye kadi.
“Mtumiaji hujaza kadi kwa kiwango cha maji anachohitaji na kuitumia kwenye mashine ya kuchotea maji. Kwa kugusa kadi kwenye mashine, anaweza kuchagua idadi halisi ya lita anazohitaji. Maji hutoka moja kwa moja hadi kiwango hicho kitakapofikiwa, kisha mfumo husitisha utoaji wa maji,” amesema”
Amesema teknolojia hiyo inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa maji kwa kuwapa watumiaji udhibiti mkubwa zaidi wa matumizi yao.